in , , ,

Liverpool wamtenga Suarez


*Wenger akaa mkao wa kumpokea Arsenal
*Fabregas awakataa Man U, kubaki Barca
*England watangaza timu mpya ya taifa
*Ronaldo wa Madrid awatandika Chelsea

Sakata la mchezaji nyota wa Liverpool, Luis Suarez limechukua sura mpya, baada ya kocha Brendan Rodgers kumtenga na kumwambia atafanya mazoezi peke yake.
Rodgers anang’ang’ania mfungaji wao huyo bora wa msimu uliopita abaki Anfield licha ya kutakiwa Arsenal, ambako anakotaka kwenda.
Rodger anadai kwamba Suarez ameonesha utovu mkubwa wa nidhamu kwa kung’ang’ania kuondoka licha ya klabu kumpa kila alichotaka na kumuunga mkono wakati wa matatizo.
Pamoja na kwamba alisema ameumia mguu hivyo asingekuwa na timu kwenye mechi ya kirafiki, Rodgers amethibitisha kwamba atajifua kivyake ili awe fiti na atachukua hatua muhimu za kinidhamu dhidi yake.
Wakati hayo yakijiri, Kocha wa Arsenal, Arsene Wenger anasema amekaa mkao wa kumsajili mchezaji huyo wakati wowote, lakini akakiri kwamba usajili wa msimu huu umekuwa mgumu kuliko ilivyowahi kutokea.
Liverpool ameviambia vyombo vya habari kwamba Liverpool walimwahidi angeondoka msimu huu iwapo klabu haingefuzu kwa Ligi ya Mabingwa, lakini Rodgers anasema ni uongo, hapakuwapo ahadi wala hawajavunja makubaliano yoyote.
Washika Bunduki wa London walitoa ofa mbili zilizokataliwa, ya pili ikiwa ni ya pauni 40,000,001, ikilenga kugusa kipengele kinachosema timu ikitoa ofa ya zaidi ya pauni milioni 40, Suarez anatakiwa kujulishwa.
Liverpool wanadai kinasema tu kujulishwa lakini si kuuzwa, na kwamba ofa ya Arsenal ipo chini kuliko thamani ya raia huyo wa Uruguay, ambaye Rodgers anadhani ana thamani ya hata pauni milioni 55 kama Edinson Cavani.
Wenger anasema anasubiri tu kitakachoamuliwa na Liverpool na kwamba ni Suarez na klabu yake tu wanaoweza kuamua hatua inayofuata.
Suarez alitarajiwa kuwasilisha barua rasmi ya kutaka kuondoka, ikishindikana atatumia mahakama au Chama cha Wanasoka wa Kulipwa ili asaidiwe kuondoka Anfield alikopachoka.

FABREGAS AWAKATAA MAN UNITED

20130724-123807.jpg
Kiungo nyota wa Barcelona, Cesc Fabregas amewakata maini Manchester United, baada ya kusema kwamba anataka abaki Camp Nou.
Kocha David Moyes na Mashetani Wekundu walipata matumaini hivi karibuni, baada ya kocha wa Barca, Carlo Ancelotti kudai kwamba hatima ya Fabregas kwenda au kutokwenda Man U ipo mikononi mwa mchezaji huyo mwenyewe.
Man U wamehangaika kutoa zaidi ya dau moja kumng’oa nahodha huyo wa zamani wa Arsenal hapo Camp Nou, lakini ameonekana kutaka kubaki katika klabu iliyomkuza kupitia La Masia – Barca wanakofunza watoto na vijana.
Dau la mwisho la United lilikuwa pauni milioni 30.7, ambalo lingevunja rekodi ya klabu hiyo, lakini Fabregas (26) anasema ndoto yake tangu akiwa mtoto ni kung’aa na Barca na kwamba ana furaha hapo, hata kama hana uhakika wa namba kikosi cha kwanza.
Anasema amezungumza na Makamu wa Rais wa Barecola, Josep Bartomeu, Rais Sandro Rosell na kocha mpya, Gerardo Martino ‘Tata’ na kuwaeleza anataka kubaki, na wao pia wanataka abaki.

