MATUMAINI ya Taifa Stars kuingia kwenye kundi la mtoano (Best loser) kuwania kufuzu fainali za Kombe la Dunia mwaka 2026 yamefifia baada ya kuchapwa 1-0 katika mchezo uliofanyika kwenye uwanja wa Aman visiwani Zanzibar. Wakati Taifa Stars ikinyukwa nyumbani, wenzao Niger waliibuka na ushindi dhidi ya Jamhuri ya Congo. Taifa Stars ilicheza mchezo huo ikiwa na matumini ya kuibuka na ushindi kujiweka katika mazingira ya kushika nafasi ya pili nyuma ya Morocco yenye pointi 21. TANZANIASPORTS inchambua kwa kina juu ya makosa yaliyojitokeza kwa benchi la ufundi la Taifa Stars linaloongozwa na kocha Hemed Suleiman ‘Morocco’. Soma zaidi…..
Injini ya Taifa Stars ilivurugwa
Katika nafasi ya kiungo kocha hajaunda uti wa mgongo, kwa sababu kwenye mchezo huu aliwapanga Yahya Zayd na Khalid Idd na kuwaweka benchi Novatus Miroshi na Yusuf Kagoma. Hili ni kosa ambalo kocha wa Taifa Stars alitakiwa kuwapanga wachezaji wake waliozoea na kucheza kwa muda mrefu katika eneo hilo ili kuimarisha hali ya ulinzi kwa walinzi. Badala yake akapanga wachezaji wapya kwenye eneo gumu ambalo ndilo injini ya Timu. Kosa hili limeigharimu Taifa Stars kwa muda mrefu hadi pale alipoingia Novatus Miroshi hali ya kiungo mkabaji iliimarika na kiungo mshambuliaji tegemeo Feisal Salum alifika eneo la hatari mara nyingi kuliko kipindi cha kwanza. Makosa haya yanaua injini ya timu ambayo haitakiwi kupanguliwa labda pale mchezaji mmoja anapokuwa mgonjwa.
Kukosa nguzo ya Taifa Stars

Hemed Suleiman tangu alipochukua jukumu la kuinoa Taifa Stars hajafanikiwa kuunda uti wa mgongo wa Taifa Stars. Tunaposema uti wa mgongo tuna maana ya wachezaji muhimu ambao wanaunda falsafa yake mfano 8 au 9 katika kikosi cha kwanza. Hawa wachezaji wanakuwa ndiyo nguzo ya timu ambao wanasimama katka mipango ya na mbinu za kocha kwa ajili ya kutafuta ushindi au matokeo chanya.
Ukiangalia namna Taifa Stars ilivyoanza kujengwa, kuitwa wachezaji wan je vijana na wengine unaona bayana kuwa timu ilihitaji mwendelezo kuliko kusambaratishwa. Mfano kiungo chipukizi kama Ben Stackle anayechez asoka huko Uingereza alipaswa kuwa sehemu ya mpango wa kuunda kikosi imara cha Taifa Stars katika eneo la kiungo. Hali kadhalika katika nguzo hiyo alitakiwa kujua wachezaji wake ambao watakuwa sehemu ya msingi ya kuifanya Taifa Stars inakwenda popote kucheza ikiwa na wachezaji wake muhimu. mfano katika safu ya ulinzi Ibrahim Bacca na Dickson Job wamekuwa guzo muda mrefu, lakini mwalimu alifanya mabadiliko na kumpa nahodha Bakari Mwamnyeto kuongoza safu hiyo.
Wawili hao hawajacheza pamoja kwa muda mrefu ingawaje wapo klabu ya Yanga. kazi na nguzo kubwa ya Dickson Job na Baaca imeifanya Taifa Stars kwenye mashindano ya CHAN kufika robo fainali. Hali kadhalika kama kocha alihitaji beki mrefu basi alijidanganya kwa sababu Zambia hawakuwa na mshambuliaji mwenye kimo cha Gaudence Mwaikimba ambacho ungeweza kusema kitawababaisha walinzi wa Taifa Stars. Katika safu ya kiungo pia changamoto ya kocha ni ileile kama ilivyo safu ya ushambuliaji na mawinga.
