Shekhan Khamis karafuu ya Kizanzibari ndani ya Taifa Stars..
KIUNGO mkabaji Pipino Junior alikuwa ameathiriwa na uamuzi mbovu wa refa wa mchezo kati ya Tanzania na Mauritania. Mwamuzi alishindwa kuwaadhibu wachezaji wawili waliokuwa wanamzingira Pipino na hivyo mmojapo kumgonga kiwiko kwenye jicho la kulia la nyota huyo. Kitendo hicho kilisababisha jicho hilo likose kuona vyema. Ili mchezaji afanye kazi vizuri inabidi macho yake yawe vizuri. Pipino alishindwa kuendelea na mchezo.
Pamoja na hilo, ujio wa mchezaji aliyechukua nafasi yake ulikuwa tofauti. Benchi la ufundi la Taifa Stars lilihitaji kiungo mkabaji ambaye Pipino alichukua nafasi yake. sababu ya Pipino kuchukua nafasi ya Yusuf Kagoma ilikuwa ni kutokana na hofu ya benchi la ufundi kumkosa nyota huyo.
Mara kadhaa mwamuzi wa mchezo alimpa onyo Yusuf Kagoma kutokana na kucheza madhambi mara kadhaa. Katika hatua ya kumlinda kwa michezo ijayo, benchi la ufundi ndipo likamwingiza Pipino. Hata hivyo haikuwa siku nzuri kwake, alifanya makosa kadhaa binafsi. Hata hivyo kilichomtoa nje ya uwanja ni kutokana na kuchezewa madhambi huku mwamuzi wa mchezo akishindwa kuona. Mchezaji aliyeingia ndiye amezua gumzo zaidi miongoni mwa mashabiki.
Kwanini Shekhan amekuwa gumzo?

Shekhan Khamis
Shekhan Khamis ni kipaji kingine kinachoendelea kukua na kiliingia na kuonesha umahiri ambao mashabiki wanazidi kuvutiwa nacho. Wakati Pipino akitolewa nje wengi walitegemea benchi la ufundi la Taifa Stars lingemwingiza kiungo mkabaji mwingine ama kumfanya beki au kiungo mshambuliaji Feisal Salum kwenda kuziba pengo la namba 6 kwa sababu Yusuf Kagoma alishatolewa dimbani.
Kocha Hemed Suleiman na wasaidizi wake Jamhuri Kihwelo na Juma Mgunda walikuwa na akili nyingine kabisa ya kiufundi kwani walimwingiza Shekhan Khamis. Wakati mashabiki wakitazama kwa jicho la kishabiki na furaha, benchi la ufundi lilikuwa na jicho la aina yake.
Kimbinu Mauritania walikuwa wakicheza mchezo wa kushtukiza na kutumia mbinu ya kujiangusha na kupata faulo nyingi ili kupunguza kasi ya Taifa Stars. Kocha wa Mauritania inaelekea alifanya ‘home work’ vizuri kwa kuisoma Taif Stars kisha akajaza viungo wengi ili kupunguza kasi ya vijana wa Hemed Suleiman ‘Morocco. Ni dhahiri benchi la ufundi la Mauritania lichunguza umahiri wa kiufundi wa kikosi cha Taifa Stars.
Katika mchezo wa pili huu Taifa Stars ilikuwa na jukumu la kuhakikisha inaibuka na alama tatu pamoja na kuwadhihirisha wale wenye mashaka kuwa mchezo wa kwanza ulikuwa mzuri upande wao. Ushindi wa bao 1-0 dhidi ya Mauritania umeipa Taifa Stars pointi 6 na kuongoza kundi lake.
Jicho la kiufundi alichoagizwa Shekhan na benchi la ufundi?
