Si mara moja au mbili kusikia habari mbaya kuhusiana na waamuzi wetu wa Ligi Kuu Tanzania. Malalamiko kutoka kwa mashabiki, viongozi na wadau wa soka dhidi ya waamuzi ni suala ambalo linatakiwa kutupiwa macho na wenye mamlaka kuhusiana na uendeshaji wa Ligi Kuu. Shirikisho la Soka nchini TFF, pamoja na Bodi ya Ligi Kuu na Chama cha Waamuzi ni mamlaka halali na kisheria kuhusiana na uendeshaji wa soka letu. Mamlaka hizo zinashirikiana kwa madhumuni ya kukuza, kuendeleza, kusimamia sheria pamoja na kubuni njia za kuhakikisha Ligi Kuu Tanzania inakuwa maarufu na bora duniani. TANZANIASPORTS inafahamu malalamiko ya wadau wa soka katika suala la waamuzi limekuwa sugu na ambalo linajirudia rudia katika mchi mbalimbali kuelekea mwisho wa msimu. Mamlaka halali za kuendesha Ligi na kusimamia waamuzi zinawajibika kusikiliza malalamiko ya wadau kuhusi viwango vya marefa wanaochezesha Ligi Kuu.
Pengine suala la malalamiko dhidi ya waamuzi wa soka si la Tanzania pekee. Kwenye mashindano ya Ligi ya Mabingwa Afrika na Kombe la Shirikisho Afrika yapo malalamiko pia. Mifano ya malalamiko hayo ni mingi na video zinazoonesha jinsi waamuzi wanavyotenda isivyo haki. Ligi mbalimbali duniani zimekuwa na malalamiko ya waamuzi lakini wakati Tanzania hali imekuwa mbaya na mashabiki wamekuwa wakielekeza lawama kwa shirikisho la soka na bodi ya Ligi.
Hata hivyo ni muhimu kuhoji nafasi ya chama cha waamuzi katika kuandaa na kuibua waamuzi wenye viwango pamoja na kuimarisha wale waliopo. Chama cha waamuzi ni sawa na kampuni ya waamuzi wa Soka nchini England, PMGOL ambacho ni chombo muhimu katika kukuza, kulea na kuendeleza waamuzi. Kwenye Ligi Kuu Tanzania malalamiko yanaelekezwa kwenye timu mbalimbali ambazo zinaamini kuwa waamuzi wanafanya upendeleo. Baadhi ya timu zinazonufaishwa na uamuzi huo hazifanyi juhudi zozote kukiri kuwa suala la waamuzi wa soka linatakiwa kufanyiwa kazi.
Je malalamiko dhidi ya waamuzi yapo maeneo gani?
Mosi, utoaji wa penati. Adhabu nyingi za penati zinatajwa kutokuwa sahihi ama mwamuzi anakuwa amekosea ama kushindwa kutafsiri sheria ya adhabu hiyo pale mchezaji anapomhadaa mwamuzi kutendewa madhambi kwenye eneo la hatari. Zipo mechi kadhaa ambazo zimelalamikiwa na timu pinzani, viongozi na mashabiki wa pande zote ambao wanasema waamuzi wamekuwa wakitoa adhabu za penati katika mazingira ya kutatanisha. Aidha, kwenye suala hilo hilo pia waamuzi wamekuwa wakizinyima baadhi ya timu adhabu za penati kwa sababu ambazo hazielezeki. Marudio ya video nyingi zinaonesha namna waamuzi wanavyofanya makosa na hivyo kusababisha lawama nyingi kuelekezwa kwao.
Nini kifanyike kukomesha hali hii?
Real Madrid ni klabu inayofahamika kukusanya video zenye makosa ya waamuzi dhidi yao na kuziweka hadharani. Video hizo zinaonesha namna waamuzi wanavyofanya makosa kutafsiri sheria 17 za soka. Kwa mfano mwamuzi anaweza kupuuza adhabu ya faulo na kusababisha timu inayonufaika kupata goli kutokana na maamuzi mabovu. Hali hiyo haiwezi kubadilishwa lakini ukweli ni kwamba makosa yanakuwa yameshafanyika. Klabu ay Aston Villa nayo imewasilisha malalamiko hivi karibuni dhidi ya mwamuzi mmoja wa Ligi Kuu England ambaye alisababisha timu hiyo ifungwe katika mazingira ya kutatanisha. Hii ina maana suala la maamuzi mabovu ya waamuzi yamekuwa katika ligi mbalimbali lakini tofauti iliyopo ni namna uongozi unavyochukua hatua. Kwa mfano waamuzi wa Ligi Kuu wanapoboronga moja kwa moja wanatakiwa kuadhibiwa kwa kupelekwa Ligi daraja la kwanza au la pili kama njia ya kumwadhibu na kumwimarisha ili aweze kukua katika kutafsiri sheria za soka. Waamuzi kadhaa wa EPL huwa wanapelekwa kuchezesha ligi daraja kwa kwanza kama adhabu, kwani wanakuwa kama wameshushwa daraja la hadhi ya urefa. Katika hali hiyo mamlaka ya soka inayohusika nchini Tanzania pamoja na wasimamizi wa waamuzi wanatakiwa kuangalia njia mbadala za kukuza kiwango cha marefu wetu ili kuipa ubora zaidi Ligi Kuu Tanzania.
Ubovu huwanyima fursa
Peter Komba na Ahmed Aragija ni waamuzi wanaosifika katika nchi mbalimbali na wanachezesha mechi kwa kiwango kikubwa. Waamuzi hao wamekuwa wakipata fursa ya kuchezesha mechi za timu ya taifa ama klabu hatua mbalimbali. Lakini ni waamuzi wachache kati ya wengi wanaopata fursa hiyo. Aragija na Komba ni wanajitahidi kuwakilisha vyema bendera ya Tanzania katika uamuzi. Lakini idadi kubwa ya waamuzi wa soka nchini na Ligi Kuu wamekuwa hawapati fursa sababu hawachezeshi kwa kiwango kinachotarajiwa na wadau wa soka. Uchezeshaji na tathmini za marefa wenzao zinaonesha bayana wana viwango vya chini na hivyo kukosa fursa za kuchezesha mechi za Kimataifa. Kwenye mashindnao ya CHAN waamuzi wanatoka nje ya Tanzania, na Ligi Kuu haiwakilishwi na waamuzi wetu kwani hawawezi kupata fursa hiyo. Mashindano ya AFCON katika orodha yao hakuna waamuzi kutoka Tanzania wanaopangiwa kuchezesha. Ni sababu hii inaonesha kukosa kuchezesha mashindano ya Kimataifa husababisha kukosekana kwa fursa ya kujifunza kutoka kwenye mechi za Kimataifa. Kwa kutumia ushahidi huu wasimamizi wa waamuzi na soka wanapaswa kuchukua hatua kuangalia namna bora ya kuinua viwango vya waamuzi wetu kwa maslahi ya Ligi Kuu na nchi.
Comments
Loading…