Kocha hajaweka nguzo yake muhimu nakuifia, kwamba hiyo ndiyo falsafa yake. Katika michezo inakumbukwa kocha mmoja wa KIbrazil amewahi kuwajibu waandishi wa habari waliomuuliza swali kutokana na pendekezo la Rais wa Brazil kumpanga mshambuliaji fulani. Kocha huyo alisema, “mimi sifanyi kazi ya kuteua Baraza la Mawaziri, kwahiyo nategemea pia Rais hatafanya kazi ya kuteua wachezaji wangu wa kucheza,”. Hii maana yake kocha alikuwa tayari kufa na falsafa na mbinu zake ili kuibuka na ushindi.
Pili, kupangua kikosi kila mara
Timu ya Taifa wanacheza wachezaji bora lakini inafaa nini ikiwa kila mechi unakuja na wachezaji wapya ambao wanaingizwa kwenye kikosi cha kwanza huku ukipangua wale ambao wangweza kuwa nguzo ya mfumo wako? Katika eneo hili kocha Hemed Morocco ameshindwa kutengeneza mfumo unaowafaa wachezaji anaohitaji na kuwapanga katika mchezo. Ni wachezaji ambao wanatakiwa kuongezewa nguvu kwa kuwaleta wapya, lakini kupangua pangua bila sababu na kiloa mechi kuwa na wapya katika mfumo mpya unasababisha Taifa Stars kukosa maelewano. Kocha hajatengeneza kikosi cha kwanza ambacho kinadumu na kuongezewa nguvu pale inapotokea mchezaji ameumia au ameshindwa kuendana na mchezo fulani. Hili linasababisha kila mara wachezaji wageni na timu kuanza upya na kukosa maelewano.
Tatu, Kulalamika jambo lilile bila suluhisho.
Kwa muda mrefu kocha Hemed Morocco amekuwa akialamikia kukosa mshambuliaji mahiri. Katika mchezo dhidi ya Zambia aliita washambuliaji wafuatao;- Suleiman Mwalimu na Abdul Suleuman. Wengine waliobaki katika safu ya ushambuliaji ni viungo, mfano Edwin balua, Morice Abraham, Charles M’mombwa na wengineo.
Katika eneo hili kocha anatakiwa kueleza umma ni kwanini analalamika kuhusu mshambuliaji nchini ikiwa ameshindwa kumkabidhi majukumu Kelvin John anayekipiga huko Denmark? Huyu ni mshambuliaji chipukizi na tayari amekuwa gumzo msimu huu huko Ulaya. Ikiwa na maana afanya vizuri kwenye ligi hiyo, lakini kocha hazungumzii vizuri kuhusiana na mchezaji huyo. Ikiwa Kelvin John ana matatizo ni wakati wa makocha kukubali kumlea ili kumsaidia kuimarika zaidi.
Katika ushambuliaji sifa nyingine ni kuvumbua aina ya wachezaji ambao wanaweza kumudu kucheza mfumo wa kocha. Unapokosa mshambuliaji kocha unakuwa na mbinu mbadala kuhakikisha unatumia wachezaji ambao wanaweza kukupa ushindi pale unapokosa namba 9 asilia. Lakini kwenye kikosi cha Taifa Stars, Suleiman Mwalimu ni mshambuliaji ambaye anakipiga klabu ya Simba kwa mkopo akitokea nchini Morocco.
Nne, kukosekana mkakati wa timu
Katika mchezo dhidi ya Zambia, Taifa Stars imecheza mifumo mwili mikuu; 4-4-2 na kurudi 5-3-2. Katika mifumo hiyo inahitaji kuwa na Suleiman Mwalimu ambaye anasimama pale kama mshambuliaji wa mwisho yaani nambari 9. Lakini mshambuliaji huyo alikuwa benchi. Kuandaa mkakati wa timu ni matokeo ya kuwa na nguzo ya timu. Nguzo ya timu inaongezewa nguvu kwa wachezaji ambao wanakamilisha mkakati wa ushindi.
