in , , , , ,

LIGI YA MABINGWA ULAYA

 

Real Madrid, Juventus wavuka

 

Hatimaye Real Madrid wa Hispania na Juventus wa Italia wametinga nusu fainali ya Ligi ya Mabingwa Ulaya (UCL) kwa ushindi mwembamba dhidi ya wapinzani wao.

 

Wakati Real waliwapiga mahasimu wao wa Madrid, Atletico Madrid kwa 1-0, Juve nao wamevuka kwa idadi hiyo hiyo ya bao dhidi ya Monaco wa Ufaransa.

 

Tofauti yao ni kwamba kwenye mechi za mkondo wa kwanza Madrid walikwenda suluhu na Atletico wakati Juve waliwapiga Monaco 1-0.

 

Real waliingia dimbani jana wakiwa wanakabiliwa na majeruhi, ambapo waliwakosa Gareth Bale, Karim Benzema na Luka Modric lakini wakafanikiwa kupata ushindi.

 

Alikuwa mchezaji wa Manchester United aliye kwa mkopo Madrid, Javier Hernandez ‘Chicharito’ aliyewainua washabiki wa Los Blancos kwa kutia kimiani mpira dakika ya 88 kutokana na pasi ya Ronaldo.

 

Hii ni mara ya kwanza kwa Real kuwafunga Atletico katika mechi nane zilizopita, ambapo mara ya mwisho waliwafunga kwenye michuano kama hii hatua ya fainali msimu uliopita.

 

Real wanatafuta kutetea ubingwa, jambo ambalo halijapata kufanywa na timu yoyote. Real na Juve wanaungana na Barcelona na Bayern Munich kucheza nusu fainali.

 

Chicharito amekuwa mchezaji wa tano katika historia kuzifungia mabao Manchester United na Real Madrid kwenye UCL. Wengine ni Michael Owen, David Beckham, Ruud van Nistelrooy na mchezaji mwenzake, Ronaldo.

 

Wageni waliwavuruga Real kwa muda mwingi wa mechi hiyo, lakini mchezo ulifunguka baada ya Arda Turan wa Atletico kutolewa nje katika dakika ya 75 kwa mchezo mbaya dhidi ya Ronaldo na Sergio Ramos.

 

Turan alipangwa mahsusi kumkabili Ronaldo, na alifanya kazi hiyo kikamilifu muda wote akiwa dimbani.

 

Kulikuwa na kila dalili kwamba mechi ingeingia muda wa nyongeza wa dakika 30, lakini Ronaldo alichomoka kisha akamtengea Chicharito pasi nzuri naye akakwamisha mpira wavuni.

 

Ronaldo kwa msimu huu amefunga mabao 50 na kutoa pasi 19 zilizozaa mabao. Kocha wa Atletico, Diego Simeone alieleza kuridhishwa na kiwango cha timu yake na walikofika na kwamba wanarudi nyumbani wakiwa na faraja.

 

Kocha wa Real, Carlo Ancelotti alimmwagia sifa Chicharito, akisema alijitoa kabisa kuhakikisha wanapata ushindi, hujituma kwenye mazoezi na kumsikitikia kwa jinsi alivyokosa nafasi za kucheza awali msimu huu.

 

Ama katika mechi baina ya Juventus na Monaco, wenyeji Monaco walitawala mchezo zaidi lakini Juventus walikuwa makini katika ulinzi na kipa wao mahiri, Gianluigi Buffon.

 

Monaco walishangaza kufika nusu fainali, ikizingatiwa kwamba walimuuza mfungaji wao mahiri, James Rodriguez kwa Real Madrid na pia wakamtoa kwa mkopo Radamel Falcao kwa Man United.

1MONACO

 

Juve wanasaka makombe matatu msimu huu – wakiwa wamefika fainali ya Kombe la Italia, wanaongoza ligi kuu kwa tofauti ya pointi 15 na sasa wanasaka ubingwa wa Ulaya. Mara ya mwisho kufika nusu fainali ilikuwa 2003.

 

Monaco walijaribu kuwafungua Juve kwa kumwingiza mshambuliaji wa zamani wa United, Dimitar Berbatov, ambaye nusura awapatie bao kama si umahiri wa Buffon.

 

Timu za Italia hazijafika nusu fainali tangu 2010 pale Inter Milan walipotwaa ubingwa. Klabu za huko ziliitawala Ulaya kisoka mwanzoni mwa milenia. Zilishinda ubingwa wa Ulaya mara tatu kati ya 2001 na 2010 lakini siku hizi zinakwenda kwa shida.

 

Juve walicheza bila kiungo mahiri duniani, Paul Pogba aliyekuwa majeruhi lakini wanaamini atakuwapo kwenye mechi ya nusu fainali wanayosubiri kwa hamu kujua watacheza dhidi ya nani.

 

Barcelona walifika nusu fainali kwa kuwatoa Paris Saint-Germain (PSG) wa Ufaransa kwa jumla ya mabao 5-1 wakati Bayern Munich waliwatoa FC Porto kwa jumla ya mabao 7-4.

Report

Written by Israel Saria

For the last 20 years I have been working as a football pundit. This experience has provided me with a very useful insight into football and the opportunity to carry out extensive research into the game including its players, the stadiums, the rules and tactics and I have also been grateful to meet a wide range of people connected to football in the UK, Tanzania, Germany .....

What do you think?

71 Points
Upvote Downvote

Comments

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Loading…

0

Diaby kupiga ‘deiwaka’ Arsenal?

Klabu zinavyokomalia tiketi