in , , , ,

Ched Evans: Sakata la mwanasoka mbakaji

England imegubikwa na mazungumzo juu ya mwanasoka Ched Evans (jina kamili ni Chedwyn Michael ‘Ched’ Evans aliyeanzia akademia ya Manchester City 2002 na sasa anahangaika bila klabu baada ya kutumikia kifungo gerezani akiisha kutiwa hatiani kwa kubaka.

Evans aliyeondoka Man City katika timu ya wakubwa 2007 akiingia Norwich kwa mkopo kisha akauzwa Sheffield United 2009, aliharibikiwa au aliharibu mambo yake 2012 baada ya kutiwa hatiani kwa kubaka na kuhukumiwa adhabu ya miaka mitano gerezani.

Tangu wakati huo hajacheza tena soka ya kulipwa, licha ya kwamba aliachiwa kutoka gerezani Oktoba mwaka jana. Hivi sasa anatengwa, anabaguliwa na hakuna timu inayomtaka. Majuzi hapa, klabu ya Oldham ilitaka kumsajili, lakini mara moja ikaachana na mpango huo baada ya wafanyakazi wa klabu hiyo na familia zao kutishiwa maisha, pengine na ndugu wa dada aliyebakwa na mwanamichezo huyu.

Watu wamegawanyika, baadhi wakisema kwamba anatakiwa apewe nafasi lakini wengine wanasema si rahisi arudi kwenye soka haraka kiasi hicho, kama atarudi kabisa. Jinsi soka au michezo kwa ujumla wake ilivyo na umuhimu kwa uchumi wa taifa hili, hata waziri mkuu ameingia.

Ndiyo, Waziri Mkuu David Cameron yeye anasema haoni ni kwa vipi ilitarajiwa au ingewezekana kivitendo kwa Evans kurudi kwenye soka moja kwa moja baada ya kuachiwa kutoka gerezani.

Ieleweke kwamba huyu hakusamehewa au si kwamba hukumu yake imetenguliwa, bali muda wake wa kuhudumu gerezani, kwa sheria za hapa umeisha na amerudi uraiani kama Panya Road wa hapo Manzese, Tandika, Buguruni na Mbagala watakavyorudi uraiani iwapo watatiwa hatiani na kufungwa, tuseme miaka mitano au miwili au 10.

Mtendaji Mkuu wa Chama cha Wachezaji wa Kulipwa, Gordon Taylor alianza kwa kufananisha suala hili na lile la utata wa kilichotokea kwa washabiki 15 wa Liverpool kuuliwa uwanjani katika Matukio ya Hillsborough, lakini baadaye ameomba radhi, labda kwa kukumbushia machungu au kuona yanaweza kumweka pabaya.

Kama kuna kitu kinaendelea kuwaumiza watu wa Liverpool ni watu hao kupoteza maisha, na kila unapofika wakati wa kuwakumbuka, kuweka maua, kusali, kupiga picha, hisia huwa juu sana na machozi huwatoka wengi.

Chama cha Soka (FA) kinafikiria kubadili kanuni zake za maadili kutokana na yatokanayo na kesi ya Evans na hali ilivyo baada ya kuwa ametoka gerezani. Je, kitaweka bayana kwamba mchezaji aendelee kule alikokuwa? Je, kitamfungia moja kwa moja? Ni jambo la kusubiri.

Lakini Kocha wa Hull, Steve Bruce analiona suala hili katika mwanga tofauti, akisema hata kama alikuwa ametiwa hatiani na hajafutiwa makosa yake, ni vyema apewe nafasi ya kucheza tena soka. Evans ana umri wa miaka 26 tu, na kipaji na kitu kilichokuwa kinamwingizia kipato ni soka.

Baada ya kutoka gerezani, Oldham wakasema wanamtaka, lakini wakati mambo yanahitimishwa ndipo soo ikatokea, na sasa ameachwa solemba. Alikataa haki yake ya kimsingi ya kukata rufaa dhidi ya uamuzi uliomtia hatiani, hivyo mantiki yaweza kuonesha kwamba alitenda kweli ubakaji.

Hata hivyo, tunavyozungumza, Tume ya Mapitio ya Mashauri ya Jinai inatafiti upya kesi hiyo. Bruce anasema anajua anaweza kukwza watu, lakini ushahidi uliotolewa uliacha mianya mingi ya kukatia rufaa.

Swali linabaki pale pale; kwa nini Evans hakukata rufaa akakubali kwenda lupango kwa miaka hiyo? Ni suala kubwa hapa, kwa sababu badala ya kurejewa kama Evans, sasa wanaandika na kumsema kama ‘convicted rapist’, yaani mbakaji aliyetiwa hatiani.

Kunakuwa na ukakasi kidogo kumwalika kwako mtu wa aina hiyo, japokuwa hakuna aliye mkamilifu. Oldham walikuwa wamesema kwa asilimia 80 wangemchukua, lakini sasa wamesema basi.

Klabu yake ya zamani, Sheffield United walikuwa wametoa ofa ya kutumia miundombinu ya klabu kwa mazoezi, lakini sasa wameifuta na hatakiwi hata kuonekana hapo. Labda Bruce na Hull wamchukue, hata kama hatacheza awe kwenye benchi akisubiri wakati wake. Ni rahisi zaidi kusema kuliko kutenda na mkuki kwa nguruwe, lakini kwa binadamu mchungu.

Report

Written by Israel Saria

For the last 20 years I have been working as a football pundit. This experience has provided me with a very useful insight into football and the opportunity to carry out extensive research into the game including its players, the stadiums, the rules and tactics and I have also been grateful to meet a wide range of people connected to football in the UK, Tanzania, Germany .....

What do you think?

71 Points
Upvote Downvote

Comments

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Loading…

0

Toure mwanasoka bora Afrika

Lampard na utata wa usajili wake