HATIMAYE mabingwa soka nchini klabu ya Yanga wamemtangaza Romain Folz kuwa kocha mpya kuanzia msimu ujao. Kocha huyu anakuja Tanzania akitokea kuwa kocha wa klabu ya Akbou huko Algeria. Yanga wanaingia msimu ujao wakiwa na sura mpya ya ukocha ambayo haijulikani katika medani ya kandanda. Zipo sifa kadhaa zinazoeelezwa kuhusiana na kocha huyo, lakini katika ngazi ya kuongoza timu kubwa kama Yanga anajikuta anapita njia ya Sead Ramovic ambaye alijiunga Yanga akitokea Galaxy ya Afrika kusini. TANZANIASPORTS inaangazia zaidi kujua kocha huyo ni nani katika ulimwengu wa soka. Folz mwenye asili ya Morocco anakuja kuongeza ushindani Ligi Kuu.
Njia ya Mamelodi Sundowns

Folz hakutokea kusikojulikana, bali ni kijana ambaye amepita njia rasmi katika kufundisha kandanda barani Afrika. Licha ya kutofundisha timu kubwa kama Yanga lakini ameonekana kuwa chaguo linalowafurahisha mabosi hao. Huenda zipo sifa amabzo mashabiki wa Yanga hwazijui, bali zinajulikana kwa uongozi wa Yanga. Folz alikuwa kocha msaidizi wa Mamelodi Sundowns ya Afrika kusini. Ni kocha kijana ambaye hakuwa na makuu zaidi ya kutekeleza mipango na mikakati ya kuandaa timu kwenye mechi mbalimbali, kusimamia mazoezi, kuongoza mbinu za kutumika katika mchezo unaokuwa kwenye ratiba. Kwahiyo Folz alikuwa kocha mwneye jukumu dogo na ambalo lilihitaji idhini ya mabosi wake. Akiwa kocha msaidizi wa Mamelodi Sundowns amejifunza namna bora ya kuwasimamia mastaa wa timu. Mamelodi ni timu yenye wachezaji wa bei mbaya ambao si rahisi kuwaongoza ikiwa ni kocha kijana. Lakini Folz alikuwa sehemu ya mchango mzuri wa maendeleo ya Mamelodi.
Ligi ya Algeria
Folz alichukua jukumu la kuifundisha klabu ya Akbou inayoshiriki Ligi Kuu Algeria. Alichukua jukumu la kuinoa timu hiyo ikiwa kwenye hatari ya kushuka daraja mapema mwezi Machi. Licha ya changamoto hiyo, Folz alifanikiwa kuituliza timu hiyo na kubaki Ligi Kuu. Kabla ya kuchukua nafasi ya ukocha alikuwa Mkurugenzi wa ufundi tangu kuondoka kwake Mamelodi Sundowns mwezi Desemba mwaka 2024. Alichukua jukumu lenye changamoto kubw ala kuifundisha Akbou yenye makao yake katika Mji wa Kabylia na kuipa ahueni ya kutoshuka daraja. Katika mechi za kukumbukwa huko Algeria aliongoza timu yake kuzifunga vigogo kama vile SC Constantine, USM Alger na MC Alger ambayo ilikuwa bingwa wa Ligi kuu na hatua ya robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika.
Uzoefu timu ndogo
Folz anafahamu namna ugumu wa kiti cha kuwa kocha mkuu. Katika maisha yake ya ukocha amewahi kukalia kiti cha kocha mkuu wa klabu za Marumo Gallants na AmaZulu zote za Afrika kusini. Ligi Kuu ya Afrika kusini maarufu kama PSL, ni ngumu na inahitaji kocha mwenye ustahimilivu, na kila timu inazo bajeti nzuri na malipo mazuri. Lakini ni Ligi ambayo timu ndogo kupenya mbele ya vigogo ni changamoto. Ni sababu hiyo kila msimu wawakilishi wao kwenye mashindano ya CAF zinasikika timu za Mamelodi Sundowns na Orlando Pirates.
