in ,

Baada ya tokomeza zero ya JOKATE ifuate tokomeza fedheha ya KARIA

Hii ni fedheha, ndicho kitu ambacho tunaweza kukuita baada ya matokeo ya Serengeti Boys katika michuano ya vijana waliochini ya umri wa miaka 17 ya Afrika.

Timu ambayo watu wengi walikuwa na matumaini nayo makubwa sana kutokana na matokeo yake mazuri kabla ya fainali hizi za Afcon za vijana walio chini ya umri wa miaka 17.

Hii ndiyo timu ambayo ilikuwa ya tatu kwenye michuano ya vijana walio chini ya umri wa miaka 17 ukanda wa Afrika Mashariki na kati (CECAFA).

Mashindano ambayo tuliandaa sisi na ndiyo mashindano ambayo tulifanya vizuri tofauti na mashindano haya ya Afcon.

Kushika nafasi ya tatu kilikuwa kitu kikubwa sana kwetu na kilianza kutujengea imani kuwa tunaweza tukafika mbali na timu yetu ya Serengeti Boys.

Ndipo hapo taratibu mizizi ya upendo na imani ilipoanza kujengeka kwetu. Timu tukawa na imani nayo kubwa sana. Tukawaamini wanajeshi wetu. Tuliamini wao wanaweza kutulindana na kushinda kwenye vita yoyote ile.

Ndiyo maana hata kwenye vita ya michuano ya vijana waliochini ya umri wa miaka 17 kanda ya nchi za Afrika Kusini (COSAFA), tulibeba ubingwa baada ya kualikwa.

Tulibeba kwa kumpiga huyu huyu Angola katika fainali ambaye Jana amekuja kutupiga goli 4-2 kwenye ardhi yetu wenyewe bila hata huruma.

Hii ni fedheha kubwa sana. Sawa tulizoea kufanya vibaya kwenye michuano mbalimbali , timu zetu kufanya vibaya ilikuwa kawaida tu.

Lakini kwa timu zetu kufungwa katika uwanja wa nyumbani mechi zote tatu, tena kwa wastani wa magoli 4 kila mechi hiki kitu hatujawahi kabisa kukizoea.

Ndiyo maana nikasema hii ni fedheha , fedheha ambayo inatakiwa kutafutiwa dawa sahihi ya kuiondoa na sisi kuwa watu ambao wanafuraha tena.

Hapa ndipo penye umuhimu mkubwa. Dawa ya kuondoa fedheha hii, hiki ndicho kitu ambacho tunatakiwa kukifiria sana. Tumefanya vingi sana ambavyo siyo tiba.

Tumeunda kamati nyingi sana ambazo hazitoi tiba sahihi ya ugonjwa wetu huu. Kamati ambazo mara nyingi zinaundwa kwa ajili ya kuzisaidia timu za taifa.

Timu za taifa ambazo misingi yake ni mibovu sana. Wachezaji wake wametokea katika mazingira ambayo hayamwandai mchezaji kubwa mchezaji bora.

Hapa ndipo kosa ambalo huwa tunalifanya, na kujikuta tunaisahau njia sahihi ya kupitia kwa kujiaminisha njia ambayo ni sahihi.

Njia sahihi ni sisi kupata misingi bora ya mpira wetu. Hiki kitu kimeongelewa na watu wengi sana, kimeongelewa mara nyingi sana lakini hakuna kitu ambacho kinafanyika kuhusiana na hiki kitu.

Siyo mbaya kukumbushana mara kwa mara kwa sababu ni kitu cha msingi katika maendeleo ya mpira wetu. Kwanini tuchoke kukumbushana?, lazima tukunbushane na kupeana mawazo ya namna ambavyo tunaweza kulitekeleza kwa pamoja.

Inawezekana kabisa labda tumekosa pesa za kutekeleza hiki kitu cha msingi na inawezekana hata vilabu vyetu havina uwezo wa kuwa na vituo bora vya kuibua, kulea na kukuza vipaji.

Hiki kitu kinawezekana kabisa, lakini kuna kitu ambacho tunatakiwa kukiangalia kwa sasa. Tuwaangalie watu ambao wanatuzunguka kwa muda huu.

Mama yangu aliwahi kuniambia mtaji mkubwa ni watu. Watu ndiyo mtaji mkubwa sana. Watu ndiyo wanaweza kukupeleka sehemu ya juu ambayo unaitamani kuifikia.

Tuwatumie hao watu wanaotuzunguka kama daraja la sisi kutupeleka katika mji wa mafanikio makubwa katika mpira na kuachana na huu mji wa fedheha.

Mji ambao hata Jokate Mwongelo mkuu wa wilaya ya Kisarawe ameamua kuepushana nao. Hataki fedheha katika mji wake, fedheha za mji wake kupata zero katika mitihani ya kitaifa.

Ndiyo maana akaja na kampeni ya kutokomeza zero, kampeni ambayo aliona hana uwezo wa kuifanikisha peke yake ndiyo maana akaamua kuwatazama watu ambao wanamzunguka.

Hawa watu ndiyo alioamua kwenda nao pamoja kuhakikisha zero katika mji wake zinapungua na kutokomezwa kabisa.

Hiki ni kitu kizuri sana tena ni kitu bora sana. Hebu na sisi tuwaangalie watu ambao wanatuzunguka. Watu ambao wanaonekana kuwa tuko nao karibu.

Tuamue kuwa ndiyo watakuwa watu ambao tutakimbia nao kwa pamoja katika kampeni maalumu ya TOKOMEZA FEDHEHA.

Yani tushirikiane kwa pamoja katika kutokomeza fedheha katika mpira wetu. Tumekuwa na watu ambao ni wakubwa sana.

Tumekuwa na utamaduni wa kuwaita kwenye kamati za kuzisaidia timu zetu mbalimbali za Taifa kushinda.

Tumekuwa tukiwaomba kuwa walezi wa timu zetu mbalimbali za taifa, lakini mwisho wa siku tumekuwa tukipata fedheha tu badala ya furaha.

Nahisi hili jambo litakuwa linawaumiza sana wao. Na kuna Siku watafikia hatua ya wao kuchoka kuendelea kuitwa kwenye hizi kamati.

Hebu tuwatumie vizuri kwa sasa. Tuwatengenezee mazingira bora kwa sasa ambayo yatatusaidia sisi kufikia mafanikio makubwa ya mpira wetu.

Kwa pamoja tuamue kuja na tokomeza fedheha. Tushirikiane wote tupate fedha ambazo zitatusaidia kupata kituo kimoja kikubwa cha Michezo , kituo ambacho kitakuwa kinaibua, kulea na kukuza vipaji vyetu.

Hii ndiyo njia bora kwetu sisi kupata timu imara ya mpira wa miguu. Timu ambayo haitotusababishia fedheha tena katika mpira wa miguu.

Report

Written by Martin

Martin Kiyumbi ni mchambuzi wa habari za michezo na mbunifu wa maudhui.

Martin Kiyumbi amewahi kufanya kazi za uchambuzi kwenye vituo mbalimbali vya habari kama Tanzaniasports (tovuti ya habari za michezo ), Jembe FM , Radio Free Africa na TVE.
Martin Kiyumbi anapatikana kwenye e-mail ya [email protected]

What do you think?

71 Points
Upvote Downvote
Tanzania Sports

Kosa lilianzia kichwani mwa Ferguson

Tanzania Sports

Wachezaji Sita ambao hawatakiwi kucheza Manchester United