Jina la Divock Origi limerudi kwenye gumzo tena kwenye vyombo vya habari za michezo. Safari hii gumzo likiwa kwenye Ligi Kuu England maarufu kama EPL. Bao la ushindi alilofunga Origi muhimu kwenye mechi ya EPL na kumpa tabasamu kocha wake Jurgen Klopp limerudisha mjadala juu ya nafasi yake katika kikosi cha Liverpool.
Hata hivyo mjadala umeibuka hapo hapo, ni kwanini Klopp amekuwa akimweka benchi kwa muda mrefu nyota huyo? Swali hilo likiwa halijapatiwa majibu, Divock Origi akaongeza joto la mjadala katika mchezo wao wa mwisho wa Ligi ya Mabingwa Ulaya dhidi ya AC Milan ambako Liverpool waliibuka na ushindi wa mabao 2-1.
TANZANIASPORTS imeshuhudia na kufanya tathmini juu ya mjadala huo katika viunga mbalimbali vya wapenzi wa kandanda huku nyota ya Origi iking’ara kwa mara nyingine tena. Swali lilelile likarejea tena kwanini Klopp anamweka benchi nyota huyo? Wadau wa michezo wanaouliza swali hilo wanatazama rekodi za Origi namna anavyomwokoa Klopp katika mechi ngumu.
Pia anasifika kuwa na uwezo mkubwa wa wa kuwasoma mabeki wa timu pinzani na wapinzani wao kwa ujumla. Wadau hao wanarudia mechi ya ushindi ya nusu fainali kati ya Liverpool na Barcelona.
Liverpool wakiwa wamechapwa mabao 3-0 walitaka kupindua meza katika dimba la Anfield bila nyota wao Mohammed Salah aliyekuwa ameumia. Wakati dunia ikitaka kujua namna gani Klopp angeweza kupindua mechi ya mchezo huo na kusonga mbele, ndipo jina la Divock Origi likaibuka tena.
Origi alipachika bao la nne na ambalo liliwahakikishia nafasi ya kutinga fainali ya Ligi ya Mabingwa Ulaya. Katika pambano hilo Origi alicheza kwa sababu Mohamed Salah alikuwa majeruhi, hivyo akawa anashirikiana na Roberto Firmino na Sadio Mane.
Siku zote Liverpool imekuwa ikitambia wapinzani wake kupitia umahiri wa Salah,Mane na Firimino, lakini mambo yanapokwenda tofauti ndipo Divock Origi hugeukiwa na kutazamwa kama mwokozi wao. Ndivyo alivyofanya dhidi ya Barcelona.
Mbinu aliyotumia ni ileile ya kuwasoma mabeki wa Barcelona ambao hawakuwa wamejipanga kwa pigo la adhabu ya kona, ambapo Trent Alexander Arnold alipiga mpira haraka kuelekea kwa Origi ambaye akaupachika kimyani.
Wakati wengi wakiamini mchango wa Origi ni mkubwa, lakini Klopp akaamua kumsajili Diogo Jota ikiwa na maana ya kumweka kando kabisa Origi.
Changamoto ya aliyoleta Klopp ilidaiwa ni kutokana na kushuka kiwango cha Roberto Firmino, hivyo walihitaji mchezaji mbadala. Lakini Origi alikuwepo, hivyo kuibua swali labda Klopp anambagua nyota huyo raia wa Ubelgiji mwenye asili ya Kenya.
Wakati Diogo Jota akisifika kwa umahiri na kupewa muda mwingi wa kucheza, Origi yeye hukalia benchi na nafasi yake kuonekana kama inapotea kadiri siku zinavyokwenda mbele.
Lakini Klopp amekuwa akikabiliwa na wakati mgumu pale machaguo yake ya kwanza yanapofeli kuleta matokeo chanya kwa Liverpool, hivyo huamua kumgeukia Divock Origi.
Labda ndiyo sababu hakutaka kumuuza nyota huyo kwenda vilabu vingine, akihitaji abaki klabuni. Katika mazingira ya kumweka benchi na kutaka abaki klabuni hapo Origi hawezi kukuza thamani yake kupitia mkataba mpya kwa vile anakuwa mchezaji wa ziada na ambaye malipo yake hayawezi kulingana na Mane,Salah au Firmino.
Wakati Klopp akiwa kwenye hali hiyo anajikuta anahitaji huduma ya Origi. Gumzo lililotokea hivi karibuni lilimlazimisha Klopp kumpa nafasi Origi katika kikosi cha kwanza katika mchezo wao dhidi ya AC Milan.
Licha ya kutojihakikishia nafasi kwenye kikosi cha kwanza, lakini Origi ametoa mchango mkubwa na kuwa mwokozi wa Klopp kwenye mechi ngumu. Wadau sasa wanajiuliza, ikiwa Klopp alimhitaji sana Origi katika kikosi chake, ni kwanini alimsajili Diogo Jota?
Je Klopp anambagua Origi na kuwapendelea Salah,Jota,Mane na Firmino? Kujibu swali hilo huenda ikawa vigumu lakini ukweli ni kwamba Origi amekuwa mchezaji ambaye anaweza kupata nafasi katika timu yoyote ile ya EPL.
Ukitazama washambuliaji wa timu kama Manchester United,Arsenal,Chelsea na Manchester City utagundua nyota huyo anaweza kucheza katika vikosi vyao. Kinachoweza kumwondoa ni mifumo ya makocha tu sio uwezo wa washambuliaji.
Hakuna mshambuliaji wa kumtisha Origi pale Man United wala Arsenal. Pale Chelsea unaona kabisa nafasi ya Origi ipo, lakini nyita huyo yuko Liverpool ambako Klopp anamweka kama mchezaji wa ziada.
Je kwa mwenendo wake wa kumwokoa Klopp katika mechi ngumu utachangia kupewa nafasi zaidi kikosi cha kwanza au kuna namna fulani kocha wake amekuwa mbaguzi? Hilo na mengine ndiyo yanayoulizwa kwa sasa, kwanini hapangwi wakati anapachika mabao kila nafasi ndogo anayopewa? Bila shaka wasomaji wetu wa TANZANIASPIRTS watakuwa na maoni juu ya mwenendo wa Origi na Klopp.
Comments
Loading…