in , , ,

Liverpool: Machungu kuvuliwa ubingwa UCL

Mdororo wa mwenendo wa Liverpool kwenye soka kuelekea mwishoni mwa msimu wa 2019/2020 umeanza kuacha maswali kwa wadau, maswali yakiwa mengi kuliko majibu.

Liverpool waliokwenda mechi 18 bila kufungwa kwenye Ligi Kuu ya England (EPL) na pia kuchanja mbuga kwenye Ligi ya Mabingwa Ulaya (UCL) wameanza kuchechemea wakati zikiwa zimebaki mechi chache.

Iwe ni kuchoka, kuishiwa mbinu mpya na ubunifu kwa kocha wao, Jurgen Klopp au timu pinzani kumaizi mbinu walizokuwa nazo na sasa kuziba mianya ya kasi ya washambuliaji, kuwadhoofisha viungo na kufumania nyavu zao, ukweli ni kwamba Liverpool wamechoka, walau kwa sasa.

Baada ya kuwa wamefungwa bao 1-0 na Atletico Madrid kwenye mechi ya mkondo wa kwanza ya UCL jijini Madrid, usiku wa kuamkia Alhamisi hii ulikuwa zaidi ya mchungu kwa Klopp, wachezaji na washabiki nyumbani kwao Etihad, baada ya kukubali tena kichapo cha 3-2 kwenye mechi ya marudiano.

Kwa kawaida ya jinsi hali ya hewa inavyokuwa kwenye dimba hilo usiku wa mechi za UCL, nguvu na kasi ya wachezaji wake kila idara, uimara wa kocha baada ya kukisuka vyema kikosi na ushangiliaji wa aina yake wa washabiki, ulitarajiwa uwe usiku wao.

Watabiri wengi walidhani kwamba Liverpool wangepindua meza kirahisi dhidi ya Atletico wanaofundishwa na Diego Simeone, kutokana na ukweli kwamba Wahispania hao hawana nguvu sana msimu huu.

Wakati Liverpool wamejihakikishia ubingwa wa England, isipokuwa itokee miujiza, kwani wamewaacha mbali mno washindani wao wa karibu – Manchester City, Atletico hawapo vizuri huko kwao, wakiachwa nafasi ya sita kwenye msimamo wa Ligi Kuu ya Hispania – La Liga na hawana ndoto ya ubingwa.

Kumbe Atletico tangu mechi ya kwanza waliingia wakichukuliwa ni wanyonge, lakini walipotoka na ushindi wa bao moja kule kwao, waliendelea kujipanga kwa ajili ya kuja kumalizia kazi nchini hapa England, na wakafanya kweli.

Ghafla msimu wao umekumbwa na hali ya ajabu – wakiruhusu mabao hivyo na kushindwa kufanya yaliyokuwa kawaida yao kwenye ushambuliaji. Hawa si wale wachezaji tuliokuwa tumewazoea katika Sadio Mane, Mohammed Salah, Virgil van Dijk na mabeki wengine wa pembeni ambao walikuwa wakitoa asisti kibao na pia kufunga mabao.

Sasa wamevuliwa ubingwa waliouchukua msimu jana jijini Madrid kwa kuwafunga Tottenham Hotspur ambao, ajabu nyingine, nao walikuwa watamu kwenye ligi ya nyumbani England na pia UCL lakini tangu siku hiyo ya fainali, wakaanza kuporomoka kama jiwe lililoachiwa juu ya kilima, au baiskeli inavyoshuka mlima – hakuna kunyonga hadi kumfukuza kazi kocha wao Mauricio Pochettino.

Liverpool walitarajiwa kwa kasi waliyokuwa nayo wangetetea taji hilo kama walivyofanya Real Madrid kwa misimu kadhaa wakati wa ngwe ya kwanza ya kocha Zinedine Zidane, lakini haikuwa, wakaishia kuangukia pua nyumbani, na ule wekundu wa Kopps haukuwa lolote mbele ya Atletico.

Reds, kama wanavyojulikana Liverpool, walitoka pia kupata kichapo cha haja, kwani timu iliyokuwa kwenye eneo la kukaribia kushuka daraja – Watford – waliwakandika mabao 3-0 na kumaliza ndoto ya kuiga rekodi ya Arsenal ya kutopoteza hata mechi moja kwenye EPL waliyoweka msimu wa 2003/4 chini ya kocha Arsene Wenger. Haijavunjwa hadi sasa.

Wakiwa wanapepesuka kwa kichapo kutoka kwa Watford, Liver nusura wapoteze tena kwa West Ham, wakitangulia kufunga lakini wakajitahidi wakakomboa bao na kuongeza la ushindi. Katika kipindi cha wiki moja tu, Liver walitupwa nje ya Kombe la FA na Chelsea kabla ya shangazo hili la usiku wa Jumatano.

Iliwauma sana Liverpool kwa ujumla wao, Klopp akisema kwamba walikosea wenyewe kuruhusu bao la kwanza, lawama zikienda kwa kipa anayeshikilia namba moja sasa, Adrian, kutokana na yule wa kwanza, Alisson kuwa ameumia na yu nje ya uwanja.

Na Liverpool walilipa gharama kwa kupigwa bao hilo, ambapo vijana wa Simeone walikuwa wakali, jeuri na wakiwatikisa Liverpool vilivyo na mwishowe wakameza chungu hiyo ya pili ndani ya siku chache, wachezaji wakionekana wamelegea kabisa kipenga cha mwisho kikiisha kupulizwa.

Ni kweli watavikwa ubingwa wa England, lakini ndio hivyo sherehe ya Liverpool ni kama chakula kilichotiwa mchanga; hakinogi tena kivile na si ajabu huu ukawa mwanzo wa kushuka kwa makali Liverpool na tusishangae kuona wakianza vibaya au kufanya vibaya msimu ujao. Ile nguvu, mwelekeo na kasi vinapotea.

Marcos Llorente aliwaadhibu Liver ambao awali walikuwa wakicheza vyema hadi kosa la Adrian lilipofanywa, Llorente akiwa ameingia kipindi cha pili, akatia kimiani mabao mawili jumla huku Alvaro Morata akitia la tatu.

Atletico, kocha wao na washabiki waliosafiri, walishangilia sana hapo Anfield, wakiwaacha wenyeji wakiwa hawaamini kilichotokea hadi wakati wa muda wa ziada unakamilika. Liver watajiuguza kwa muda mrefu kwa jeraha la usiku huo mbaya kwao. Kama kuna aliyewanyima kabisa nafasi ni kipa wa Atletico, Jan Oblak aliyekuwa kama ukuta uliowekwa kuzuia chochote kupita.

Report

Written by Israel Saria

For the last 20 years I have been working as a football pundit. This experience has provided me with a very useful insight into football and the opportunity to carry out extensive research into the game including its players, the stadiums, the rules and tactics and I have also been grateful to meet a wide range of people connected to football in the UK, Tanzania, Germany .....

What do you think?

71 Points
Upvote Downvote
Tanzania Sports

Corona na hatari ligi kubwa Ulaya

Magoli ya Meddie

Tuanze kumlaumu Mwigulu kwenye kifo cha Singida United ?