Ikiwa mkakati unaopangwa kila mara unakuw ana wachezaji wapya maana yake kocha hana mkakati wa msingi wa kufa nao ili abakie kwenye njia yake kusaka ushindi. Mkakati unasaidia kuteua wachezaji ambao wanaingia kwenye kikosi cha kwanza ulichonacho ili kuimarisha sio kubomoa mara kwa mara. Kimkakati dhidi ya Zambia Taifa Stars haikuwa na ubora tangu mwanzoni hadi pale ilipoamshwa kwenye kipindi cha pili. Na kwenye mkakati wa timu huwezi kupanga wachezaji wapya ambao wanaanza kuelewana upya na kutofahamiana namna bora ya kuibuka na ushindi.
Tano, nafasi finyu ya ufundi kwa wachezaji
Hapa Uingereza, mojawapo ya jambo lililokuwa linabishaniwa ni nafasi ya Harry Maguire kwenye timu ya Taifa, Three Lions. Lakini aliyekuwa kocha wake Gareth Southgate alisimama kidete kulinda nguzo ya timu yake ili kuhakikisha mpango wa ufundi haubomolewi. Haikuwa rahisi kuona Harry Manguire akiwekwa benchi kwenye kikosi cha Taifa kwa sababu alikuwa mkakati wa kiufundi na nguzo ya timu. Kilichofuata ni maingizo machache kwenye maeneo ambayo mwlaimu aliamua kufanya mabadiliko.
Harry Maguire hakuwa mchezaji chaguo la kwanza katika kikosi cha Manchester United lakini alikuwa muhimu kwa timu ya Taifa ya England na alikuwa mwandamizi na mwenye kuipa maarifa mazuri timu hiyo katika safu ya ulinzi. Nataka kusema nini? Kiufundi kila kocha anakuwa na wachezaji ambao wanalinda nguzo na falsafa yake ili kuwa rahisi kutekeleza majukumu ya kiufundi. Ilikuwa rahisi kuona Maguire, Bellingham, Kyler Walker, Luke Shaw, Kalvin Philips wakiwa waandamizi wa kikosi cha kwanza hata kama hawakuwa wakitamba kwenye klabu zao. Kocha alilinda mkakati wa kiufundi na nguzo ya timu.
Sita, kuwajaribisha wachezaji kwenye mechi ya mashindano
Moja ya mambo yaliyoshangaza kwenye kikosi cha Taifa Stars dhidi ya Zambia ni uamuzi wa kocha kuwajarbisha wachezaji kwenye mchezo muhimu wa kuwania kufuzu fainali za Kombe la Dunia mwaka 2026. Kocha Hemed Morroco alifanya makosa hayo kwa kuingiza wachezaji wapya kwenye mfumo ambao ulitakiwa kutumiwa na wale waandamizi ili wampe uzoefu zaidi.
Lakini kocha aliamua kufanya mabadiliko ya safu ya ulinzi wa kati, safu ya ulinzi wa pembeni na safu ya kiungo mkabaji na kiungo mshambuliaji na kuifanya timu iwe ngeni kuliko walivyokuwa Zambia. Je ni kweli kwamba benchi la ufundi la Taifa Stars halioni makosa hayo? Kitendo cha kuwajaribisha wachezaji kwenye mchezo muhimu ni makosa ambayo Hemed Morocco atakuwa anajutia. Wachezaji wapya walioingizwa walipaswa kupimwa kwenye mchezo wa kirafiki ili kuwaandaa kwenye michezo mingine ya ushindani wakiwa wanaelewa falsafa na msingi wa ufundi wa mwalimu. Kinyume na hilo kocha amejiharibia.