in

Huyu ndiye nahodha anayewafaa Yanga..

Dar young africans

Jumamosi wiki hii saa 10 jioni kwa saa za Tanzania wakongwe wa soka nchini klabi ya Yanga watakuwa dimba la Kaitaba mjini Bukoba mkoani Kagera. Kikosi cha Jangwani kitaingia kwenye mechi hiyo kikiwa kinashikilia nafasi ya 6 katika msimamo wa Ligi Kuu kwa kujikusanyia pointi 4.

Yanga watakuwa kwenye dimba hilo kwa shughuli moja tu; kumenyana na timu ngumu ya Kagera Sukar inayonolewa na kocha kijana Mecky Mexime. Huo utakuwa mchezo wao wa tatu tangu kuanza Ligi Kuu Tanzania Bara msimu huu 2020-2021.

Hadi sasa Yanga wamecheza mechi mbili nyumbani katika dimba la Mkapa dhidi ya Tanzania Prisons na Mbeya City zote za jijini Mbeya. Mchezo wa kwanza Yanga walitoka sare 1-1 na Tanzania Prisons, kisha wakaibuka na ushindi wa bao 1-0 dhidi ya Mbeya City.

Katika mechi zote mbili Yanga wameingia wakiwa na manahodha wawili tofauti. Mchezo wa kwanza Yanga waliongozwa na nahodha Deus Kaseke. Katika mchezo wa pili Yanga walioongozwa na mnyarwanda, Haruna Niyonzima.

Wakati mchezo dhidi ya Mbeya City ukiendelea kocha wa timu hiyo alimpumzisha kiungo wake Niyonzima kipindi pili na nafasi yake ikachukuliwa na Calinhos na kitambaa cha unahodha kilikwenda kwa beki wa kati Lamine Moro.

Hivyo basi hadi hapo wachezaji wawili wa kigeni wamepata kuongoza Yanga katika mechi mbili, huku mzawa akiwa amefungua dimba. Swali kubwa lililobaki akilini mwa mashabiki wao sasa ni nani anafaa kuwa nahodha wa Yanga?  

Kwa mujibu wa Meneja wa Yanga, Hafidh Saleh ambaye amezungumza na chombo kimoja cha habari nchini Tanzania amebainisha kuwa nafasi ya nahodha wa Yanga bado haikabidhiwa kwa mchezaji yeyote. Meneja Saleh anasema cheo hicho hadi sasa hakijaamuliwa nani akabidhiwe rasmi na kocha Zlatko Krmpotic anahitaji muda ili kuteua kiongozi wa wachezaji. Hii ina maana katika mchezo dhidi ya Kagera Sugar mashabiki wa Yanga wajiandae kushuhudia nahodha mwingine ama wale waliokabidhiwa awali kuongoza jahazi la mechi mbili zilizopita.

NAHODHA ANAKUWA NA SIFA GANI?

Nahodha wa timu anatakiwa kuwa nna nguvu ya ushawishi miongoni mwa wachezaji. Nadhoha anatakiwa kuwa mchezaji ambaye amekuwa chachu ya utulivu,ustahimilivu na kiongozi thabiti ambaye anaweza kukemea,kuelekeza,kuwasimamia,kuwaongoza wachezaji, kudhibiti presha, kuzungumza na waamuzi, uwezo wa kuwasiliana na benchi la ufundi.

Itoshe kusema nahodha anatakiwa kuwa alama ya timu kokote anakokuwepo pamoja na kuhakikisha  wachezaji wanatii na kufuatilia taratibu zinazowekwa. Nahodha anapaswa kuwa kiunganishi cha wachezaji na viongozi, msemaji wa wachezaji na mhamasishaji kila wakati. Kuwamudu wachezaji wote wa timu pinzani na wa kwake.

NI LUGHA IPI ISHINDE YANGA?

Miongoni mwa sifa za kuteua nahodha katika klabu za Ligi Kuu England ni uwezo wa kuzungumza lugha ya Kiingereza. Nahodha anakuwa kiungo ambaye anapokea maagizo kutoka kwa waamuzi wanaowasiliana na mchezaji ambaye hazungumzi lugha ya Kiingereza. Kwa mfano nahodha wa Arsenal, Piere Aubameyang anazungumza lugha za Kiingereza na kifaransa, kwhaiyo atawasiliana na wachezaji wa pande zote mbili.

Yanga wanao wachezaji kutoka Burkina Fasso (lugha ya Kifaransa),Ivory Coast (lugha ya Kifaransa), Angola (lugha ya Kireno) na Tanzania (lugha za Kiswahili na Kiingereza). Mgawanyo wa lugha hizo unaweza kuwaweka katika makundi yao manahodha watatu waliohudumu katika mechi mbili za Ligi Kuu; Haruna Niyonzima, Lamine Moro na Deus Kaseke.

Kwa upande wa lugha Lamine Moro na Haruna Niyonzima wanazungumza nyingi kuliko Deus Kaseke. Kwahiyo lugha za Kiingereza, Kiswahili na Kifaransa zinaweza kuchukua nafasi Yanga ambapo mchezaji mmoja akateuliwa kuwa nohodha.

