in

Jezi za YANGA zitauza AFRICA

Kuna vitu viwili ambavyo watu wanatakiwa kuvifahamu kuhusu jezi ya Yanga. Achana na uzuri au ubaya wa jezi hizi kitu ambacho mimi binafsi sitaki kukizungumzia.

Kuna kitu kimoja ambacho wafanyabiashara wengi huwa wanakitumia katika kukuza masoko kwenye bidhaa zao wanazozalisha.

Wafanyabiashara wengi huuza hisia zilizo ndani ya bidhaa ila huwa hawauzi bidhaa tu. Bidhaa ambazo huwa wanauza huongezewa hisia ambazo mara nyingi huongeza idadi ya mauzo.

Hisia huwekwa kwenye kama ujumbe maalumu wa kusukuma masoko. Mfano , Coca Cola wana ujumbe ambao unaosema “onja msisimko” ujumbe huu ndiyo hisia iliyoongezwa kwenye bidhaa ya Coca Cola.

Unapoenda kunywa Coca Cola huendi kunywa soda kama soda ila unaenda kunywa soda yenye msisimko wa ziada. Msisimko ni ujumbe wa ziada katika kukuza mauzo.

Unapoenda kununua bidhaa za Nike utakutana na ujumbe ulioandikwa “Just Do It”. Ujumbe huu husimama kama ukumbusho kwa mteja kuwa anatakiwa aendelee kufanya anachokifanya bila kujali ugumu anaopitia.

Ujumbe huu huongeza mauzo ya bidhaa za Nike kwa sababu ni ujumbe ambao umesimama kwa ajili ya kuhamasisha watu kutokata tamaa kwenye vitu ambavyo wanavifanya.

Hisia ndani ya bidhaa ni kitu cha msingi sana kwenye biashara ya bidhaa yoyote ile duniani. Jana Yanga wamezindua jezi , jezi ambayo ina hisia ambayo inaweza kuisaidia Yanga katika maeneo mawili.

Jezi ya Yanga ina ramani ya Afrika. Ramani ambayo kwa Yanga ina maanisha kuwa ni moja ya timu ambayo imeshiriki katika ukombozi wa Tanzania kutoka kwa wakoloni na Afrika kwa ujumla.

Yanga ni sehemu ya ukombozi wa Afrika. Ukombozi wa Afrika kutoka kwa wakoloni ulitafutwa na watu wengi ikiwemo Yanga. Yanga inatoa ujumbe kwa wa Afrika kuwa hii ni timu ya wananchi,  timu ya Waafrika.

Waafrika wanatakiwa kuwa sehemu ya Yanga kwa sababu ilishiriki katika upatikanaji wa uhuru wao. Ujumbe huu ukisukumwa kwa kiasi kikubwa  utasaidia Yanga kupata mashabiki wapya Afrika na kuuza jezi zao.

Hiki ndicho kitu cha kwanza ambacho Yanga watanufaika kutokana na hii jezi. Kitu cha pili ambacho Yanga watanufaika kutokana na hii jezi ni hali ya upiganaji ndani na nje ya uwanja.

Wachezaji wa Yanga watakapokuwa wanavaa hizi jezi kitu pekee ambacho kitakuwa kinawakumbusha kuwa hii ni timu ya wapiganaji, wapiganaji walioshiriki kupata uhuru kwenye nchi mbalimbali za Afrika.

Kwa hiyo na wao wanatakiwa kupigana vya kutosha uwanjani. Mashabiki nao watakuwa wanaimba jukwaani kwa kuwakumbusha kuwa wapo kwenye timu ya wapiganaji.

Timu ya wananchi,  Timu ya Afrika. Hivyo nje ya uwanja mashabiki watapigana kuwaunga mkono wachezaji wao kwa ajili ya kupata uhuru wa matokeo ndani ya uwanja.

Report

Written by Martin

Martin Kiyumbi ni mchambuzi wa habari za michezo na mbunifu wa maudhui.

Martin Kiyumbi amewahi kufanya kazi za uchambuzi kwenye vituo mbalimbali vya habari kama Tanzaniasports (tovuti ya habari za michezo ), Jembe FM , Radio Free Africa na TVE.
Martin Kiyumbi anapatikana kwenye e-mail ya [email protected]

What do you think?

71 Points
Upvote Downvote

Comments

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Loading…

0
Gareth Bale

Hawa ndiyo ‘maadui’ wa Gareth Bale Real Madrid

Tanzania Sports

Liverpool, Leeds United, magoli saba!