in , ,

Hayatou: Woga na udikteta

 

*Mbinu zake zimemwengua Anouma kugombea

*Wadau waunganishe nguvu ili kutengua kanuni

*Hayatou: Kwa nini asipingwe?

*Ni woga wake uliomng’oa mpinzani wake

*Tusipokuwa makini udikteta huu unakuja kwenye vyama vyetu

 

Wakati dunia ikibadilika na sekta ya michezo ikikua, Afrika imebaki kwenye giza, baada ya kuendekeza mgombea wa urais wa shirikisho lake asipingwe.

Issa Hayatou aliyeongoza Shirikisho la Soka Afrika (CAF) tangu 1987 ndiye anasimama Jumapili hii kutetea kiti chake.

Ingekuwa hakuna wagombea wengine waliojitokeza, Hayatou angekuwa na haki ya kuendelea, lakini tatizo ni kwamba wapo, na mbaya zaidi Hayatou, raia wa Cameroon mwenyewe amewaengua.

Rais huyo anayeonekana sasa kuwa kama wa maisha, alitumia nguvu nyingi na ushawishi wa wajumbe kutoka nchi mbalimbali kujihakikishia ulaji.

Raia wa Ivory Coast, Jacques Anouma alikuwa ameomba kugombea urais wa CAF, lakini kikao cha shirikisho hilo kilichotiwa shinikizo na Hayatou nchini Ushelisheli kilimwengua kwa kanuni zake tata.

FBL-AFR-CAF-ELECTION-PRESIDENT

Kuondolewa kwake ni kama kashfa, ambapo Shirikisho la Soka Ivory Coast lilimpitisha kupeperusha bendera yake, lakini kanuni mpya ya CAF inasema ni wajumbe wenye nguvu ya kupiga kura tu wanaweza kugombea urais wa CAF.

Viongozi wengi wenye maono na busara, akiwamo Rais wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Leodeger Tenga walipinga kwa nguvu kanuni hiyo, lakini kampeni za Hayatou zilishatia sumu wajumbe kutoka kanda nyingi za Afrika, wakapitisha kanuni hiyo.

Hapakuwa na busara ya kujibania watu wachache uwezo wa kugombea nafasi hiyo kubwa na muhimu kwa maendeleo ya soka Afrika na duniani, kwa vile wapo wengi wenye uwezo walio nje ya wateule hao wapiga kura wa CAF.

Anouma ni mmoja wa wawakilishi wa Kamati ya Utendaji ya Shirikisho la Soka Duniani (FIFA), ambapo kwa wadhifa huo anaingia Kamati ya Utendaji ya CAF, lakini hana haki ya kupiga kura.

Eti kigezo hicho tu kinamnyima sifa ya kuwania urais wa CAF kiasi cha kufanya Hayatou mwenyewe agombee. Je, Hayatou anaingia tena kwenye uongozi Jumapili hii akiwa na mapya gani?

Kwa umri wake wa miaka 66 na kulewa madaraka miaka yote hiyo 25, atabaki kuongoza kwa mazoea, wakati soka yetu inahitaji kiongozi chipukizi mwenye mawazo mapya na anayeendana na sayansi na teknolojia.

Walau ile kubadilisha mtu pale kwenye kiti kunaweza kusaidia kuleta mambo mapya kwa mwelekeo mpya wa nahodha chomboni.

Kumzuia Anouma (60) au wengine wenye sifa kama yeye kuwania urais wa CAF ni mambo yaliyopitwa na wakati.

Huo ni uamuzi usioheshimu soka ya Afrika, na hivyo wadau wanatakiwa wasikate tamaa, waendelee kukusanya nguvu hata Hayatou akisharudi madarakani, ili kutengua kanuni hiyo siku zijazo.

Chama cha Soka cha Liberia kilifanya vyema kupinga kanuni hiyo kwa kwenda Mahakama ya Usuluhishi wa Michezo (CAS).

Nyota bado ilimwangukia Hayatou hata hapo, kwa sababu mahakama iliwataka Liberia kwenda kumaliza kwanza ngazi zote za rufaa ndani ya CAF kabla ya wenyewe kufikia kutoa uamuzi.

CAS hatimaye ilihitimisha kwamba Anouma anatakiwa kufuata kanuni za CAF na kwamba kanuni hizo zinamnyima sifa ya kugombea, isipokuwa hadi pale zitakapobadilishwa.

Bahati mbaya ni kwamba tarehe ya uchaguzi imefika, ni Jumapili hii Machi 10, na wajumbe wameshafika Marrakech, Morocco kwa kile kinachochukuliwa kama ni kupitisha tu jina, labda itokee maajabu walikatae.

Haiingii akilini jinsi mjumbe wa FIFA anavyokosa sifa za kuongoza soka barani Afrika, na kwamba hiyo ni kashfa kubwa mno, na lazima hatua zichukuliwe kutengua kanuni hiyo.

Mbinu kama hizi zimeididimiza soka ya Afrika kwenye nchi nyingi, na ni aibu kwamba zinaendelea kupanda hadi ngazi ya juu kabisa ya uongozi wa soka.

1214

Ni bahati mbaya kwamba hata kwetu TFF sumu hiyo imeingia, hivyo kwamba mtu mmoja tu anafikia kupitishwa kwa ajili ya kugombea urais, wakati wapo wengi wenye uwezo wa kufanya kazi hiyo.

Tujaribu kuepuka fitna hizi za michezo za kuenguana, kwa sababu ni kuua vipaji na kuzima ndoto za kuibuka fikra za mageuzi ya kisoka kwa maendeleo.

Kwa nini wanawaogopa wagombea watarajiwa wenye nguvu kiasi hicho, wakati umahiri wao unahitajiwa na wadau katika kuikuza soka Tanzania, Afrika na duniani?

Nashindwa kuelewa kwa nini Hayatou, na wengine wenye mawazo kama yake, wasiwapokee wenye uwezo mzuri na wafanye kazi pamoja, ikiwezekana wawapishe madarakani.

Kama ajenda zao ni nzuri, wapiga kura watawachagua, kama si nzuri watawakataa, lakini haikubaliki kuwaengua kwa kanuni kwenye kikao cha watu wachache tu.

Ile tabia ya baadhi ya viongozi wa Afrika kukatalia madarakani hadi wafie humo, sasa inaingia kwenye shirikisho ongozi la soka barani, kwa kuwakata miguu mapema watu wenye uwezo na kipaji ili wasifikie kiti cha uongozi.

Ifike mahali CAF na baadhi ya mashirikisho ya soka Afrika yaache kuongozwa na watu ambao huwa hawaulizwi wala kuwajibika kwa lolote, zaidi ya kufurahia mishahara au posho na safari nyingi kutoka FIFA.

 

 

 

Enhanced by Zemanta

Report

Written by Israel Saria

For the last 20 years I have been working as a football pundit. This experience has provided me with a very useful insight into football and the opportunity to carry out extensive research into the game including its players, the stadiums, the rules and tactics and I have also been grateful to meet a wide range of people connected to football in the UK, Tanzania, Germany .....

What do you think?

71 Points
Upvote Downvote

Comments

Leave a Reply

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Loading…

0

Man City nusu fainali FA

Liverpool watupia Tatu kuwaua Spurs