in , , ,

JOHN OBI MIKEL- ANAIKABA NIGERIA

Mechi tatu zinazowahusisha wawakilishi wetu wa bara la Afrika lakini hakuna hata mechi moja ambayo timu zetu zimefanikiwa kupata ushindi hata alama moja katika michezo yote.

Baada ya Nigeria kufanya vizuri katika mavazi, wengi wetu tulitaka kujua watafanya kipi kikubwa ndani ya uwanja na ikizingatia wachezaji wa Nigeria walitoa ahadi ya kufanya vizuri katika michuano ya kombe la dunia mbele ya raisi wao.

Walitujaza matumaini mengi tukasubiri kuona mwanzo wao, mwanzo ambao ulikuwa mbaya kwao.

Kwanini walianza vibaya?

Hapana shaka kuwa na wachezaji wengi ambao hawana uzoefu mkubwa katika michuano hii ya kimataifa ndiyo itakuwa ni sababu kubwa kwa Nigeria kupoteza mchezo wake wa kwanza.

Kwanini nasema hivo? Ukiangalia magoli yote mawili yalifanyika kwa sababu ya ukosefu wa kutoa maamuzi yaliyokomaa hasa hasa goli la pili ambalo lilifungwa kwa mkwaju wa penalty. Tukio la penalty lilitokana na mchezaji wa Nigeria kukosa maamuzi ya kikomavu mpaka akasababisha kufanya madhambi ambayo hayakuwa na ulazima kuyafanya.

Ukuta wa Croatia ulikuwa ni changamoto kwa Nigeria?

Hakuna kificho kwenye hili, ukuta wa Croatia ulikuwa mgumu kiasi ambacho kilisababisha Nigeria kutumia aina nyingine ya kushambulia ambayo hawajawahi kuitumia hivi karibuni , yani kushambulia kwa kutumia mipira mirefu na ya juu kitu ambacho hakikuwa na faida kubwa sana kwao.

Kipi walitakiwa kukifanya ?

Hapana shaka Mikel Obi ndiye ambaye alikuwa anaikaba Nigeria wakati wanashambulia, Croatia walikuwa na beki wa ziada aliyekuwa amevaa jezi ya kijani.

Kwanini nasema hivi?

Nigeria walikuwa wanakosa mtu wa kutengeneza nafasi za kufunga magoli kwa sababu Mikel Obi hana uwezo huo wa kucheza nyuma ya mshambuliaji wa mwisho kama alivyofanya Jana.

Ighalo alionekana yuko peke yake tena akiwa mpweke bila msaada wowote kwa sababu hakuwa anapata mipira mingi na hakuwa anapata msaada kutoka kwa wenzake.

Muda mwingi Mikel Obi alikuwa anashuka chini katikati hivo kufanya eneo la katikati uwanja kuwa na uwazi na eneo la mbele ya timu ya taifa ya Nigeria.

Kipi wangefanya ? Kasi ya Mikel Obi imepungua sana, hana msaada mkubwa sana akicheza eneo la nyuma ya mshambuliaji kama kipindi kile ambacho alikuwa na kasi nzuri.

Hivo kuna vitu viwili ambavyo Nigeria wanatakiwa kufanya cha kwanza ni kumchezesha Mikel Obi katika eneo la kiungo cha chini au mbele kidogo kwa Ndindi , ili kumpa nafasi Alex Iwobi kucheza nyuma ya mshambuliaji wa mwisho (Ighano).

Jana Alex Iwobi alionekana hana msaada mkubwa kwenye timu kwa sababu alitumia muda mwingi kucheza pembeni, eneo ambalo humuwia ugumu kucheza akiwa huru.Alex Iwobi huwa huru na msaada wake huonekana sana akicheza nyuma ya mshambuliaji.

Kumchezesha Alex Iwobi nyuma ya mshambuliaji kungesaidia sana kutotengeneza uwazi wa eneo la kiungo cha kushambulia na eneo la safu ya ushambuliaji la Nigeria, hivo kutomfanya Ighano aonekana yuko mpweke kule mbele.

Jambo la pili ni kutomwanzisha Mikel Obi. Umri umekwenda, anapunguza kasi ya mashambulizi ya timu.

Sawa anaonekana kama mtu mkongwe, mwenye uzoefu, na kiongozi ndani ya timu lakini linapokuja suala la ndani ya uwanja anakuwa hana faida kubwa sana kutokana na kasi yake kuonekana ni ndogo kulinganisha na kasi ya mchezo husika.

Kwa hiyo ni watu wapi ni sahihi kucheza katika eneo hili la kiungo?

Wilfred Ndindi , Etebo na Alex Iwobi wanafaa kucheza eneo hili ili kuendana na kasi ya mchezo na ubunifu katika eneo hili la katikati mwa uwanja.

Report

Written by Martin

Martin Kiyumbi ni mchambuzi wa habari za michezo na mbunifu wa maudhui.

Martin Kiyumbi amewahi kufanya kazi za uchambuzi kwenye vituo mbalimbali vya habari kama Tanzaniasports (tovuti ya habari za michezo ), Jembe FM , Radio Free Africa na TVE.
Martin Kiyumbi anapatikana kwenye e-mail ya [email protected]

What do you think?

71 Points
Upvote Downvote
Tanzania Sports

MESSI ALIFANYA KILA KITU SAWA KASORO KUFUNGA GOLI

Tanzania Sports

MISRI INATAKIWA KUSHUKA MGONGONI MWA SALAH