in , ,

Ligi ya Mabingwa Ulaya:

FAINALI ZA AINA YAKE

Ligi ya Mabingwa Ulaya (UCL) msimu huu imekuwa ya aina yake, ambapo
wababe wanne waliobaki huko ni Barcelona, Liverpool, Tottenham Hotspur
na Ajax.

Wawili wa mwisho hawakupewa nafasi na wengi, lakini walishangaza
dunia, pale Spurs walipofanikiwa kuwatoa Manchester City na vijana
wadogo wa Ajax wakapindua kabati kwa kuwapiga nje Juventus katika
mechi za robo fainali.

Juventus walijiamini kwamba wangeweza kuwatuliza vijana hao wa
akademia, ikizingatiwa kwamba mechi ya mkondo wa pili ilikuwa
ikifanyika Torino. Man City waliofungwa 1-0 kwenye mechi ya kwanza
ugenini, walijiamini kwa kiasi kikubwa kwamba wangepindua meza.

Manchester United nao walikuwa kwenye mbio hizo, chini ya Ole Gunnar
Solskjaer, lakini walikuwa butu na hovyo kwenye mechi zote mbili,
wakipigwa 1-0 ya kwanza nyumbani Old Trafford na wakalambwa 3-0 mechi
ya pili nyumbani kwa Barcelona, kule Camp Nou.

Kama kuna mechi iliyovuta wengi ni ile ya Man City dhidi ya Spurs,
ambapo makocha Pep Guardiola na Mauricio Pochettino mtawalia walikuwa
katika hali ngumu muda wote wa mchezo, kama ilivyokuwa kwa washabiki
na wachezaji wao waliocheza kwa ari kubwa kutafuta ushindi.

Dakika 21 za mwanzo zilishuhudia mabao matano, kwenye mechi
iliyomalizika kwa Man City kushinda 4-3, jumla ikawa 4-4, lakini Spurs
wakavuka kiaina, kutokana na wingi wa mabao ya ugenini ambayo ni
matatu dhidi ya sifuri ya Man City.

Ilikuwa hekaheka tangu mwanzo hadi mwisho wa mchezo, makocha wakihemka
na wakati mwingine kupiga magoti, hasa Guardiola ambaye kama wachezaji
wake, hawakuamini kipenga cha mwisho kilipomalizika.

Kubwa ambalo hadi sasa wanajiuliza ni jinsi dakika za mwisho
walivyokataliwa bao la Raheem Sterling kutokana na Sergio Aguero kuwa
ameotea, lakini lile la tatu la Spurs lililotiwa kimiani na Fernando
Llorente ambapo ilionekana kama mchezaji alinawa mpira kabla ya
kuingizwa kimiani.

Ndio hivyo, matokeo yakawa, wachezaji wa City wakawa kwenye hisia
kubwa na masononeko huku Pochettino na timu yake wakiwakimbilia
washabiki wao waliosafiri hadi Manchester, wakaenda kwenye kona ya
mbali kushabikia, na inasemwa hadi Ijumaa Kuu Spurs walikuwa bado
wakishangilia.

Mechi ya Man United na Barcelona ilikuwa zaidi ya upande mmoja, na
dhihirisho kwamba Mashetani Wekundu wanatakiwa kubadilika, kocha
atafute wachezaji wengine kadhaa, afungue mlango kwa ‘mizigo’ na kuuza
wengine.

Kwa matokeo hayo sasa zinasubiriwa nusu fainali za aina yake, ambapo
Barcelona watachuana na Liverpool huku Spurs wakikabiliana na Ajax
wanaotoka nchini Uholanzi. Je, atakuwa Lionel Messi au Mo Salah
atakayetamba?

Spurs na Ajax wanapepetana Aprili 30 wakati Barcelona na Liverpool ni
Mei Mosi kwa mechi za mkondo wa kwanza, kisha marudiano ya jozi ya
kwanza ni Mei 7 na jozi ya pili Mei 8. Fainali ya mwaka huu inachezwa
Juni mosi.

Report

Written by Israel Saria

For the last 20 years I have been working as a football pundit. This experience has provided me with a very useful insight into football and the opportunity to carry out extensive research into the game including its players, the stadiums, the rules and tactics and I have also been grateful to meet a wide range of people connected to football in the UK, Tanzania, Germany .....

What do you think?

71 Points
Upvote Downvote
Tanzania Sports

Hii ni BARCA ndani ya miaka 10 iliyopita

Tanzania Sports

Kosa lilianzia kichwani mwa Ferguson