Lampard na upotoshaji wa usajili
Manchester City wamechafua hali ya hewa, kutokana na dalili za kutoa taarifa potofu juu ya kiungo wa zamani wa Chelsea, Frank Lampard aliyedaiwa kusajiliwa na New York City FC kwa mkataba wa miaka miwili.
Zimekuwa zikitolewa taarifa tofauti tangu ‘usajili’ huo ulipofanyika, ambapo awali baada ya Chelsea kuelekea kumuacha mchezaji huyo, ilidaiwa angekwenda Marekani, na kweli akasafiri, akapiga picha akiwa na jezi na skafu ya klabu hiyo yenye uhusiano na Man City.
Hata hivyo, kwa mshangao wa wengi, alirudi England bila kucheza mechi yoyote huko Marekani, kwa maelezo kwa vile ligi ya huko inachelewa kuanza, ametolewa kwa mkopo wa miezi sita kwa Man City.
Yeye mwenyewe Lampard alisema majuzi kwamba lengo la kutolewa kwa mkopo ni kumpa fursa ya kupata utimamu wa mwili kabla ya kwenda Marekani mapema mwaka huu, jambo ambalo hakufanya.
Taarifa zilizofuata ni kwamba wameamua kuongeza muda wa mkopo wa mchezaji huyo Man City hadi mwisho wa msimu huu wa soka, taarifa ambazo klabu na Lampard pia walitolea ufafanuzi kwamba atabaki Manchester.
Hata hivyo, dodoso za watafiti na hatimaye taarifa rasmi ya City iliyotolewa Ijumaa hii inaonesha kwamba Lampard hakupata kutia saini yoyote kuchezea klabu hiyo ya Marekani, ikimaanisha kwamba alisajiliwa Manchester kama mchezaji huru tangu mwanzo.
Tayari Bodi ya Ligi Kuu inafuatilia suala hilo, kwa sababu kanuni zinakataza timu kumsajili mchezaji (wa kudumu) kwa pungufu ya miezi 12. Man City wanasema walichokuwa wamefanya wenzao wa New York ni makubaliano ya awali na si usajili wa Lampard kama ilivyotangazwa, na kwamba hilo lilikuwa kosa.
Bodi ya Ligi Kuu imecharuka kuhusu msisitizo mpya wa City kwamba Lampard alisaini mkataba wa miezi sita hadi mkesha wa mwaka mpya, ikiitaka Man City iseme kwamba alisaini mkataba wa miezi 12 ulioanza Agosti mwaka jana, ukiwa na kifungu cha kutoa likizo Desemba 31 ambacho kiliondolewa kwenye mkataba huo, hivyo kumfanya abaki City moja kwa moja na hivyo kuwa mkataba halali.
Licha ya maelezo, au majaribio ya Bodi kujinasua kwenye suala hilo, Man City wametoa taarifa kwamba hapakuwahi kuwapo kifungu cha mkataba kuwekwa likizo Desemba 31, bali kwamba alikuwa na makubaliano ya awali na jamaa wa New York lakini wao wakamsajili kwa muda huo.
Kadhalika wanasema kwamba ilikuwa kosa kueleza kwamba Lampard ameongezewa muda wake wa mkopo Man City hadi mwisho wa msimu, wakisema kwa vile hakupata kusajiliwa Marekani na hakuwa na klabu nyingine yoyote, asingeweza kutolewa kwa mkopo.
Lampard (36) alikuwa na tamaa ya kuendelea kucheza Chelsea, lakini Koch Jose Mourinho alionesha kutomhitaji, hivyo akaondoka akiwa mchezaji huru na sasa ni mmoja wa wachezaji tegemeo wa City.
Kocha wa City , Manuel Pellegrini alipoulizwa Ijumaa hii juu ya suala hilo na maudhi yanayobebana nalo kama trekta na trela yake, alikataa kuingizwa kwenye sakata lenyewe, akisema badala yake:
“Nadhani suala hili limeshamalizwa. Frank sasa yupo hapa. Najua kuna maoni tofauti juu yake nami naheshimu yote, lakini uamuzi tayari umechukuliwa na Frank atabaki hapa hadi mwisho wa msimu.
“Narudia, sitaki kuendelea kuzungumza juu ya kitu hiki kwa sababu kimeshamalizwa. Matatizo yote tofauti huwa yana tatizo jingine ndani ya tatizo. Nafikiri kwa sasa hili limemalizika.”
Comments
Loading…