HATIMAYE bingwa wa soka barani Ulaya ngazi ya klabu amepatikana, Paris Saint Germain. Katika fainali hiyo ya kukata na shoka iliyochezwa kwenye dimba la Allianz Arena ilishuhudiwa na maelfu ya mashabiki huku ikishangaza pia namna mchezo wenyewe uligeuka kuwa wa upande mmoja.
Katika fainali hiyo iliyoshuhudiwa na TANZANIASPORTS na kubaini mambo kadhaa ambayo yalitokea na kuleta somo kubwa kwa makocha, wachezaji na mashabiki wa kandanda duniani. Makala haya yanaelezea masuala makuu muhimu yanayotoa somo katika ulimwengu wa michezo.
Rekodi ya kibabe
Fainali ya Ligi ya Mabingwa msimu huu imekuja na rekodi ya aina yake baada ya Inter Milan kukubali kipigo cha mabao 5-0. Katika historia ya Ligi ya Mabingwa hasa mchezo wa fainali, timu iliyofungwa mabao mengi ni Barcelona ambayo ilikubali kipigo cha 4-0 kutoka kwa klabu ya AC Milan mwaka 1994. Fainali ya mwaka huu imevunja rekodi ya Barcelona, ambapo Inter Milan wameingia kenye vitabu vya historia kwa kuchapwa mgoli matano kwa nunge.
Kuyumba Inter Milan
Ukitazama jinsi Inter Milan walivyocheza dhidi ya Barcelona katika hatua ya nusu fainali ungeweza kuhisi mchezo huo ndiyo ulikuwa fainali ya Ligi ya Mabingwa. Ukianza mechi ya kwanza nchini Hispania na pili nchini Italia ilikuwa tamu, kasi, ufundi na maarifa ya hali ya juu. timu zilisakata kandanda la kiwango cha juu kuliko ilivyotarajiwa. Lakini jambo la ajabu kwenye mchezo wa fainali Inter Milan ilipotezwa mapema kuanzia kipindi cha kwanza ambapo ilikubali kipigo cha mabao 2-0 ndani ya dakika 45. Kipindi pili Inter Milan walikubali kuwa wanyonge kwa kuchapwa mabao matatu na hivyo kuweka rekodi ya kipigo kikali cha mabao 5-0 katika mchezo wa fainali.
Inter Milan walikuwa wazito dimbani, na mipango ya mbinu za mchezo hazikuwa rafiki kwa upande wao. Mipango ya kutaka kushambulia haikuwa na matokeo mazuri. Safu ya kiungo mshambuliaji iligeuzwa nyanya na safu ya ushambuliaji ulikuwa dhaifu mno. Washambuliaji wawili wa Inter Milan Lautaro Martinez na Marcus Thuram wote wanacheza aina moja ambayo inafaa katika mfumo wa 4-4-2. Lakini uwezo wao wa kuliandama lango la PSG ulikuwa hafifu kwa sababu hawakuwa na kasi na eneo lao la kiungo lilivunjika vibaya mno.

Inter Milan walicheza mifumo mitatu katika mchezo huo, ambapo awali walianza na 5-3-2 ambapo nafasi mbili za mbele na kwenye kujilinda. Walipoanza kukabia juu walikuwa wanatumia 4-3-3. Kipindi cha pili ndicho kilikuwa balaa zaidi kwani mifumo yao ilianza kupoteza mwelekeo. Wakati PSG wakiliandama lango la Inter Milan walikuwa wameanzisha mfumo mwingine 5-5. Wachezaji watano walikuwa eneo la mstari wa katikati kurudi nyuma kwenye eneo lao, kisha wachezaji watano walikuwa mbele ya mstari wa katikati ya dimba kuelekea langoni mwa PSG. Changamoto ya mfumo huu wa 5-5 walisababisha eneo la kiungo kukosekana mtu wa kulinda, hivyo mipira ya kasi ya PSG ilipoelekezwa pembeni kushoto na kulia ikawawia vigumu kuzuia. Hapo Inter Milan waliyumba kwa kiasi kikubwa.
PSG na umri
Kama kuna kitu kimewasaidia PSG kuchukua ubingwa huu ni mabadiliko ya mfumo wa Ligi ya Mbaingwa Ulaya, lakini suala la umri mdogo wa wachezaji wao nalo lina mchango mkubwa sana. kama ungekuwa mfumo wa zamani, PSG wangetumwa nje ya mashindano. Umri wa wachezaji wa PSG wengi wao ni kuanzia miaka 27 kushuka chini. Lakini wachezaji wengi wa Inter Milan ni wale wenye umri juu ya miaka 30 ambao walishindwa kuendanja na kasi ya vijana. Mfano Desire Doue ana umri wa miaka 19, ikiwa na maana ni chipukizi ambaye alitakiwa kupambana na beki Acerbi mwenye umri wa miaka 38. Kwa mfano wakati bao la pili linafungwa unaona Acerbi alizidiwa kasi na hivyo hakuweza kuendana na uchezaji wa PSG.
Vita mpya ya wababe Ulaya
Desire Doue ni kama ametangaza vita vya ushindani katika soka barani Ulaya dhidi ya kinda mwenzake wa Barcelona Lamine Yamal. Doue amefunga mabao mawili katika mchezo wa fainali na kutengeneza bao la kwanza lililofungwa na beki wa kulia Achraf Hakimi. Kinda huyo mfaransa na mwenye asili ya Ivory Coast ameingia kwenye vita vya kuwania ufalme wa soka barani Ulaya, huku akionekana kuwa mpinzani halisi wa Lamine Yamal. Wachambuzi wa soka wanasema vita mpya itakuwa kwenye kuwania tuzo za uchezaji bora Ulaya na duniani kwani makinda hao wote wana vipaji vya hali ya juu.
Comments
Loading…