in , ,

LUIS ENRIQUE NI MTU SAHIHI KWA CHELSEA, ILA CHELSEA SI MAHALA SAHIHI KWAKE

Kipigo cha aibu cha 4-1 dhidi ya Chelsea kutoka kwa Watford juzi Jumatatu kiliashiria msumari wa mwisho kabisa wa ndoto za Chelsea za kujaribu kutetea taji lao la Ligi Kuu ya England msimu huu. Sasa kuna pengo la alama 19 kati yao na vinara Manchester City zikiwa zimebaki raundi 12 tu za msimu huu.

Lengo kuu walilo nalo sasa ni kuhakikisha wanasalia kwenye nafasi nne za juu ili kushiriki michuano ya Ligi ya Mabingwa Ulaya msimu ujao. Hapa pia kuna vita kali mno. Wanahitaji kupambana na vigogo wengine wote wa EPL ukiwatoa Manchester City wanaoonekana kuwa salama mno.

Ripoti zinapendekeza kuwa Antonio Conte yuko kwenye hatari ya kutupiwa virago. Muitaliano huyu ameiongoza Chelsea kushinda michezo miwili tu kwenye michezo kumi ambayo Chelsea wamecheza kwenye mashindano yote kwa mwaka huu 2018. Wameshindwa kupata bao kwenye michezo minne kati ya hiyo.

Wiki mbili zijazo atakutana na FC Barcelona kwenye mchezo wa raundi ya 16 ya Ligi ya Mabingwa Ulaya kisha kuwatembelea Manchester United ndani ya Old Trafford kwenye mchezo wa EPL. Lolote linaweza kumtokea Antonio Conte iwapo timu itapata matokeo mabaya kwenye michezo hiyo.

Hata hivyo ripoti zaidi zinaarifu kuwa Chelsea hawatamtimua Conte iwapo hatawaweka Chelsea kwenye hatari ya kukosa nafasi nne za juu. Lakini uwezekano wa kubakia kwenye klabu hiyo kwenye msimu ujao ni mdogo mno kwa namna yoyote ile. Yeye pia anaonekana kuchoshwa na migogoro kati yake na bodi.

Mameneja kadhaa mashuhuri wanahusishwa na kuchukua mikoba ya Muitaliano huyo endapo atatimuliwa au kuondoka kwa namna nyingine hivi karibuni au baadae. Wamo Massimiliano Allegri wa Juventus na Maurizio Sarri wa Napoli. Limo pia jina la meneja aliyewongoza FC Barcelona kushinda mataji 9 ndani ya misimu mitatu aliyokuwa nao kabla ya msimu huu. Huyo ni Luis Enrique.

Falsafa ya ki-Barcelona iliyomjenga meneja huyu akiwa mchezaji na baadae meneja inaweza kumuongoza vyema kupata mafanikio kwenye ligi yoyote ulimwenguni. Madai kuwa aina ya mpira unaochezwa na Barcelona hauwezi kutawala ndani ya EPL ni madai ya kupuuzwa vikali. Tayari yameshazikwa na mambo yanayofanywa na Guardiola ndani ya ligi hiyo.

Ukiachilia mbali uwezo wake wa kimbinu, Luis Enrique ana uwezo mkubwa wa kushinda heshima za wachezaji wake na kuwafanya wawe tayari kumpigania kwa namna yoyote. Jinsi alivyoweza kumaliza tofauti kati yake na Lionel Messi walipoingia kwenye mgogoro akiwa kati kati ya msimu wake wa kwanza ndani ya Barcelona ni ushahidi tosha kwenye hili.

Hata hivyo mshindi huyo wa tuzo ya Kocha Bora wa Mwaka wa FIFA ya 2015 yupo kwenye mapumziko ya mwaka mmoja baada ya kuachana na Barcelona msimu uliopita. Kumpata kwenye kipindi hiki si rahisi, hivyo Chelsea watalazimika kutafuta kocha wa muda iwapo watamtimua Conte kabla ya kuisha kwa msimu.

Kwa upande wake Luis Enrique iwapo atavutiwa na kibarua hiki ni lazima atambue kuwa Chelsea si mahala sahihi kwake iwapo anahitaji heshima kama meneja. Amedumu na Barcelona kwa misimu mitatu na kuondoka kwa uamuzi wake mwenyewe huku klabu ikimpatia heshima kubwa. Nafasi ya kupata heshima ya namna hiyo ndani ya Chelsea ni finyu.

Chelsea huwa haiwapi mameneja wake heshima wanayostahili. Yaliyowakuta Carlo Ancelotti, Roberto di Matteo na Jose Mourinho yanatoa funzo la maana. Ukiwa meneja wa Chelsea unafanya kazi kwenye mazingira magumu mno ya kuhofia kufungashiwa virago muda wowote mambo yanapokwenda vibaya.

Sera ya usajili ya Chelsea inapafanya Stamford Bridge kuwa mahala pasipo na utulivu kwa meneja yeyote. Antonio Conte amekuwa akilalamika mara kadhaa kuwa hana mamlaka ya kutosha kwenye swala la usajili. Asilimia kubwa ya maamuzi huwa yanafanywa na bodi. Hiki ndicho chanzo kikubwa cha mgogoro kati yake na bodi na pia kimechangia matokeo mabovu ya Chelsea msimu huu.

Chelsea wanaweza kufaidika iwapo watampata Luis Enrique. Ni mtu sahihi mno kwao anayeweza kuwaongoza vyema kwenye vita dhidi ya Pep Guardiola, Jose Mourinho na wakali wengine. Hata hivyo Chelsea si mahala sahihi kwa Enrique. Anahitaji kuwa na moyo wa chuma kufanya kazi kwa furaha na utulivu ndani ya Stamford Bridge.

Report

Written by Kassim

What do you think?

71 Points
Upvote Downvote
Tanzania Sports

MWILI WA CONTE UNAONESHA KESHO YAKE

Tanzania Sports

YAFUATAYO NI MAKOSA YA BAKAYOKO