Mashindano ya CHAN yanayoendelea katika nchi tatu za Kenya, Tanzania na Uganda yameibua wachezaji wakali ambao wamekuwa gumzo hadi sasa. Wakati nchi zikiingia katika hatua ya robo fainali, wapo nyota ambao wametumia vema nafasi zao kuwakilisha wenyeji wa CHAN. TANZANIASPORTS inachambua na kuhitimisha kuwa nyota watatu wamekuwa wakibeba majukumu makubwa ya timu zao hadi sasa.
ALLAN OKELLO
Uganda Cranes walicheza mchezo wao wa mwisho wa kundi dhidi ya Afrika kusini na kwa mara nyingine nyota huyu mwenye umri wa miaka 25 alionesha umahiri mkubwa. Akiwa anavalia jezi nambari 21 mgongoni, utulivu wake anapokuwa na mpira au bila mpira inamfanya awe kivutio kwa uchezaji wake. Allan Okello anaweza kucheza nafasi ya winga wa kulia, winga wa kushoto, na mshambuliaji wa pili yaani namba 10. Katika kikosi cha Uganda Cranes, nyota huyu amekuwa akitumika kama kiungo huru ambaye anaanzisha mashambulizi akitokea upande wa kulia au katikati kuelekea lango la adui. Ni nyota ambaye anapewa mpira nje ya 18 ili apange mipango ya mashambulizi langoni mwa adui., ni mchezaji ambaye anafaa kucheza katika mfumo 4-3-3 na 4-5-1 ambayo humfanya kuwa namba 10 mwenye jukumu la kurahisisha kazi iliyofanywa na viungo wakabaji na hivyo kumpa wakati mzuri zaidi mshambuliaji kupachika mabao. Mipango mingi ya Uganda ilikuwa inaanzia kwenye miguu ya Allan Okello.
FESAIL SALUM
Kwa utani unawez akumwita jina la Fei Toto. Ukitaka kuona utulivu wa Taifa Stars basi mtazame kiungo huyu. Ni nyota ambaye anaweza kusaiudia ulinzi, kushambuliaji, na kuituliza timu pale inapokuwa kwenye shinikizo kubwa la kushambuliwa au kushambulia. Chini ya uongozi wa Feisal Salam, Taifa Stars inapewa maelekezo mahali pa kushambuliaji. Anaweza kwenda upande wa kulia akamtayarishia kazi nzuri beki wa kulia Shomari Kapombe. Ama anaweza kwenda upande wa kushoto akamtayarishia akzi Iddy Nado. Pia anaweza kuwa katikati ya dimba akapokonya mipira au kutengeneza mashambulizi. Anaweza kuliandamana lango la adui kwa kupiga mashuti makali langoni. Ni kiungo ambaye anaonekana kila mahali. Anaweza kuwa kiungo mkabaji, wakati huo anakuwa kiungo mshambuliaji, pia winga kulia au kushoto, na wakati mwingine akiwa eneo na ushambuliaji. Feisal Salum ni silaha ambayo inalindwa na Mudathir Yahya katika eneo la kiungo. Nyota huyu ndiye anabeba silaha za kushambulia za Taifa Stars.
AUGUSTINE ODHIAMBO
Utawaambia nini wakenya wakuelewe? Huyu ni miongoni mwa wachezaji wanaompa kiburi kocha Ben McCarthy raia wa Afrika kusini na nyota wa zamani wa vilabu mbalimbali vya Ulaya. Odhiambo ndiye mchezaji anayerahisisha kazi ya Harambee Stars. Tangu mwanzo wa CHAN, wakati Harambee Stars ikiwa inasaka bao la kwanza iliwachukua muda mrefu kuja kuwatungua wapinzani wao. Mtungaji wa bao hilo ni nyota huyu. Je Odhiambo ana ubora gani? Jambo la kwanza huyu ni mhezaji anayefaa kwenye mifumo miwili 4-3-3 au 3-5-1-1 kwa kuwa hana kasi kubwa lakini ana maarifa makubwa akiwa lango la adui. Pia ni mchezaji ambaye anaweza kutengeneza mabao, ubora katika utoaji wa pasi za mwisho na jinsi anavyoivuta timu katika eneo la hatari. Kiufundi anafaa kucheza nambari 10 ama mita tano kutoka eneo la 18 la adui pale timu inaposaka bao. Ushahidi wa mbinu hii umetumika mara nyingi, huwa anasimama kwenye kona ya kulia ya uwanja kwenye 18, ambapo anao uwezo wa kumtazama vizuri golikipa. Kazi yake ni kutembea nje ya mstari wa 18. Ni kama anazurura hivi, lakini anakuwa na jukumu la kupokea pasi na kujaribu kufunga bao au kutengeneza mabao akiwa kwenye mstari huo. Kwa vile ana ubora wa kutumia mguu wa kushoto, inamwezesha kupiga pasi zenye macho makali ambazo zinawahadaa wapinzani. Huyu ni nyota ambaye anayafanya maisha ya Harambee Stars kwenye CHAN yawe mazuri hadi kutinga hatua ya robo fainali. Iwe amefunga au hajafunga lakini anaifanya Kenya iwe na matumaini makubwa anapokuwa uwanjani.
