WIKI hii kumekuwa na gumzo kubwa miongoni mwa wapenzi wa michezo, baada ya kushuhudia klabu ya Yanga ikitajwa kutoa mchango wa shilingi Milioni 100 kwenda kwa Chama cha Mapinduzi (CCM). Mchango wa Yanga ni katika Harambee ya CCM kutafuta fedha za kugharamia uchaguzi mkuu utakaofanyika mwezi Oktoba mwaka huu. Yanga ni klabu ya soka, mwanachama wa TFF, CECAFA, CAF na Shirikisho la Soka Duniani FIFA. Kuwa mwanachama Mashirikisho ya soka kuna masharti na taratibu zake. Miongoni mwa masharti ambayo FIFA kama msimamizi mkuu wa mchezo wa mpira wa miguu ni kuagiza wanachama wake kutojihusisha na kampeni za kisiasa.
Kwa mujibu wa taratibu za FIFA kalbu ya Yanga hairuhusiwi kuchangia fedha za kampeni za siasa hivyo kitendo cha kutoa shilingi milioni 100 kwa CCM kinanajisi kanuni na sheria za mpira wa miguu. Kanuni za mpira zinataka wanachama wote wa FIFA chini ya sheria wasichague upande wowote kwani itasababisha kugawa wafuasi wa mpira pamoja na kuleta vurugu zisizo na sababu. Kwa utaratibu huo FIFA inakataza kampeni za kisiasa kwenye mchezo wa soka.
Miongoni mwa mifano ambayo imetokea hivi karibuni ni kitendo cha shirikisho la soka CAF, kutoa adhabu kwa shirikisho la soka la Tanzania, TFF kulipa adhabu ya faini kwa kosa la kukiuka sheria na taratibu kwenye mashindano ya CHAN. TFF iliadhibitiwa kutokana na kitendo cha baadhi ya mashabiki wa soka kuingia uwanjani na mabango yenye picha ya kampeni ya kisiasa. Kwenye mabango hayo yalionesha picha ya Rais wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan na ujumbe wa ‘Oktoba tunatiki’. Licha ya nia ya kuonesha upendo kwa Rais Samia, lakini kanuni na taratibu haziruhusu kampeni za namna hiyo ndani ya viwanja vya soka.
Adhabu kama hizo zimetolewa huko nchini Kenya ambako FKF imetakiwa kulipa faini kutokana na kuvunjua taratibu za soka za mashindano ya CHAN. Kenya ni mwenyeji wa CHAN kama ilivyo kwa Tanzania na Uganda.
Wakati mashabiki wa soka wakiwa na kumbukumbu ya kuadhibiwa kwa shirikisho lao la mpira wa miguu, uongozi wa Klabu ya Yanga ukafanya makosa mengine ya kuvunja sheria za FIFA kwa kushiriki kampeni za siasa kwenye harambee ya CCM. Inafahamika kuwa viongozi wa vyama vya soka wanaweza kuwa na shughuli zao nyingine za kisiasa, lakini wanapaswa kufuata sheria na miongozo inayotolewa na FIFA. Kwenye tukio la klabu ya Yanga kutoa fedha hizo, kumesababisha hasira kali kutoka kwa mashabiki mbalimbali wa klabu hiyo.
Kwa kuwa mchezo wa soka unawaleta pamoja watu wenye itikadi tofauti ya vyama vya siasa, wengi hawapendi kushuhudia siasa zikiingizwa kwneye timu zao. Kitendo cha Yanga kimesababisha hasira za mashabiki wake ambao hawajali kuhusu mrengo wa chama cha siasa. Baadhi ya warekodi video mbalimbali wakiwa anachoma moto jezi za Yanga kwa hasira huku wakimimina rundo la matusi na kejeli dhidi ya Rais wa klabu hiyo Eng. Hersi Said na Arafaf Yusuf.
Katika mazingira hayo uongozi wa klabu ya Yanga ulitambua makosa yake, na kwamba walifanya kazi ya kuwagawa mashabiki kisiasa kinyume cha sheria za FIFA. Yanga walilazimika kutoa taarifa kwa umma kwa kuomba radhi kwa kitendo hicho pamoja na kufafanua zaidi.
Bahati mbaya zaidi Yanga wamefanya kosa lingine la kisheria kwa kueleza kuwa shilingi milioni 100 zilizotangazwa siku ya harambee zimetolewa na Taasisi binafsi ya GSM Foundation kama mchango wake kwa CCM. Taasisi hiyo ni mali ya kampuni la GSM ambaye ni mfadhili wa klabu ya Yanga.
Kulingana na sheria za usajili wa asasi za kiraia GSM Foundation hawaruhusiwi kushiriki katika kampeni za kisiasa. Usajili wa taasisi ya GSM Foundation umejikita katika maeneo mawili; elimu na afya na ipo chini ya sheria ya asasi za kiraia ya mwaka 2021 (ambayo pamoja na mambo mengine inatamka ni marufuku kujihusisha na shughuli za kisiasa). Kwahiyo taarifa iliyotolewa na Yanga kueleza kuwa haikushiriki harambee ya kampeni ya kisiasa katika uchaguzi mkuu ni kosa na imejitumbukiza kwenye ushahidi zaidi. Hilo lilikuwa kosa la pili kwa Yanga.
Kosa la tatu ni kushindwa kutenganisha ufafanuzi wa shughuli za GSM Foundation na Yanga. Kosa hili limefanyika na linaweza kutumika kama kielelezo cha kuadhibiwa. GSM Foundation walitakiwa kujitokeza na kutoa ufafanuzi kuhusiana na utoaji wa fedha kiasi cha shilingi milioni 100 kwa ajili ya kusaidia CCM.
Kama makosa ya kisheria ya usajili wake, GSM Foundation walitakiwa kukamatwa wenyewe bila kuhusisha taasisi ya Yanga. Kwa maana hiyo makosa hayo matatu yanaifanya Yanga kuwa kwenye shinikizo la kuadhibiwa. Ni makosa ya dhahiri ambayo viongozi wake wanatakiwa kujiandaa kujitetea iwapo CAF na FIFA wataingilia kati kufanya uchunguzi. Uzuri ni kwamba CAF wapo hapa nchini kwa ajili ya mashindano ya CHAN, kwahiyo kila jambo wanaliona, na watawajibika kutoa ushirikiano kwa FIFA.
Makosa kama haya uongozi wa Yanga ulitakiwa kuyaona na kutambua kuwa ni mahali gani sheria inaelekeza nini na wapi wanatakiwa kutogusa. Hivi leo Yanga imegeuzwa kuwa msemaji wa GSM Foundation katika suala ambalo wanalalamikiwa. Hali kadhalika GSM Foundation nao wamefanya kosa badala ya kujitokeza wanaliacha liende kwa Yanga na kuzidi kugombanisha taasisi hizo na mashabiki.


Comments
Loading…