in , ,

KATIKATI YA GIZA LA MARTIAL KUNA PENZI ZITO LA MASHABIKI

Upendo alianza kuutengeneza alipofika katika uwanja wa Old Trafford akiwa kama kijana mwenye kipaji cha hali ya juu.
Kipaji ambacho kilibeba matumaini ya watu wengi. Kila mtu alimtazama katika jicho lake. Kuna watu walimtazama kama kijana ambaye atakuja kuisumbua dunia kutokana na kipaji chake kikubwa, na wengine walifikia hatua ya kumtazama kama Thierry Henry ajaye.

Yule Gwiji wa Arsenal, Barcelona na timu ya taifa ya Ufaransa. Kwa karibu walikuwa wanarandana vitu vingi ndani ya uwanja.

Mbio zake zilibeba taswira ya Thierry Henry, chenga zake na aina ya magoli aliyokuwa anayafunga yalikuja kukamilisha kuwa huyu ndiye atakayekuwa Thierry Henry mpya.

Hapana shaka alikuwa na kipaji kikubwa ndani yake ndiyo maana ikafikia wakati akatabiriwa makubwa.

Na alitakiwa kwenda sehemu kubwa ili akaonesha makubwa yaliyokuwa katika miguu yake. Manchester United ikawa sehemu sahihi na salama kwake.

Alipelekwa sehemu ambayo vijana wengi wanaochipukia katika mpira hutamani hata kufika tu kuona majengo ya klabu husika.

Hii ni kwa sababu Manchester United ni moja ya klabu kubwa duniani. Klabu yenye mashabiki wengi duniani, klabu yenye pesa nyingi duniani na hapana shaka ni moja ya klabu yenye mafanikio makubwa kwa upande wa kuchukua vikombe.

Kwa hiyo historia imeifanya Manchester United kuonekana ni moja ya klabu kubwa duniani. Na bado ina hadhi kubwa mpaka sasa. Ni sehemu ambayo huwa ni fahari kubwa kwa mchezaji ngozi yake kufunikwa na jezi ya Manchester United.

Na ndiyo ilikuwa sehemu ambayo Antony Martial alibahatika kuvaa jezi ya Manchester United na Manchester United ikabahatika kumfanya Antony Martial kuwa mmoja wa wachezaji ndani ya uwanja wa Old Trafford.

Ilikuwa ni biashara yenye faida kwa kila upande. Manchester United ilinufaika na Anatony Martial alinufaika. Kazi ikabaki kwa Antony Martial kurudisha pesa za Manchester United ndani ya uwanja.
Hakukuwepo na mshambuliaji ambaye angeonekana kama ndiye mhimili wa timu kwa wakati huo kwani Wayne Rooney kasi yake ilikuwa inapungua kila jua lilipokuwa linachomoza na kuzama!.

Ikawa nafasi nzuri kwa Antony Martial kuonesha uwezo wake baada ya kupewa nafasi na Luis Van Gaal kama mshambuliaji kiongozi katika kikosi cha Manchester United.

Ulikuwa mtihani makubwa sana kwake!, mchezaji mpya, ndiyo kwanza akiwa katika msimu wake wa kwanza na akiwa hajakomaa vizuri tena akiwa na umri mdogo akakabidhiwa uongozi wa kuiongoza safu ya ushambuliaji ya Manchester United.

Hapo ndipo ilikuwa mwanzo kwake yeye kujenga asali ya upendo ndani ya mioyo ya mashabiki wengi wa Manchester United. Asali ambayo ilikuwa tamu kwao, asali ambayo unaweza kuiona kama imeenda kuwatia upofu mashabiki wa Manchester United.

Kwani kwa muda huu , Antony Martial ndiye mchezaji ambaye anapenda zaidi ndani ya kikosi cha Manchester United na mashabiki. Wanamwamini sana!, wanamkubali sana! na wanaamini hakuna mshambuliaji mwenye uwezo makubwa ndani ya kikosi cha Manchester United kama Antony Martial ila amekosa kuaminiwa tu.