CLEMENT MZIZE
Mabao mawili muhimu katika mechi tatu, yameonesha ukubwa wake katika soka. Yameonesha umahiri wake katika ufungaji wa mabao. Ameonesha sababu za matajiri wa vilabu mbalimbali kumfukuzia kijana huyu kutoka kwa mabingwa wa soka wa Ligi Kuu, Yanga. Mshambuliaji huyu ana kasi, chenga, mashuti makali na anaweza kucheza eneo lolote katika safu za mbele. Kocha Hemed Suleiman anaweza kumpanga katika winga ya kulia au kushoto, pia anaweza kumpa jukumu la kuwa mshambuliaji wa pili yaani namba 10 au mshambuliaji namba 9. Anaweza kucheza katika mifumo ya 4-4-2, 4-3-3 na hata 5-4-1 kama mshambuliaji pekee pale mbele anamudu. Siri kubwa ya nyota huyu ni kuwafanya mabeki wa timu pinzani kuwa macho muda wote. Ana madhara makubwa bila kujali aina ya mabeki.
KAKANDE
Kimo chake kinaweza kukufanya umpuuze. Ni mchezaji mfupi ana, pengine unaweza kumlinganisha na kimo cha aliyekuwa staa wa Taifa Stars Mrisho Ngassa au beki wa kulia wa Yanga, Kibwana Shomari. Kakande ni kiungo mshambuliaji wa Uganda Cranes. Ni winga wa kulia, pia anamudu namba 10 na winga wa kushoto. Ana kasi, chenga na uwezo wa kulifanya lango la adui lionekane nyanya. Sifa kubw aya uchezaji wake ni uwezo wa kuipeleka Cranes kwa kasi kwenda lango la adui. Mashambulizi mengi ya Uganda yanatayarishwa na Kakande akisadiana na Allan Okello. Huyu ni mchezaji ambaye ana nguvu, maarifa na uwezo wa kuichachafya ngome ya adui.
SSEMUGABI
Uganda Cranes ina kipaji kizuri sana. kama umewahi kumwona nyota wa zamani wa Simba, Jean Baleke basi unaweza kumlinganisha na Ssemugabi. Tofauti ya nyota hawa ni kwamba Ssemugabi ana nguvu nyingi kumzidi Jean Baleke. Pia Ssemugabi ana kasi ya mchezo pamoja na kumudu nafasi nyingi katika safu ya ushambuliaji.
Wakati Uganda ilipokuwa inatafuta bao la kuongoza dhidi ya Afrika kusini, miguu yake iliongea kwa kupachika bao safi kutokana na pande murua toka kwa Kakande. Ssemugabi, ni mchezaji anayemudu kucheza nafasi ya ushambuliaji (namba 9), winga wa kulia au kushoto, na mshambuliaji wa pili. Ssemugabi akimaliza mashindano ya CHAN bila shaka yoyote ataondoka katika Ligi ya Uganda. Huyu ni mshambuliaji ambaye anaweza kutumika katika mifumo ya 4-3-3 na 4-5-1. Kwa sababu ya kasi yake na kimo inamwezesha kusimama pale mbele kama mshambuliaji peke yake huku viungo wa pembeni wakikamilisha kazi ya kumlisha krosi na pasi za kawaida. Anaweza kufunga mabao kwa krosi (vichwa), kupiga mashuti, na kutengeneza mabao dhidi ya wapinzani wao.


Comments
Loading…