in , ,

TUNAUFICHA UKWELI KWENYE MAMBO YA UCHAWI

Sikukuu ya Simba na Yanga jana ilimalizika. Ushindani ulianza nje ya uwanja kabla hatujahamia ndani ya uwanja.

Sehemu pekee ambayo ukweli huwa haujifichi. Huwezi kuficha ukweli ndani ya uwanja kwa sababu ndiyo sehemu pekee ambayo nyeusi huonekana nyeusi na nyeupe huonekana nyeupe.

Ndiyo sehemu ambayo mara nyingi huwa inatuhukumu sisi kutokana na maneno mengi ambayo huwa tunayatumia kuwasifia wachezaji wetu.

Ndiyo sehemu ambayo magazeti yetu huonekana yanapamba vinyago vya Simba. Vinyago ambavyo having’ati hata kutisha havitishi.

Ndiyo sehemu ambayo ukweli huwa uchi. Ni ukweli usiofichika tuna wachezaji wa kawaida sana katika sekta hii ya mpira.

Wachezaji ambao hupambwa na kuonekana kama wachezaji ambao ni bora na wana uwezo mkubwa sana ndani ya uwanja ilihali ni wachezaji wa kawaida sana!.

Ukawaida wao huanzia kwenye malezi yao wanayoyapata.Wachezaji wengi hukulia katika mazingira ambayo hayawapi nafasi wao kuwa wachezaji bora kama tunavyotamani sisi.

Ni mazingira ambayo hawalelewi na kufundishwa namna ya kuwa mchezaji mkubwa duniani, badala yake wanaonekana kama wachezaji wa kawaida sana ambao wanacheza mpira kama burudani na siyo kazi.

Kwao wao suala la mpira kama kazi halipo kwa asilimia kubwa kwa sababu wakati wakiwa wadogo walikuwa wanapitia mazingira ambayo yalikuwa hayafundishi kuwa mpira ni kazi.

Hakuna kituo cha kuibua, kulea na kukuza vipaji ambacho kimehusika kuwatengeneza hawa vijana wa Leo. Mitaa ndiyo imewakuza, na hata walipofikia wamefika bila wao kujua kwanini wamefika hapo.

Hayo ndiyo maisha halisi, maisha ambayo yanatoa nafasi kwa vijana wetu kutokuwa na nidhamu ya kitu chochote wanapokuwa uwanjani.

Hawana nidhamu ya nafasi ambazo huzipata, hawana nidhamu ya kila mpira unapokuja katika miguu yao ndiyo maana ni vyepesi kwao wao kupoteza mipira kirahisi.

Kwa kifupi akili zao hazijakomaa ipasavyo mpaka kufikia kuitwa hawa ni wachezaji wa kulipwa, tunawachezaji wachache sana ambao wanaweza kufikia hadhi ya kuitwa ni wachezaji wa kulipwa ila wachezaji wengi tulio nao ni wachezaji wa burudani.

Kwao wao burudani inatangulia na kazi haipo katika akili zao ndiyo maana ni rahisi sana kufanya makosa ambayo hayana ukomavu ndani ya uwanja.

Jana kuna nafasi nyingi sana ambazo timu ya Simba imekosa, na hii ni kutokana na kukosa aina ya wachezaji ambao wanaukomavu katika maamuzi.

Tuna wachezaji ambao hawana ukomavu mkubwa katika maamuzi yao ndani ya uwanja, wachezaji hawa hawa ndiyo wanatusababisha tuone kuwa kuna njia za kishirikina ambazo zinatumika katika mchezo husika.

Kwa sababu akili zetu zinapenda kujadili vitu vya ajabu, vitu visivyo kuwa na maana yoyote na sisi hujikuta tunaamini kabisa kuhusu ushirikina katika mpira!.

Tunakosa kabisa muda wa kujadili mambo kiufundi na tunaendekeza kuyapa muda mrefu mambo yasiyokuwa na maana katika majadiliano yetu.

Tuna uhakika ushirikina una nafasi kubwa katika mpira ?, kwanini hatufanyi vizuri katika michuano ya kimataifa?, kwanini Yanga imetolewa katika hatua ya makundi ya kombe la shirikisho barani Afrika?.

Kwanini timu yetu ya taifa haifanyi vizuri katika michuano ya kimataifa, kwanini tusitumie ushirikina angalau tufuzu Afcon?.

Ni ujinga kuyapa nafasi kubwa mambo yasiyokuwa na umuhimu katika vinywa vyetu, vinywa vyetu tuvitumie kujadili namna ambavyo tutapata wachezaji bora ambao watakuwa na ukomavu mkubwa katika matumizi ya kila nafasi ambazo huzipata.

Tujadilini namna ambavyo vilabu vyetu vinavyotakiwa kuwa viwanda vya kuzalisha wachezaji bora kwa kuwekeza katika misingi bora ya mpira.

Misingi ambayo itakuwa inatupa njia bora ya sisi kupata wachezaji wanaojitambua wakiwa uwanjani, wajitambue kuwa wapo uwanjani kwa ajili ya kufanya kazi na kila nafasi wanayoipata ni muhimu mkubwa sana katika ufanisi wa kazi zao.

Tusiukumbatie ukweli na kuuachia uongo uonekane ni kitu cha msingi katika jamii yetu. Hatutofika , lazima tukubali kuwa hatuna wachezaji bora ambao wanaweza kutumia wastani mzuri wa nafasi wanazopata kwa kufunga magoli.

Hatuna Clinical Finishers, na hatutaki kabisa kufanya mikakati ya kuwaibua hawa ili wake kuwa msaada mkubwa katika mpira wetu.
Kiongozi anatakiwa awe na njia mbadala katika kuinua mpira wetu na siyo kuongea vitu ambavyo havina msaada katika maendeleo ya mpira wetu.

Report

Written by Martin

Martin Kiyumbi ni mchambuzi wa habari za michezo na mbunifu wa maudhui.

Martin Kiyumbi amewahi kufanya kazi za uchambuzi kwenye vituo mbalimbali vya habari kama Tanzaniasports (tovuti ya habari za michezo ), Jembe FM , Radio Free Africa na TVE.
Martin Kiyumbi anapatikana kwenye e-mail ya [email protected]

What do you think?

71 Points
Upvote Downvote
Tanzania Sports

KATIKATI YA GIZA LA MARTIAL KUNA PENZI ZITO LA MASHABIKI

Tanzania Sports

JONAS MKUDE, HADITHI AMBAYO TULIKUWA TUKIITAMANI