Wanamini katika kumpa nafasi, hawaamini katika kuwekwa benchi kwa Antony Martial. Imani yao iliyojengeka kuanzia mwaka 2015 mpaka sasa hivi haijapotea.

Antony Martial aliwekeza mbegu ya imani baada ya kuaminiwa na Louis Van Gaal. Aliwaonesha mashabiki wa Manchester United hakika yeye ni Thieryy Henry ajaye na akawaomba kupitia miguu yake kuwa wamuunge katika safari yake ndefu ya kufikia sehemu ambayo Thierry Henry aliwahi kufika.

Kwa pamoja waliweka agano la pamoja, wakaahidiana kupendana katika shida na raha. Kwenye kila mapito waliyokuwa wanayapitia waliapa kupita kwa pamoja bila kuachana.

Ndiyo maana leo hii unaweza kumuona Antony Martial anapitia wakati mgumu sana, kuanzia kwenye klabu yake mpaka timu ya taifa ya Ufaransa lakini mashabiki wako nyuma yake.

Hawataki kumwacha aendelea kulia alipoangukiwa, kila akianguka wanamwinua na kumsihi akimbie bila kujalisha ugumu ambao anaokutana nao.

Wao wanaamini kupitia ugumu, wanaamini ugumu humtegengeza shujaa. Kwao wao Antony Martial ni shujaa mkubwa ajaye ndiyo maana hawataki kumwacha katika nyakati hizi ngumu anazopitia.

Haijalishi kwa kiasi kipi hapati nafasi katika kikosi cha Manchester United lakini wao wanaamini kupitia kipaji chake, ndiyo maana hufaraha huvaa miili yao kila wanaposikia jina la Antony Martial likijumuishwa katika kikosi cha Manchester United.

Ulitazama usiku wa ulaya katikati ya wiki hii?, ulitazama mechi ya Young Boys na Manchester United?, mechi ambayo Antony Martial alianza na ni mechi ambayo alifanikiwa kufunga goli lake la nne tangu January mwaka huu!.

Goli hili lilielezea ni jinsi gani ambavyo Antony Martial alivyo na maana kubwa ndani ya mioyo ya mashabiki wa Manchester United. Walimshangilia sana, hawakumzodoa alipokosoa, walimpa nguvu na kumwaminisha kuwa anaweza kufanya kitu kikubwa.

Antony Martial alijitoa kulipa mapenzi mazito yaliyokuwa yanaoneshwa na mashabaki wa Manchester United. Hata baada ya mechi kuisha, Antony Martial alikuwa ndiye mchezaji wa mwisho kutoka uwanjani.

Alitumia muda wake kuwashukuru mashabiki wa Manchester United waliosafiri kwa ajili ya kuishangilia timu. Pendo lao lilikuwa na maana kubwa sana kwa Antony Martial. Moyo wa Antony Martial ulikuwa unabubujikwa na chozi la furaha kwa sababu pamoja na nyakati ngumu anazopitia, pembeni yake kuna bega mahususi la kuegemea kwa ajili ya kupata faraja, penzi la mashabiki wa Manchester United ni taa muhimu katika giza zito linalofunika maisha ya Antony Martial kwa sasa.

Report

Written by Martin

Martin Kiyumbi ni mchambuzi wa habari za michezo na mbunifu wa maudhui.

Martin Kiyumbi amewahi kufanya kazi za uchambuzi kwenye vituo mbalimbali vya habari kama Tanzaniasports (tovuti ya habari za michezo ), Jembe FM , Radio Free Africa na TVE.
Martin Kiyumbi anapatikana kwenye e-mail ya [email protected]

What do you think?

71 Points
Upvote Downvote
Tanzania Sports

Ukurasa wa Mwisho wa kitabu cha John Bocco utakuwa wa Majonzi

Tanzania Sports

TUNAUFICHA UKWELI KWENYE MAMBO YA UCHAWI