ENGLAND WATANGAZA KIKOSI KIPYA

Kocha Mkuu wa Timu ya Taifa ya England, Roy Hodgson ametangaza kikosi chake, safari hii akimwita mshambuliaji Rickie Lambert wa Southampton.
Kikosi hicho ni mahsusi kwa ajili ya kuchuana na ndugu zao wa Scotland, ambapo Wayne Rooney anayetaka kuondoka Manchester United amejumuishwa, licha ya kutoshiriki mechi nyingi za kujiandaa kwa msimu mpya kutokana na majeraha.
Winga wa Manchester United, Wilfried Zaha amepandishwa kutoka timu ya taifa ya vijana chini ya miaka 21 na kuingia kwenye kikosi hicho pia.
Lambert (31) alichezea klabu za Macclesfield, Stockport, Rochdale na Bristol Rovers kabla ya kujiunga na Southampton iliyokuwa ikicheza League One Agosti 2009 kwa dau la pauni milioni moja .
Magoli ya mshambuliaji huyo ndiyo yaliisaidia klabu hiyo ya pwani ya kusini mwa England kupanda madaraja hadi Ligi Kuu msimu uliopita, lakini wadau walishangaa kwa nini hakuitwa timu ya taifa.
Msimu uliopita alimaliza ligi akiwa mfungaji mwenza bora Mwingereza kwenye ligi, akiwa na mabao 15 sawa na Frank Lampard.
Kikosi cha England kina magolikipa Ben Foster, Joe Hart na John Ruddy.
Walinzi ni Leighton Baines, Gary Cahill, Ashley Cole, Phil Jagielka, Glen Johnson, Phil Jones, Chris Smalling na Kyle Walker.
Hodgson ameteua viungo Michael Carrick, Tom Cleverley, Steven Gerrard, Frank Lampard, Jack Wilshere, James Milner, Alex Oxlade-Chamberlain, Theo Walcott, Ashley Young na Zaha.
Wapachika mabao ni Jermain Defoe, Lambert, Rooney na Danny Welbeck.

CRISTIANO RONALDO AWANYOA CHELSEA

Chelsea wamepata kipigo cha mabao 3-1 katika mechi ya kirafiki dhidi ya Real Madrid iliyofanyika Miami, Marekani.
Katika mechi hiyo, nyota wa Madrid, Cristiano Ronaldo alimwadhibu kocha wake wa zamani, Jose Mourinho kwa kufunga mabao mawili.
Mourinho ‘The Only One’ anasema Real Madrid walistahili kushinda, kutokana na makosa ya timu yake, ambapo Ronaldo alimtengea Marcelo aliyefunga bao la kwanza.
“Kwangu mimi ni sawa kabisa kwa makosa tuliyofanya ili tuweze kuyafanyia kazi…kama nilivyosema wiki iliyopita tulipata ushindi katika mechi tano lakini hatuna hata pointi moja.
“Sasa tuna ushindi mara tano na kushindwa mara moja na pia hatuna pointi, hakuna cha ajabu, wao wanacheza La Liga, sie EPL, ingekuwa tumekutana kwenye Ligi ya Mabingwa wakatufunga, yangekuwa mengine,” Mourinho aliuambia mtandao wa Chelsea.

Enhanced by Zemanta

Report

Written by Israel Saria

For the last 20 years I have been working as a football pundit. This experience has provided me with a very useful insight into football and the opportunity to carry out extensive research into the game including its players, the stadiums, the rules and tactics and I have also been grateful to meet a wide range of people connected to football in the UK, Tanzania, Germany .....

What do you think?

71 Points
Upvote Downvote

Comments

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Loading…

0

Barcelona wamtaka David Luiz

Liverpool ndio wanajua ubaya wa Suarez?