Jina la Shekhan Khamis ni miongoni mwa yaliyochanua katika mchezo huo. Shekhan alikuwa mchezaji aliyeingia kutokana na uamuzi bora wa benchi la ufundi. Uamuzi ambao ulikuwa na unalenga kuwaskuma zaidi nyuma timu nzima ya Mauritania. Huyu ni mchezaji ambaye anaweza kucheza nafasi zote za ushambuliaji na winga. Alianza soka huko visiwani Zanzibar katika klabu ya JKU kabla ya kujiunga na mabingwa wa Soka wa Tanzania, Yanga. Yanga walimsajili nyota huyo na kumwanzisha katika kikosi chao cha pili kabla ya kumhamishia timu ya wakubwa. Shekhan Khamis ana umri wa miaka 22 kwa sasa. ni kinda mwenye uwezo mkubwa wa kutumia mguu wa kushoto.
Mara baad aya kuingia dimbani mambo kadhaa yalibadilika. Kwanza winga wa kushoto wa Mauritania alilazimika kurudi nyuma kusaidia ulinzi akishikiriana na El Mami. Kitendo cha winga wa Mauritani kurudi nyuma kilimpa nafasi Shomari Kapombe kupandisha mashambulizi. Wakati huo Shekhan alikuwa akicheza wingi ya kulia, ambako alimtetesha vilivyo mlinzi wao wa kushoto.
Jukumu la Shekhan lilikuwa kuongeza mashambulizi langoni mwa Mauritania. Benchi la ufundi lilimwagiza kushambulia akitokea kulia kuingia katikati kwenye eneo la kiungo. Shekhan alikuwa akitokea upande huo na kukaribia mita tano kutoka kona ya mstari wa 18. Mara nyingi alikuwa akaungana na kiungo mkabaji mpya baada ya Pipino kutolewa. Kiungo aliyecheza namba 6 alikuwa Feisal Salum na kwa vile alipednelea kushiriki jukumu la kiungo mshambuliaji ikawa rahisi kwa Shekhan kupokea pasi na kuachia haraka. Uwezo wa Shekhan kukokota mpira na kasi ni vitu ambavyo vimeongezeka tofauti na alivyokuwa anasajiliwa kwa mara ya kwanza Yanga. Shekhan ana mikimbio na mpira unaka mguuni (boli linatembea).
Uwezo wa kupokea pasi, kuachia, kufungua nafasi, kulazimisha na kuwapa shinikizo walinzi ndicho kitu kilichosababisha benchi la ufundi la Mauritania kumtoa nje winga wao wa kushoto ili kuongeza ulinzi. Shekhan alikuwa na wakati mzuri zaidi na kuonesha aliingia kutekeleza majukumu ya walimu. Jinsi anavyoachia mpira haraka, anavyofungua nafasi, kutafuta nafasi, jinsi anavyoweka mwelelekeo, kuivuta timu kwenda kushambulia, na kifupi alikuwa anatia vikorombwezo vingi hadi beki zao zikawa zinazidiwa kwa presha. Uchezaji huu ndiyo unapaswa kuwa na maana kubw aya mchezaji wa akiba. Mchezaji ambaye amepewa maelekezo kutokana na kuwaona wapinzani wakati mchezo unaendelea. Shekhan alifanya majaribio kadhaa langoni mwa Mauritania, na huenda ubao ungesoma jina lake kwa bao.
Jinsi Taifa Stars walivyopata bao ni ushahidi kuwa mchango wa Shekhan ulikuwa mkubwa. Viungo na mabeki wa Mauritania walikuwa wanehesabu dakika za mwisho wakiamini mchezo huo utamalizika wakiwa na alama moja. Lakini shinikizo dhidi yao liliongezeka kwani Shekhan alimfanya Shomari Kapombe awe na uhuru zaidi kwa sababu beki za Mauritania hazikuwa na nguvu kukabiliana na nyota huyo wa Kizanzibari. Matokeo yake ni bao la Shomari Kapombe lililotokana na kazi nzuri ya timu, huku krosi ya Iddy Nado ikidhihirisha sababu za kuwa panga pangua kikosi cha Taifa Stars.
Akiwa na umri miaka 22 tu, Shekhan ana vitu vingi vya kuwafurahisha mashabiki na benchi la ufundi. Na kama mawakala wa soka wanamechukua ‘notes’ basi huyu ni kinda ambaye hatamaliza msimu mmoja Yanga.


Comments
Loading…