NANI AMEKAA MUDA MREFU?

Real Madrid kuna kuna utaratibu wa wachezaji waliokaa muda mrefu kupewa unahodha. Kanbla ya Cristiano Ronaldo hajaondoka Real Madrid alikuwa nahodha wa tatu, baada ya Sergio Ramos na Marcelo, huku nafasi ya nne ikienda kwa Rafael Varane.

Baada ya Ronaldo kuondoka, nafasi yake ilichukuliwa na Karim Benzema, ambaye amedumu klabuni hapo misimu 10. Hivyo basi kiongozi mkuu Sergio Ramos anao wasaidizi watatu; Marcelo, Karim Benzema na Rafael Varane.

Yanga inao wachezaji wenye uzoefu na wamekaa muda mrefu. Deus Kaseke anaingia katika kundi hili, naye anaweza kupita njia hii kupewa unahodha. Haruna Niyonzima anao uzoefu katika majukumu ya unahodha kuanzia timu ya taifa ya kwao, Amavubi (Rwanda). Je, ni mchezaji gani amekaa muda mrefu Yanga? Hiki nacho kinatakiwa kuwa kigezo cha kumpa unahodha yeyote.

YUPI NAHODHA ANAYEWAFAA YANGA?

Mashabiki mbalimbali kwenye mitandao wanapendekeza majina ya Lamine Moro, Haruna Niyonzima, Abdalah Shaibu Ninja, Deusi Kaseke, Feisal Salum. Pengine katika mchezo wa tatu dhidi ya Kagera Sugar huenda benchi la ufundi la Yanga likaja na nahodha mwingine wa mchezo huo. Je kati ya majina tajw ahapo juu ni nani anafaa kuwa nahodha wa Yanga?

FEISAL SALUM: Hata hivyo Feisal Salum bado haonekani kuwa na ubavu wa kuwapanga wachezaji wenzake au kupewa jukumu la kuwaelekeza litakuwa kubwa kwake. Pia ana hasira na umri mdogo. Hata hivyo anapaswa kuandaliwa sasa kushika nafasi hiyo kwani itamjenga na kumfanya kuwa bora, na zaidi ni alama ya taifa na Yanga. Kuwa nahodha nambari tatu ni jambo muhimu kwake na klabu kwa ujumla wake.

DEUS KASEKE; winga huyu anaonekana hana namba ya kudumu kikosini Yanga. Ingawa amepangwa kikosi cha kwanza katika mechi zote mbili za Ligi Kuu inaonekana anaweza kupoteza nafasi yake kwa Tuisila Kisinda au Ditram Nchimbi. Hivyo hoja inaibuka ni kwanini Yanga wamteue nahodha ambaye hana uhakika wa kupangwa kikosi cha kwanza? Anaweza kuwa nahodha namba nne.

LAMINE MORO; Anatajwa kuwa nauhakika wa namba ya kudumu, ni mchezaji anayekupa pumzi zote katika dakika 90 za mchezo, anajituma na kuhamasisha wachezaji na mashabiki, anashambulia na kukaba. Tatizo anakosa utulivu na mkorofi. Mara kadhaa amelimwa kadi nyekundu kutokana na kukosa utulivu pamoja na matumizi makubwa ya nguvu katika soka la kisasi linalohitaji maarifa. Anafaa kuwa nahodha nambari moja au mbili.

NIYONZIMA; Ni mchezaji mzoefu kwenye klabu ya Yanga. Ni mzoefu kwenye majukumu ya unahodha. Anakupata vitu vingi uwanjani, anaituliza timu, anaweza kuelekeza, kukemea na kutoa maarifa ya ziada. Katika siku za karibuni amekuwa kama kocha mchezjai dimbani. Anaelekea, anafundisha, na kuonesha uwezo. Tatizo anakuwa amepunguza majukumu ya kiuchezaji. Anafaa kuwa nahodha nambari moja au mbili.

MWAMNYETO; ni beki mgeni aliyejiunga na klabu msimu huu 2020/2021. Anacheza soka la shoka. Ana nguvu, uhakika wa namba kikosi cha kwanza, mtulivu. Anafaa kuwa nahodha namba mbili au tatu.

Report

Written by Mark Mpangala

*Markus Mpangala ni Mhariri, Mwandishi wa Makala Maalumu, Mwanahabari,Mwanablogu,Mwanafasihi na Mwanasafu, ambapo kwa kipindi cha miaka 12 amefanya kazi katika vyombo vya habari mbalimbali vikubwa na vidogo nchini Tanzania katika Michezo, Siasa, Elimu na utalii. Pia ni mchambuzi mchangiaji wa masuala ya siasa na utawala bora katika idhaa ya Kiswahili ya Shirika la Utangazaji la Uingereza (BBC SWAHILI). Ni mhariri na mhamasishaji wa usomaji wa vitabu*

What do you think?

72 Points
Upvote Downvote

Comments

Leave a Reply

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Loading…

0
Aubameyang

AUBAMEYANG alivyokataa kuwa VAN PERSIE

Ligi Kuu Tanzania

Uchambuzi mzunguko wa tatu VPL