in , , ,

JOSE MOURINHO NA MANCHESTER UNITED NI VITABU VYA KISHUJAA

Historia daima hubaki ndani ya moyo wa mwanadamu. Ni ngumu sana kwa
mhuri wa historia uliopigwa kwenye moyo wa mwanadamu kufutika kwa njia
yoyote.

Kizuri zaidi historia hudumu pale unapofanya kitu chanya kwenye jamii,
ndipo hapo historia yako huwa na nyama au msuli mkubwa.

Ndipo hapo neno shujaa huzaliwa, kila mtu huzaliwa shujaa lakini
tunachotofautiana ni kwa njia zipi tunazotumia kuutafuta huo ushujaa.

Uchaguzi wa njia ndiyo hutoa matokeo tofauti katika maisha yetu. Wapo
wanaobahatika kuchagua njia ambayo ni nzuri ambayo huwafanikisha wao
kufika kwenye daraja na ushujaa, na kuna wengine hukosea kwenye
uchaguzi wa njia ya kupitia na ndiyo huwa sababu kwao kutoliona daraja
la ushujaa.

Shujaa huimbwa kwa mafanikio yake mafanikio ya mtu humweka katika
ngazi ya ushujaa na kila hubaki wa kimtazama.

Na ndiyo sababu kubwa ambayo inaifanya Manchester United kuwa klabu ya
kishujaa kutokana na mafanikio yake iliyoyapata.

Kuwa klabu ambayo imechukua makombe arobaini na tano (45) ambayo ni
mengi kuzidi klabu nyingine yoyote England hii inaifanya kuwa shujaa
ambaye anatazamwa sana.

Jana wamefanya kitu kikubwa cha kishujaa baada ya kuchukua kombe la
UEFA Europa Cup , kombe ambalo limeifanya Manchester United kuwa timu
pekee England kuchukua makombe yote iliyoshiriki na kuongeza thamani
katika ushujaa wao kwani wameonesha wanauwezo mkubwa wa kushinda
kwenye kila uwanja wa vita wanaoingia kupigana.

Ushajaa wao umeimarika tena umeimarika zaidi baada ya kukutana na
kocha ambaye ni shujaa pia.

Kocha ambaye ni rafiki wa vikombe ambaye anafanya kazi kwenye klabu
ambayo kuchukua kombe ni mila na desturi ya klabu, kuacha kuchukua
kombe ni sawa na kuvunja mila na desturi.

Muunganiko huu wa mashujaa wawili ndiyo ukaipa nafasi Manchester
United kuwa na njaa msimu huu.

Ni ngumu kwa kocha msimu wake wa kwanza tu ndani ya klabu kufanikiwa
kuchukua makombe matatu, lakini kwa Jose Mourinho imewezekana kwa
sababu ni shujaa ambaye alipata kuishi nchi ya kishujaa.

Lilikuwa jambo la kushangaza kusikia kocha akisema waziwazi kuwa hana
nia ya kushika kati ya nafasi nne za juu ili afuzu UEFA hii ni kwa
sababu alikuwa anajua ni kipi alichokuwa anakitafuta.

Aliamini kufuzu UEFA kupitia njia ambayo itampa heshima, njia ambayo
itabaki kwenye kumbukumbu za watu wengi na kuandikwa kwenye vitabu
vingi vya kumbukumbu.

Njia ambayo itawapa furaha wachezaji, benchi la ufundi, viongozi wa
timu, washirika wa kibiashara wa timu na mashabiki kwa ujumla.

Njia ambayo itamfanya shingoni mwake aongeze idadi ya medali ambazo
ziliwahi kupita shingoni mwake.

Ndicho kitu alichodhamiria kutimiza furaha yake, alifanya kila awezalo
ili afanikiwe kwa kiasi kikubwa.

Haikuwa ajizi kumwamini Rashford kwenye mechi ya fainali kwa sababu
aliweka sumu ya upambanaji ndani yake .

Hali ya ushindi ilikuwa inaonekana ndani ya wachezaji wa Manchester
United ambao kila mmoja alikuwa anapigana kutafuta ubingwa.

Ndani ya mishipa yao ya damu waliamini ubingwa ndicho kitu pekee
kitakachosaidia kusambaza damu kwenye miili yao kwa ufasaha.

Ndiyo maana hakuna hadithi kubwa ilikuwa kwenye kichwa chao kama
hadithi ya ubingwa, kila mtu alikuwa na uchu wa mafanikio ya usiku wa
jana. Mbele ya macho yao walikuwa wanaona ubingwa pekee na siyo kitu
kingine.

Nafsi zao zilitawaliwa na shauku ya kuvalishwa medali, hakuna kitu
ambacho ƙwalikiruhusu kiwe kama kikwazo kwao kwa sababu walikuwa
wanajua ni kipi wanachokitafuta.

Kwenye maisha uchaguzi wa jambo fulani ni muhimu na hakuna kitu
kinachotia moyo kama kuchagua kuwa sehemu ya historia ya ushujaa na
mwisho wa siku ukatunukiwa ushujaa mbele ya mashujaa.

Na hii yote ni kwa sababu walikuwa wanacheza ndani ya klabu ya
kishujaa chini ya kocha shujaa ilikuwa rahisi kwao kufungua kurasa ya
hivi vitabu viwili na kuvisoma ili wawe mashujaa pia.

Report

Written by Martin

Martin Kiyumbi ni mchambuzi wa habari za michezo na mbunifu wa maudhui.

Martin Kiyumbi amewahi kufanya kazi za uchambuzi kwenye vituo mbalimbali vya habari kama Tanzaniasports (tovuti ya habari za michezo ), Jembe FM , Radio Free Africa na TVE.
Martin Kiyumbi anapatikana kwenye e-mail ya [email protected]

What do you think?

71 Points
Upvote Downvote
Tanzania Sports

COURTOIS KUTWAA ‘GOLDEN GLOVE’ NI DHULUMA

Tanzania Sports

MAENEO YATAKAYOAMUA MECHI YA FAINALI YA FA KATI YA CHELSEA NA ARSENAL.