Maneno ya Arsene Wenger
Folz ni kijana anayewavutia makocha wengi wakongwe akiwemo Arsene Wenger. Kocha huyo wa zamani wa Arsenal amekaririwa na vyombo vya habari mbalimbali kuwa anavutiwa na uwezo wa kiufundi wa Folz. Chombo kimoja cha habari kilidokeza kuwa Arsene Wenger ametoa mchango mkubwa wa kimawazo hadi jopo la uongozi wa Yanga kumteua Romain Folz kuwa kocha mkuu wa klabu yao. Arsene Wenger ambaye kwa sasa ni Mkuu wa idara ya Maendeleo ya Soka Kimataifa ya FIFA anadaiwa kuvutiwa na kukubali uwezo wa Folz kiufundi na angetamani kufanya naye kazi katika idara hiyo ya Shirikisho la soka la FIFA.
Soka lake, ufundi wake
TANZANIASPORTS ilibahatika kuona video mbalimbali za mifumo ya mazoezi ya kocha Romain Folz mapema mwaka 2024. Kocha huyo anapenda timu inayocheza pasi za kutosha, nguvu, kasi na ufungaji mabao mengi. Katika falsafa hii Folz anahusudu zaidi mabadiliko ya ndani kwa ndani ya kutoka kwa wachezaji. Mabadiliko ya nafasi kwa ndani, upigaji pasi zenye uhakika, kushambulia kwa pamoja, kurudi nyuma kusaidia ulinzi kwa pamoja. Kifupi Folz ni kocha ambaye anataka kuona kila mchezaji anashiriki kwa aislimia 100 kwenye kushambulia na kujilinda. Ni sahihi kusema anapenda pasi nyingi, udambwidambwi mwingi na zaidi anahitaji wachezaji wabunifu zaidi na wenye nguvu za mwili katika kukabiliana na wapinzani wababe. Na mfumo anaoendelea zaidi ni ule wa 3-4-2-1 ambapo katikati ya dimba kunakuwa na shughuli ya viungo wa kibabe na wabunifu kuelekea langoni mwa adui.
Njia ya Ramovic
Ramovic alikuja Yanga akiwa kocha mwenye wasifu mdogo kuliko hata wachezaji wake. wachezaji wa Yanga wana wasifu mkubwa ikiwemo kushiriki Ligi ya Mabingwa na kufika hatua ya robo fainali, pia fainali ya Kombe la Shirikisho. Hivyo basi Sead Ramovic alikuja Yanga kama kocha ambaye hajui ladha na raha ya mashindano hayo. Ramovic alikuja Yanga, ni klabu ambayo ilimfungulia maisha na kwenda kuonwa na vigogo wa sokma wa huko Algeria. Bila Yanga kumpa nafasi ya kuonekana kwenye mashindani ya Kimataifa huenda ingemchukua muda mrefu.
Hali kadhalika Folz anakuja Yanga katika njia ileile ya Ramovic, anawakuta wachezaji waandamizi ambao wana wasifumkubwa kumzidi yeye. Ni wachezaji ambao wameshampa maisha kocha mwezake aliyeondoka Ramovic. Folz naye anaweza kuitumia Yanga kupandisha daraja la jina lake na wasifu wake.
Makocha wa Afrika kusini
Wimbi la Makocha wa PSL kumiminika nchini linaonekana kuwavutia hata wadau wa soka. Miguel Gamondi aliwahi kufundisha Afrika kusini. Hali kadhalika Troti Moloto amewahi kuifundisha Simba lakinia alitokea Afrika kusini. Fadlu Davids aanaifundisha Simba akitokea Afrika kusini. Sead Ramovic alikuja Yanga akitokea Afrika kusini. Na sasa Romain Folz anakuja Yanga akitokea Afrika kusini.
Hii maana yake makocha wa kigeni hasa kutokea PSL wamegundua fursa za kufundisha soka Ligi kuu. Ni Ligi ambayo inazidi kuchanja mbuga kuelekea kwenye mafanikio zaidi. Hii ni Ligi ambayo inazidi kuwavutia wataalamu zaidi. Huenda makocha mbalimbali watakuja Ligi Kuu Tanzania mahali ambako ni jukwaa lingine ya kukuza ufundi wao na wasifu kwa ujumla.


Comment*romain forz ni kocha bora kwa timu kama yanga kwasababu yanga inahistoria ya kuleta makocha wasio julikana hata sv zao lakini wakija wanafanya makubwa;
Comment*romain forz ni kocha bora kwa timu kama yanga kwasababu yanga inahistoria ya kuleta makocha wasio julikana hata sv zao lakini wakija wanafanya makubwa;