Menu
in , , , ,

Mambo ya kiufundi kuhusu timu ya Magadascar 

Tanzania Sports

KWA mara ya pili mtawalia, timu ya Taifa ya Madagascar imetinga hatua ya nusu fainali ya Kombe la Mataifa ya Afrika kwa wachezaji wa Ligi za ndani. Ushindi wa Madagascar haukutarajiwa na wengi na pengine hata benchi la ufundi halikuwa na ndoto hizo. TANZANIASPORTS imefanya uchambuzi wa kina kuhusiana na uchezaji wa Madagascar ambao waliwatupa nje wenyeji wenza wa CHAN, Harambee Stars. Je, kiufundi Madagascar ni timu ya aina gani? Hilo ndilo swali linaloulizwa na mashabiki na wachambuzi wengi wa kandanda. 

Kutambua namna ya kutumia mbinu zao

Akizungumza na vyombo vya habari nchini Kenya, kocha Romuald Rakotondrabe alisema “Sisi hatuna Ligi imara kama za Morocco au Tanzania, na hatuna wachezaji wenye viwango bora kama Clement Mzize ambaye anaibeba timu na kuleta matokeo. Lakini tunacheza kwa malengo maalum na umoja kati yetu. Tunacheza kitimu zaidi.

Mojwapo ya sifa muhimu ya kikosi cha Madagascar ni kucheza kwa ushirikiano. Timu hii inacheza katika mtiririko ambao unajuliikana bayana; pasi fupi za haraka, kasi na kutumia nafasi za pembeni. Madagascar wamekuwa wakicheza kitimu ambao unaweza kusema ni wa Kiholanzi yaani ‘total Football’. 

Uwezo binafsi umewekwa kando

Uchezaji wa timu hii unategemea sana muundo wa kiufundi. Ni timu ambayo ina wachezaji wasio na vipaji vikubwa lakini wanacheza kwa ushirikiano mzuri. Mifumo yao inapobadilika kutoka 4-3-3 au 4-2—3-1 au 4-4-2 na 4-5-1 wanakuwa katika msingi uleule wa kucheza kitimu. Ni timu iliyoundwa kutegemeana kuliko kumtegemea nyota mmoja. Uwezo wa wachezaji wake mfano safu ya ushambuliaji hakuna anayweza kumshinda Clement Mzize, lakini ili kulifikia lango la adui wanakuwa wamefika wote, na wanarudi wote kufanya kazi ya ulinzi. Mfumo wao unawafanya wapigiane pasi za haraka na kutawala mchezo kwa muda mrefu. Kwao muhimu ni kupokonya mpira na kuwa upande wao, kisha waanze kupanga mipango.

Kimbinu, si tishio ila usiwadharua

Kimbinu ni timu ya kawaida. Mipango yao mikubwa inategemea jinsi wanavyotumika kulingana na mahitaji ya kocha. Kwa mfano kwenye mchezo dhidi ya Taifa Stars, walipangwa viungo wengi katikati ya dimba kiasi kwamba mshambuliaji wake namba moja aliwekwa benchi. Kazi yao kubwa viungo hao ilikuwa kuwadhibiti Mudathir Yahya, Fei Toto na Yusuf Kagoma. Mchezo wa kupokonya mpira na kumiliki unawapa nafasi ya kupigiana pasi kuelekea lango la adui kirahisi na kucheza kwa mtindo wao. Timu zilizocheza na Madagascar na ambayo haikuwadharau ni Taifa Stars. Timu hii iliwachukulia kwa uangalifu mkubwa kwa sababu iliwafunga kwenye COSAFA. Kwahiyo mchezo baina yao ulionesha ufundi wao.

Udhaifu katika pasi ndefu

Mojawapo ya maeneo ambayo Madagascar ni dhaifu ni katika mipira mirefu (Long balls). Wao wanategemea zaidi pasi fupi fupi kuelekea lango la adui, lakini kila viungo wao wakijaribu kupiga pasi ndefu wanajikuta hawawezi kuzifikia. Mpango huo unawafanya washindwe kufika eneo la tukio kwa haraka kwani wamejengwa katika mfumo wa pasi fupi. Bahati mbaya, Harambee Stars hawakuwa watu wa ‘kutembeza balls’. Viungo wao na washambuliaji ‘boli halitembei’. Hii iliwapa nafasi Madagascar kucheza kwa utulivu, ingawaje walikuwa na makosa mengi ndani ya dimba. Kama kuna timu inacheza pasi ndefu au mipira mirefu basi ni changamoto kwa Madagascar.

