Lakini kwenye mchezo wa soka kuna takwimu za aina mbalimbali. Hapa kwetu TFF inategemewa kuwa chanzo muhimu cha taarifa za soka nchini
“Rekodi zimewekwa ili zivunjwe”. Huo ni msemo maarufu wa wahenga duniani. Ni msemo ambao unatumika zaidi kwenye michezo na burudani. Miongoni mwa rekodi zilizovunjwa ni ile ya gwiji wa soka Edson Arantes do Nascimento maarufu kama Pele ya kufunga mabao 767 katika maisha yake ya soka.
Takwimu za Pele zinaonesha mabao aliyofunga kuanzia katika maisha yake ya kandanda duniani. Kuanzia Ligi Kuu Brazil akiwa na klabu yake ya Santos, timu ya taifa ya Brazil na kadhalika. Pele amepachika mabao kwenye Fainali za Kombe la Dunia ambazo alianza kucheza akiwa na umri wa miaka 17 tu. Ni umri ambao unadhihirisha mapishi ya Kibrazil kwenye kandanda.
Takwimu za sasa zinaonesha Cristiano Ronaldo ndiye mchezaji pekee aliyevunja rekodi ya Pele. Ronaldo amefunga mabao 770, ikiwa ni matatu zaidi ya Pele. Takwimu hizi zinatumika kwenye mijadala mbalimbali ili kuonesha umahiri wa wanakandanda duniani.
Habari ya pili baada ya ile ya kwanza ya Pele na Ronaldo inamhusu winga mahiri Theo Walcott. Taarifa ya Walcott iliwahusu waendeshaji wa Ligi Kuu England kumzawadia tuzo nyota huyo wa zamani wa Arsenal ambaye sasa anakipiga katika klabu ya Southampton, Theo Walcott.
Top 10 Most Impressive Records In Football History
Theo alizawadiwa kutokana na kutimiza mechi 300 za Ligi Kuu England. Tunafahamu kuwa katika Ligi Kuu England kuna tuzo za aina mbalimbali kuanzia kocha bora wa mwezi, kocha bora wa msimu, mchezaji bora wa mwezi na msimu au tuzo za wachezaji bora wa mechi.
Si EPL pekee, bali La Liga, Lique 1, Serie A, Bundesliga,PSL na nyinginezo duniani kumekuwa kukitolewa tuzo mbalimbali kwa wana michezo.
Tanzania ni nchi ambayo ina wanasoka mbalimbali ambao wanatumika kwenye vilabu vya Ligi Kuu na Timu za Taifa. Ligi Kuu tanzania bara inahusisha wageni kutoka Ivory Coast,Zamba, DR Congo,Angola,Ghana,Togo,Burkina Fasso, Kenya, Uganda,
Burundi, Rwanda, Zimbabwe na nchi nyinginezo.
Kwahiyo ni Ligi ambayo inabeba nyora wan chi nyingi ambapo taarifa zao na michango yao katika kandanda inatakiwa kuoneshwa kokote ulimwenguni.
Ligi Kuu Tanzania Bara pia kumekuwa na zawadi wanazopewa wachezaji bora wa mechi, mwezi na msimu kama ilivyo kwa makocha bora wa mwezi na msimu. TFF kama vilivyo vyama vingine vya soka wanajaribu kuboresha na kuhamasisha mchezo wa soka. hilo wanatakiwa kuungwa mkono.
Lakini kwenye mchezo wa soka kuna takwimu za aina mbalimbali. Hapa kwetu TFF inategemewa kuwa chanzo muhimu cha taarifa za soka nchini. Kuanzia historia ya wachezaji mbalimbali, takwimu na taarifa nyinginezo.
TFF ndio wanaolea na kusimamia mchezo wa soka kwa kushirikiana na Bodi ya Ligi Kuu wanaweza kuwa vyanzo muhimu vya maendeleo ya kandanda nchini.
Iko hivi, kwenye mchezo huu inabidi TFF na Bodi ya Ligi watuambie takwimu mbalimbali. Kwa mfano TFF na Bodi ya Ligi Kuu walitakiwa watuambie ni mchezaji gani amecheza mechi nyingi za Ligi Kuu Tanzania bara tangu ilipoanzishwa.
TFF waweke hadharani (tovuti na mitandao ya kijamii) na kutuambia kinaubaga kuwa ni mchezaji gani ambaye amefunga mabao mengi ya Ligi Kuu Tanzaniua Bara tangu ilipoanzishwa.
Hapo sina maana ya mchezaji aliyefunga mabao mengi kwa msimu mmoja. Nina maana na mchezaji aliyefunga mabao mengi katika historia ya Ligi Kuu hadi sasa.
Bodi ya Ligi na TFF walitakiwa watuambie ni mchezaji gani amecheza mechi nyingi za Ligi Kuu Tanzania. Matahalani wanaweza kuiga mfano wa kutunza takwimu za wachezaji gani wamecheza mechi 100 za Ligi Kuu Tanzania Bara.
Tunaweza kumchukua mastaa wetu wa zamani kama Nadir Haroub na kutazama alicheza mechi ngapi za Ligi Kuu Bara. Mrisho Ngassa alifunga mabao mangapi ya Taifa Stars au nani alifunga mabao mengi katika kikosi cha timu ya taifa?
Kuna wachezaji wan je, bila shaka TFF ilitakiwa kutunza takwimu zao, nani kati yao alifunga mabao mengi kati ya wanakandada hao. Takwimu kama hizo zinawezesha TFF kuitangaza Ligi yetu nje ya mipaka hususani wale wanaofuatilia na kutaka kujua mambo mengi ya mpira wetu.
Zama zimebadilika, si kutunza nyaraka kwenye karatasi kabatini bali pia kutumia nyenzo za kisasa kuweka takwimu na taarifa ambazo zinawezesha wadau wa soka wa ndani na nje kuzifuatilia na kuzitumia kwa maslahi ya soka la Tanzania.
Haya mambo ni muhimu na yanahitaji kutumia nguvu kidogo kwa watu waliopo si lazima kutengeneza ajira mpya kwa watu. Ninaamini TFF na Bodi ya Ligi inao watu wenye weledi ambao wanatambua umuhimu wa kutangaza takwimu za wachezaji wetu iwe kwa mwezi au msimu.
Inawezekana kabisa kuwatangaza na kuwazawadia wachezaji waliotengeneza mabao, hata kwa kutambua mchango wao. Inawezekana kabisa kuchagua bao bora la wiki ambalo litakuwa chachu kwa wachezaji na kutangaza ligi yetu. Hizi ni takwimu rahisi ambazo hata Shirikisho la soka Ulaya, UEFA wanatumia kunadi vipaji vya nchi wanachama wao. Inawezekana tukiamua.
Comments
Loading…