England iliwahi kuwa na mchezaji ambaye mpaka anamaliza soka lake la
ushindani mashabiki wengi walikuwa hawaamini kama kweli alimaliza soka
bila mafanikio makubwa yake binafsi na makombe kwenye timu.
Mchezaji ambaye waliamini ndiye mchezaji ambaye alikuwa na uwezo
mkubwa wa kufunga magoli.
Wastani wake wa kufunga magoli ulikuwa 0.667 ambapo ukifanya makadirio
alikuwa na wastani wa kufunga goli moja kwenye kila mechi.
Siyo jambo la kushangaza kwa sababu mpaka sasa ndiye mchezaji ambaye
anaongoza kufunga magoli mengi kwenye ligi kuu ya England akiwa na
magoli 283.
Ligi ambayo inasemekana ndiyo ligi ngumu, yenye kutumia kasi na nguvu
kwa pamoja, lakini mwanaume huyu alikuwa anawatesa makipa na mabeki
bila kujali ugumu wa ligi.
Ndiyo maana hata mchezaji bora wa duniani wa wakati wote Pelle aliwahi
kudiriki kumtaja kwenye orodha yake ya wachezaji bora 100 wa muda
wote.
Hii yote ilionesha alikuwa mchezaji wa pekee mwenye uwezo mkubwa.
Waingereza walijivunia naye kwa sababu ya uwezo wake.
Waingereza walitamani kumuona anachukua tuzo ya FIFA mchezaji bora wa
dunia au ya ballon d’or.
Matamanio yao yalikuwa makubwa sana juu ya Allan Shearer.
Mchezaji ambaye alijiwekea utawala wake katika vilabu ambavyo kwa
macho ya nyama vilionekana vidogo.
Hapana shaka Shearer alikuwa mshambuliaji wa kiwango cha juu, ambaye
kila timu kubwa ilitamani kuwa naye kwenye kikosi.
Mpaka sasa ameacha alama kubwa sana kwenye ligi kuu ya England. Alama
ambayo haikuwa na msaada wowote katika kuchukua tuzo za Ballon d’or.
Tuzo ambazo kila mchezaji duniani anatamani siku moja aweze kufanikiwa kupata.
Ndiyo maana hata Harry Kane ameshakili kuwa anatamani siku moja
achukue tuzo ya Ballon D’or.
Ni jambo ambalo siyo la kushtusha kwa sababu Harry Kane kwa sasa ni
mmoja wa washambuliaji wa daraja la juu.
Amefanikiwa kufika daraja la juu la washambuliaji bila yeye kuchukua
hata kikombe kimoja.
Ni mfungaji bora wa ƙligi kuu ya England kwa misimu miwili mfululizo
huku timu yake ikishika nafasi ya tatu na ya pili ndani ya misimu hiyo
miwili.
Mpaka sasa amefunga magoli 28 katika mechi 23 zilizopita.
Katika umri wake wa miaka 24 inaonesha tayari ameshakomaa, tayari yupo
daraja la juu la washambuliaji bora duniani.
Daraja ambalo linampa nafasi kubwa kuwania na kushinda tuzo ya Ballon D’or.
Katika umri wa miaka 24 tayari ameshafunga magoli 104 , ana miaka
mingine 5 ya kucheza soka la ushindani miaka ambayo itadhihirisha kuwa
Kane ni moja ya washambuliaji bora kwenye ardhi ya England.
Magoli pekee hayatoshi kumfikisha katika matamanio yake ya juu ya
kuchukua Ballon D’or.
Kufunga na kutoa pasi za mwisho za magoli siyo karata ya mwisho ya
yeye kuchukua tuzo hiyo.
Miaka inakimbia sana, anatakiwa kutafuta vitu vya kujivunia.
Vitu vitakavyomsaidia kufikia katika matamanio yake ya juu.
Vitu ambavyo vitaacha alama katika soka la England na duniani kwa ujumla.
Vitu hivo ni makombe.
Muda huu, ni muda muafaka kwa Harry Kane kushinda makombe .
Ni muda wa yeye kubeba kikombe cha ligi yoyote kubwa duniani ( EPP, LA
LIGA, BUNDESLIGA).
Ni muda kwake yeye kushinda kikombe cha ligi ya mabingwa barani ulaya
yani ( UEFA).
Vyote hivi hawezi kuvipata katika timu shindani ila atavipata katika
timu bingwa.
Asione aibu kuikana Spurs na kufuata mafanikio mahali pengine.
Spurs ni timu nzuri, ila siyo timu bora ambayo ina ubora wa kushindana
na miamba mikubwa ya soka barani ulaya.
Jezi ya Spurs inamcheleweshea mafanikio yake binafsi.
Alan Shearer aliikataa Barcelona, hii ilikuwa na maana aliyakataa
mafanikio yake binafsi kwa kuendelea kuwepo Newcastle United.
Kama Shearer angekubali kuvaa jezi ya Barcelona leo hii jina lake
tungelisoma katika orodha ya wachezaji ambao walibeba Ballon D’or.
Kitu hiki hatakiwi kukifanya Kane, hatakiwi kuyakataa mafanikio yake
binafsi. Vitabu vya kumbukumbu vitamkumbuka na kumtukuza zaidi kwa
mafanikio yake binafsi.
Asisite kuikana njia aliyopitia Shearer na kuamua kuchagua njia yake
binafsi ambayo itakuwa na msaada mkubwa katika mafanikio yake binafsi.