in , , ,

JUVENTUS NA REAL MADRID WANA 60% YA KWENDA CARDIFF

Jana kwenye mechi ya Monaco na Juventus kuna vitu vingi ambavyo
vilikuwa vinasubiriwa kwa hamu vitokee, moja ya kitu kikubwa ni
kusubiri kuona kama Monaco ambayo ilikuwa na safu imara ya
ushambuliaji kama inaweza ikavunja mwiko wa Juventus wa kutofungwa
hata goli moja kwenye michezo mitano iliyopita ya ligi ya mabingwa
msimu huu.

Kwangu mimi mshangao mkubwa ulianzia kwenye mabadiliko ya kikosi kwa
timu zote. Juventus walimwanzisha Andrea Barzaghi na kumuacha nje Juan
Cuadrado.

Kitu ambacho kilimpa nafasi Dani Alves kucheza kama Wing Back Right.
Yawezekana wewe ukawa mmoja wa watu ambaye mlikatishwa tamaa na ujio
wa Dani Alves Juventus akitokea Barcelona.

Ilikuwa rahisi kwa mtu kutabiri mwisho wa Dani Alves lakini kwa msimu
huu ametoa jibu sahihi kuwa kuja kwake Juventus hakukuwa mwisho wake
kisoka. Mpaka sasa ametoa msaada wa magoli manne kwenye michuano hii
ya ligi ya mabingwa barani Ulaya.

Jana alionesha uwezo wake mkubwa wa kuilazimisha timu ikabe vizuri
upande wake wa kulia na ishambulie vizuri upande wake wa kulia.

Ushirikiano wake na Andrea Barzaghi ulikuwa unaleta ugumu mkubwa
katika eneo lao la ulinzi , pita alifanikiwa kuleta mlinganyo mzuri
kati ya eneo la kushambulia na eneo la kuzuia . Ushirikiano wake mzuri
na Higuain katika upande wa kushambulia ulisababisha wafanikiwe kupata
magoli mawili.

Higuan bado yupo na ataendelea kuwepo, jicho lake halijapofuka,
analiona vizuri goli na ana vipimo sahihi vya kupitishia mpira kwenye
goli.

Mario Mandzukic ni Wingback mpya , Massemiliano Allegri ameamua
kutuzalishia mtoto mpya. Na amefanikiwa kutuletea mtoto ambaye
anatimiza majukumu yake ipasavyo.

Kwa kusaidiana na Sandro wamefanikiwa kujitengenezea mazingira mazuri
ya kuilinda timu.

Real Madrid waliwafanya Atletico Madrid wawe wanyonge, Atletico Madrid
iliyokuwa inapigana kwa nguvu zote na kwa muda mwingi wa mchezo
haikuonekana juzi.

Varane alicheza vizuri tofauti na matazamio ya wengi wetu. Yeye na
Sergio Ramos walitengeneza ukuta imara uliosababisha kutowapa nafasi
Gameiro na Antoinne kufurukuta.

Ronaldo kasi yake inapungua, lakini kuna kitu ambacho hakipungui kadri
muda unavyozidi kwenda nacho ni uwezo wake wa kufunga magoli.

Kwa sasa amekuwa mtu ambaye yuko makini sana na goli kuliko vitu
vingine kwa sababu anajua kabisaa kwa sasa magoli ndiyo yatampa nafasi
ya kuwepo kwenye ramani kuliko chenga za maudhi na sanaa zingine.

Wakati umakini mkubwa wa kufunga magoli ukiwa unaongezeka kwa Ronaldo
lakini Benzema anazidi kupunguza umakini kwenye hili.

Mara ya mwisho kwa Benzema kufunga kwenye michuano ya ligi ya mabingwa
ilikuwa kwenye mechi dhidi ya Napoli ya kumi na sita bora mpaka sasa
hivi hajafunga.

Kitu ambacho siyo kizuri kwa mshambuliaji wa kati. Ni wakati sahihi
kwa Zidane kufikiria kumwanzisha Alvaro Morata maana amekuwa akifunga
kila anapoaminiwa.

Majeraha ya Bale yatakuwa faraja kwa Isco kwani anajua kabisaa huu ni
wakati wake sahihi wa kuitumia hii nafasi na kizuri zaidi anacheza
sehemu ambayo yuko huru kuwepo eneo lolote lile.

Kwa matokeo ambayo wamepata Real Madrid na Juventus wanajiwekea nafasi
ya asilimia 60% kwao kuvuka fainali.

Na hii itakuwa fainali bora kwa sababu timu hizi mbili ni bora kuzidi
timu zilizobakia kwa sasa

Report

Written by Martin

Martin Kiyumbi ni mchambuzi wa habari za michezo na mbunifu wa maudhui.

Martin Kiyumbi amewahi kufanya kazi za uchambuzi kwenye vituo mbalimbali vya habari kama Tanzaniasports (tovuti ya habari za michezo ), Jembe FM , Radio Free Africa na TVE.
Martin Kiyumbi anapatikana kwenye e-mail ya [email protected]

What do you think?

71 Points
Upvote Downvote
Serengeti boys

SERENGETI BOYS ITUPE FUNZO KWENYE MAENDELEO YA SOKA LA VIJANA

Tanzania Sports

MBAO FC KUFUTA UTEJA DHIDI YA KLABU ZA DAR BAADA YA MIAKA 16 ?