Nchi hiyo inafurahia pale inapocheza na wapinzani wanaotandaza boli mguuni na wanapenda kucheza kwa mhezo huo wakiwa na uhuru kuliko zile zinazocheza kinyume chake. Lakini ukicheza nao usiuwadharau.

Heshima kwa wapinzani kuliko uwezo wao

Tangu mwanzo wa mashindano ya CHAN Kocha wa Madagascar Romuald Rakotondrabe alisifia timu mbalimbali kwa kucheza vema hadi kutinga fainali hizi. Katika mazungumzo yake na vyombo vya habari, kocha huyo anaonesha bayana kuwa nchi yao si tishio katika kandanda lakini wanajiandaa kufanya vizuri siku zijazo. Madagascar iliingia mashindano hayo kama timu ambayo haikuwa ikipewa nafasi kubwa, lakini mwalimu wake alikuwa akifanya kazi nzuri kuzungumza na kuwajenga wachezaji kupitia mahojiano yake na vyombo vya habari. Hii ni sababu muhimu inayoleta utulivu kwa wapinzani ambao huwa hawawezi kuhangaika sana kama ambavyo kocha wa Kenya, Benni McCarthy alivyofurahia kupangwa nao kwenye hatua ya robo fainali. Kiufundi kocha huyu hapa anadhihirisha namna bora ya kuzungumza kwenye mikutano.

Kukubali kisasi cha Tanzania

Kwenye mashindano ya COSAFA ya kusini mwa Afrika, Madagascar waliifunga Tanzania 1-0. Taifa Stars ilishiriki mashindano hayo kwama mwalikwa. Hata hivyo kwenye mashindano ya CHAN, Tanzania iliitungua Madagascar 2-1 yaliyofungwa na Clement Mzize. Katika mchezo huo ndani ya dakika 45 Madagascar walijikuta wakizabwa mabao mawili na kuifanya timu yao ishindwe kuwa hodari uwanjani. Kipindi cha pili walijaribu kurudi katika uimara wao wakafanikiwa kupata bao la kufutia machozi. Kwa maana Madagascar ilikuwa tayari na ilitambua alzima ikutane na kisasi. Kwahiyo jukumu la kocha na benchi lake la ufundi walifanikiwa kuiandaa timu katika mazingira ya mapambano. Utayari na uimara wa wachezaji mmoja mmoja ulikuwa kivutio kingine licha ya kupoteza mchezo.

Je wataweza kufua dafu mbele ya Morocco?

Mchezo wa nusu fainali unazikutanisha Morocco na Madagascar. Ni mchezo mgumu kwa pande zote, lakini hadi sasa inaonesha Morocco wana nafasi nzuri ya kushinda mchezo huo. Sababu za Morocco kushinda ni kutokana na uwezo wao walionao katika kandanda na wameitupa nje mbabe wa Madagascar yaani Taifa Stars. Kiufundi Morocco wanaweza kuonekana wana ujuzi na uzoefu mkubwa  mbele ya Madagascar lakini dakika 90 zitazungumza nani ataibuka kuwa mbabe.

Written by Israel Saria

I have been involved with sports in Tanzania as a Volleyball Coach for many years—and was a Tanzania Amateur Volleyball Association (TAVA) leader. I studied sports management at Leipzig University in Germany and understand the science behind sports. That led me to work as a football pundit, with the BBC ( Swahili service) in London. That experience and exposure took me to covering the 2010, World Cup in South Africa. This provided me with a great insight into international level football commentary and the opportunity to carry out extensive research into the game including its players, the stadiums, the rules and tactics.I have also been grateful to meet a wide range of people connected to football in the UK, Tanzania, Germany, Italy, Belgium, Ireland, France, Kenya etc, and visited almost all of the key football stadiums across United Kingdom, and Europe.

Leave a Reply

Exit mobile version