Mabingwa watetezi wa Ligi Kuu ya England (EPL), Manchester City na kocha wao, Manuel Pellegrini wapo katika sintofahamu.
Walianza vyema mechi zao lakini kadiri muda unavyokwenda wanajikuta wakiingia matatani, kwa kupoteza mechi, tena dhidi ya timu ndogo.
Walikuwa wakitetea vyema ubingwa wao, hata walipokuwa nafasi ya pili walikuwa pointi chache tu nyuma ya Chelsea, lakini sasa wapo nafasi ya nne, wakiwa pointi tisa nyuma ya vinara hao.
Wapo katika uwezekano wa kumaliza ligi kwenye nafasi hiyo ya nne ikiwa hawatabadilika, lakini wakienda vyema huenda wakashika nafasi ya pili na kwa ile ya kwanza inaonekana ni ngumu, maana Chelsea wana mechi moja mkononi.
Crystal Palace ndio waliowagawia maumivu makali zaidi kwa kuwapiga 2-1 wikiendi iliyopita katika dimba la Selhurst Park.
Wanaweza kutamba kuwa wataingia kwenye Ligi ya Mabingwa Ulaya (UCL) msimu ujao, kwa sababu wana pointi saba zaidi ya wanaowafuata, Liverpool, lakini hiyo bado haitoshi.
Matajiri wa Mashariki ya Kati walionunua klabu hiyo hawakufanya hivyo ili washike nafasi ya nne, wamekuwa wakitaka watwae ubingwa EPL, wasonge mbele vya kutosha UCL kwa hiyo hatima ya Pellegrini nayo iko matatani, kwa sababu namna walivyo sasa ni mbaya kuliko ilivyokuwa kwa Roberto Mancini alipofutwa kazi.
Huenda mechi dhidi ya Manchester United wikiendi ijayo ikaamua hatima hiyo, maana ni ya watani wa jadi na mshindi yeyote atapanda juu ya mwenzake, kwani wanapishana kwa pointi moja, United wakiwa na 62 na City 60.
City hawajaonekana kufanya vyema na kujituma ipasavyo kwenye mehi kadhaa, kiasi kwamba hata kocha alimweka pembeni nahodha Vincent Kompany kabla ya kumrejesha lakini bado hakuna matunda.
Mbaya zaidi ni kwamba wawekezaji ambao ni matajiri wa visima vya mafuta wamenunua wachezaji ghali na wengi.
Ilifika mahali kocha na wadau wakawa wanajitamba kuwa wana wachezaji wawili imara katika kila nafasi, lakini sasa hakuna kinachoonekana uwanjani.
Manchester City walitumia zaidi ya pauni milioni 200 chini ya Mancini na wakiwa na Pellegrini licha ya kutwaa ubingwa msimu uliopita, kikosi hakilipi ipasavyo.
Wamenunua watu kama beki Eliaquim Mangala licha ya kununuliwa kutoka Porto kwa bei kubwa ya pauni milioni 32 wakati Fernando aliyenunuliwa kwa pauni milioni 12 kutoka huko huko hajaonesha cheche.
Wilfried Bony aliwasili akitoka Swansea City kwa pauni milioni 25 Januari kwa ajili ya kuziba mapengo ya kwenye ushambuliaji lakini mambo hayaendi vyema.
Wachezaji wengi walitarajiwa wang’are kwa kusajiliwa kwa bei kubwa, kama vile Stevan Jovetic, Alvaro Negredo, Martin Demichelis, kipa Willy Caballero.
Hata beki aliyewaliza Arsenal kwa kuwaacha akiondoka kama mchezaji huru, Bacary Sagna amezorota na wakati mwingine hapati namba, huku kiungo mahiri aliyekuwa Chelsea, Frank Lampard ameshindwa kuwapaisha.
Kuna watu waliokuwa matata kama David Silva, Sergio Aguero, Edin Dzeko lakini mambo hayaendi na inaelezwa kwamba kikosi kinatakiwa kubadilishwa, lakini utabadili umsajili nani? Labda wageukie chipukizi kama Arsenal.
Katika hali hiyo, labda kocha ndiye tatizo, na ni kwa sababu hii matajiri wa mafuta wanaweza kuamua kubadili kocha mwishoni mwa msimu au hata kabla kama walivyofanya kwa Mancini.
Hawapendi kuona City wakiwa nyuma ya United, Arsenal na Chelsea.
Comments
Loading…