TANZANIASPORTS imetathmini masuala machache yanayojenga mvuto wa Ligi Kuu Tanzania na kuwa kinara katika ukanda wa Afrika mashariki na Afrika kwa ujumla wake…
LIGI KUU Tanzania Bara imemalizika kwa Yanga kutetea taji lake. Katika Ligi ya msimu huu shamrashamra zilikuwa nyingi na matukio kadhaa ambayo yanachora taswira ya soka la Tanzania barani Afrika. kwa mkusanyiko wa wachezaji waliopo Ligi Kuu Tanzania Bara ni kama Umoja wa Mataifa. Ni Ligi ambayo imekusanya wachezaji kutoka mabara ya Afrika, Amerika ya Kusini,Asia na Ulaya. Mkusanyiko huo unatukumbusha namna kikosi cha kocha wa zamani wa Arsenal, Arene Wenger ambaye alikuwa na wachezaji kutoka karibu kila bara. Arsenal iliwahi kuitwa jina la utani “Timu ya Umoja wa Mataifa.” Hivi ndivyo hali ilivyosisimua katika Ligi Kuu.
TANZANIASPORTS imetathmini masuala machache yanayojenga mvuto wa Ligi Kuu Tanzania na kuwa kinara katika ukanda wa Afrika mashariki na Afrika kwa ujumla wake.
Ligi ya Umoja wa Mataifa
Timu ya Geita Goldmine ilisajili mshambuliaji toka Japan. Simba walimsajili Dejan kutoka bara la Ulaya kabla ya kuachana naye. Simba hao hao pia wana makocha raia wa Brazil. Singida Big Stars wanamiliki wachezaji kutoka bara la Amerika ya Kusini katika nchi ya Brazil. Watani wao wa jadi Yanga wana mkusanyiko wachezaji wa kigeni kutoka mataifa mbalimbali barani Afrika.
Ligi ya Mataifa ya Afrika
Asilimia kubwa ya timu za Ligi zilifanya usajili wa wachezaji wa kigeni. Ukiangalia vikosi vyao utaona wachezaji kutoka mataifa mengine ya Afrika ambayo yanaipa thamani Ligi yenyewe. Mashabiki wa soka kutoka nchi kama vile Mali, Zambia, DRC, Senegal, Kenya, Uganda, Nigeria,Malawi,Ghana,Ivory Coast na nyinginezo watakuwa na haku ya kuwafuatilia wachezaji wao wanaokipiga Ligi Kuu Bara.
Mali watamwangalia Djigui Diarra, wakati Zambia watawaangalia Kennedy Musonda na Cletous Chama. Halafu kuna wale kutoka mataifa mengine Ghana, Burundi,Nigeria na kadhalika nao watawafuatilia wachezaji wao wanaokipiga Ligi Kuu Bara. Makocha wa Taimu za Taifa watatupia macho wachezaji wao wanaocheza Ligi Kuu Bara. Hivyo kunaifanya Ligi hii kuwa pendwa na ndiyo inakuwa kama vile Ligi ya Afrika kwani imeleta vipaji vyote pamoja.
Wazawa waburuza mkia
Katika msimamo wa wafungaji bora wa Ligi Kuu msimu huu wachezaji wa ndani wameshindwa kufurukuta kwa mara nyingine na kuwaacha wageni watamba. Wachezaji wa kigeni wamefumania nyavu mara 127. Idadi hiyo inapatikana katika orodha ya vinara wa mabao msimu huu ambapo washambuliaji wazawa waliotoboa ni John Bocco (mwenye mabao 10), Sixtus Sabilo (mwenye mabao 9) na Reliants Lusajo(mwenye mabao 8.
Washambuliaji wa kigeni vinara wa kupachika mabao ni Fiston Mayele raia wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo amepachika mabao 17, Saido Ntibazonkiza (17, raia wa Burundi), Prince Dube(12, raia wa Zimbabwe), Moses Phiri (10, raia wa Zambia), Bruno Gomes (10, raia wa Brazil), Stephane Aziz Ki (9, raia wa Ivory Coast), Pape Sakho (9, raia wa Senegal), Meddie Kagere (8 raia wa Rwanda), Jean Baleke (8, raia wa DRC), Idriss Mbombo (8 raia wa DRC), Collin Opare (9). Hawa ni wachezaji wa kigeni wenye mabao juu ya 8.
Nafasi nne CAF
Hii ni fursa ambayo itazidi kuwavutia wachezaji na wataalamu mbalimbali kuja Tanzania. Wachezaji wataamini kuwa nafasi nne za uwakilishi katika mashindano ya CAF zina maana kubwa kwao katika kuendeleza vipaji vyoa na njia ya mafanikio.
Nafasi hizo zimeonesha namna zinavyotumika vizuri kwani Simba na Yanga zimekuwa na msimu mzuri na rekodi za nyuma zinavutia maelfu ya wachezaji wa kigeni kuja kucheza Ligi ya Tanzania. Msimu ujao katika mashindano ya CAF Tanzania itawakilishwa na Yanga,Simba,Azam na Singida Big Stars. Hii ni nafasi kwa wachezaji wengi kutafuta mafanikio na kuvutia zaidi wageni wengine.
Simba,Yanga wamegawana
Msimu umemalizika kwa klabu kongwe za Simba na Yanga kugawana wachezaji bora. Kikosi kilichotangazwa na Shirikisho la Soka nchini Tanzania kilionesha asilimia 99 ya wacheaji hao wametoka klabu za Simba na Yanga na kudhihirisha ushindani na ubora wao. Katika kikosi hicho Yanga wametoa wachezaji Djigui Diarra, Dickson Job, Bakari Mwamnyeto na Fiston Mayele. Simba nao wametoa wachezaji kama vile Hennock Inonga, Mzamiru Yassin,Shomari Kapombe,Saido Ntibazonkiza, Cletous Chama na Mohammed Hussein. Mchezaji pekee aliyeingia akitokea timu nyingine ni Bruno Gomes toka Singida Big Stars.
Comments
Loading…