Huwa namtazama vizuri sana kwa siku za hivi karibuni mzee wangu Sir Alex Ferguson. Mzee mwenye heshima kubwa sana katika klabu ya Manchester United.
Alifanikiwa kutengeneza dunia yake ya peke yake pale Manchester United. Dunia ambayo ilivutia watu wengi kuja kuishi kwa furaha kubwa.
Unakumbuka nyakati ambazo aliichukua Manchester United? Zilikuwa nyakati ambazo ilikuwa Manchester United walikuwa wanapitia.
Hilo lilikuwa linaonekana kwa macho ya nyama kabisa bila uficho. Ndizo nyakati ambazo Liverpool walikuwa wamejitengenezea ufalme wao wa peke yao.
Hakuna ambaye alikuwa ana uwezo wa kugusa falme yao. Ilikuwa falme imara sana kuzidi falme zote kwenye ardhi ile ya malikia.
Ilikuwa falme ambayo ilitawala kwa muda mrefu. Na hakukuwepo na mtu wa kukohoa mbele ya Liverpool kwa kipindi hicho.
Miaka 19 timu nyingi zilikuwa kwenye utumwa wa ufalme wa Liverpool. Iliburuza kila kitu ambacho iliona inastahili kuburuza.
Ilisimama mbele na kujitanua na wengine wakipiga goti chini na kushujudia mbele yake. Haya ndiyo yalikuwa maisha halisi ya Liverpool.
Maisha ambayo hata kwenda bafuni walitumia maziwa kuogea. Hawakuwa na wasiwasi kabisa. Ila walikuwa wanaishi maisha ambayo walistahili kuishi kipindi hicho.
Utawaambia nini kuhusu neno njaa wakusikie kwa kipindi hicho ?. Utahubiri nini kuhusu neno ukame wakuelewe vizuri ?
Kwao hakukuwepo na jua la ukame, kila uchwao walikuwa wanapata mvua ya maziwa tu. Mito, bahari na maziwa yote yaliyokuwepo katika kiunga chao yalitapakaa kimiminika hiki.
Hii ndiyo ilikuwa Liverpool, Liverpool yenye miraba minne. Liverpool yenye shibe tele. Liverpool ambayo chozi kwao lilikuwa nadra kushuka.
Wakati unaizungumzia shibe ya Liverpool, basi kulikuwepo na njaa kubwa sana kwa Manchester United.
Hawa hadithi zote zilizohusu furaha walikuwa wanazisikia kwa Liverpool pekee. Mahasimu wakubwa sana.
Ilikuwa inawauma sana. Adui yako kunenepa afu wewe unakonda?, ni maumivu makubwa sana. Maumivu ambayo walikuwa wanayapitia sana Manchester United.
Walisimangwa sana kipindi hicho. Hawakuwa na uwezo wa kujitanua barabarani kwa kujitapa kuhusiana na neno mafanikio mpaka pale Alex Ferguson alipokuja Manchester United.
Mtu ambaye kwa baadaye jina lake liliongezeka kutoka Alex Ferguson na kuwa Sir. Alex Ferguson baada ya kupata mafanikio makubwa mwaka 1999 kwa kuchukua vikombe vitatu.
Mtu ambaye aliikuta Manchester United ikiwa klabu ya tatu kwa kuchukua vikombe vingi vya ligi kuu ya England nyuma ya Liverpool na Arsenal.
Mtu ambaye hakutazamiwa sana kufanya makubwa akiwa na wanajeshi hawa wenye kutumia magwanda ya rangi nyekundu kwenye vita.
Nani alitegemea Ferguson atakuwa mfalme mkubwa wa soka la England?. Mtu ambaye alitoka kwenye timu ambayo haikuwa na jina ?
Mtu ambaye alikua hajawahi hata siku moja kuiongoza timu kubwa kwenye maisha yake ya ukocha? Lakini akapewa jukumu la kupambana na Liverpool ya moto.
Lakini alifanya tofauti na matazamio ya watu wengi. Alirudisha furaha kubwa ndani ya Manchester United.
Huyu ndiye aliyeleta kiangazi kikubwa kwenye ufalme wa Liverpool na kuleta masika kila mwaka katika kikosi cha Manchester United.
Alishinda kila kikombe ambacho kilikuwa kinashindaniwa na kikosi cha Manchester United katika.maisha yake ya ukocha.
Hatimaye akaanza kurudisha furaha iliyokuwa imepotea kwenye kikosi cha Manchester United kwa muda mrefu wa soka.
Akawa mtawala rasmi wa soka la England. Aliogopeka mno. Alikuwa na uwezo wa kushinda kombe lolote akiwa na aina yoyote ya kikosi alichokuwa nacho.
Alikuwa na uwezo wa kuwafanya wachezaji ambao kwenye macho ya kawaida ya watu walikuwa wanaonekana wa kawaida lakini akaifanya timu iwe hatari.
Hakuamini katika ukawaida wa mchezaji mmoja mmoja. Wala hakuamini katika uhatari wa mchezaji mmoja mmoja.
Kwake yeye aliamini katika uhatari wa timu kwa ujumla. Ndiyo maana alikuwa na uwezo mkubwa sana wa kujenga timu imara kupitia wachezaji ambao walikuwa wanaonekana wa kawaida.
Wachezaji ambao hakuwa na ukawaida usio wa kawaida. Wachezaji ambao walikuwa na uwezo wa kupigana sana kwa ajili ya jezi ya Manchester United.
Ndiyo maana hata muda wa yeye kuondoka Manchester United ulipowadia kitu cha kwanza kukiona baada ya kutakiwa kutoa maoni ya mrithi wake ni kupata kocha wa aina yake.
Kocha ambaye alikuwa na uwezo wa kutumia wachezaji wa kawaida kutengeneza timu hatari.
Hapa ndipo kosa kubwa ambalo lilifanyika ambalo mpaka Leo linaigharimu Manchester united kwenye mafanikio yao.
Walimleta David Moyes, walisahau soka la sasa limebadilika. Lilikuwa linahitaji wachezaji hatari na kocha hatari.
Na kocha ambaye alistahili kuwa mrithi wa Sir Alex Ferguson alikuwa anastahili kuwa kocha hatari ili kuendeleza utamaduni wa ushindi wa Manchester United.
Lakini ikawa tofauti, Sir Alex Ferguson akafanya kosa mwishoni kosa ambalo linawahangaisha kwa sasa kukifuta kivuli chake cha mafanikio.