in , , ,

KERR ANATARAJIA MIUJIZA

Kwenye msimu wa Ligi Kuu ya Tanzania bara wa 2011/12 Simba SC walitwaa ubingwa wao kwa mara ya mwisho. Imepita misimu mitatu sasa timu hiyo haijafanikiwa kumaliza ligi katika nafasi mbili za juu.

Ni Yanga na Azam FC zimekuwa zikibadilishana nafasi hizo mbili.

Kwa sasa wekundu hao wa Msimbazi wapo kwenye maandalizi kwa ajili ya msimu ujao.

Gazeti moja la hapa nyumbani liliripoti katika moja ya matoleo yake ya karibuni kuwa kocha wa timu hiyo Dylan Kerr alisema kuwa kikosi chake kinajiandaa vizuri kwa ajili ya msimu ujao kikiwa na lengo la kumaliza ligi katika nafasi mbili za juu.

Wanafanya maandalizi hayo ili kupata nafasi ya kushiriki michuano ya kimataifa. Kiuhalisia wana kikosi kizuri. Uwepo wa nyota kama Mohammed Hussein, Said Ndemla, Jonas Mkude na wakali wengine unaweza kumpa matarajio makubwa kocha Kerr na wapenzi wa Simba.

Hivi karibuni pia wamesajili nyota wapya kadhaa wakiwemo Hamisi Kiiza na Mwinyi Kazimoto. Hata hivyo kuna mambo mawili yananitia mashaka. Nayaona kuwa ni vikwazo imara dhidi ya matumaini ya kocha Kerr.

Jambo la kwanza ni uimara wa vikosi vya timu za Azam FC na Yanga. Timu hizi mbili zina vikosi vizuri zaidi ya kile cha Simba.

Sioni namna ambavyo Simba inaweza kumaliza juu ya yoyote kati ya timu hizi. Ukiwatazama Azam kwenye michuano ya Kagame inayoendelea jijini Dar-es-salaam utakubaliana na mimi kuwa kuna uwezekano mkubwa wa timu hiyo kutwaa ubingwa wa ligi kuu msimu ujao.

Serge Wawa, Aggrey Morris na walinzi wengine wameonyesha uimara kwenye safu ya ulinzi. Azam hawajaruhusu bao lolote kwenye michuano hiyo kwenye michezo mitatu waliocheza mbaka sasa.

Kwenye safu ya kiungo pia Salum Abubakary, Himid Mao, Frank Domayo na wengine wameonyesha viwango.

Pia Azam wamefunga mabao 8 kwenye michezo mitatu. Ni ishara kuwa John Bocco, Kipre Tchetche na washambuliaji wengine wa Chamazi wanatisha. Usajili wa Ramadhani Singano na Allan Wanga umeiongezea makali zaidi ya safu ya ushambuliaji.

Yanga nao wameonyesha ubora kwenye michuano ya Kagame ingawa walipoteza mchezo wa kwanza dhidi ya Gor Mahia. Wanayumba kidogo kwenye safu ya ulinzi ila kwenye kiungo na ushambuliaji wameonyesha uimara.

Mshambuliaji wao mpya Malimi Busungu ameonyesha uwezo kwa kupachika mabao matatu mbaka sasa. Bado wana Simon Msuva aliyenyakua tuzo ya mfungaji bora wa ligi kuu msimu uliopita kwa kupachika mabao 17 na Amis Tambwe aliyeshika nafasi ya pili.

Ingawa Simba hawashiriki michuano ya Kagame na bado hawajacheza mchezo wowote mkali wa kujipima nguvu lakini unaweza tu kuona kuwa kikosi chao kimekuwa dhaifu zaidi baada ya kuondoka kwa Okwi na Singano.

Kwa namna timu za Azam na Yanga zilivyo Simba wana kibarua kigumu.
Jambo lingine ambalo naliona ni kikwazo dhidi ya matarajio ya Kerr ni yeye mwenyewe. Hapa naziruhusu rekodi zicheze mpira. Mwaka jana alikuwa kocha mkuu wa Hai Pong FC ya Vietnam.

Hakuweza kuipa mafanikio Hai Pong FC kwenye ligi kuu ya Vietnam. Alimaliza katika nafasi ya 10 kati ya timu 12. Alichofanikiwa ni kushinda kombe la ‘FA’ la Vietnam.

Kwenye ligi akawa na matokeo mabaya mno baada ya kufungwa michezo 11 kati ya 22 huku akishinda michezo 5 na kutoa sare 6.

Nikimtazama Kerr, kikosi chake na namna vikosi vya sasa vya Azam na Yanga vilivyo nakosa chaguo zaidi ya kuhitimisha kuwa Simba hawana uwezo wa kumaliza kwenye nafasi mbili za juu kwenye ligi kuu msimu ujao. Kerr anatarajia miujiza.

Report

Written by Kassim

What do you think?

71 Points
Upvote Downvote

Van Gaal: Mke ataniondoa United

Platini kuwa bosi wa Fifa?