Wakuu wa Chelsea wanafanya mazungumzo na kocha wao wa zamani, Guus
Hiddink ili azibe walau kwa muda pengo lililoachwa baada ya kumfukuza
Jose Mourinho.
Hiddink (69), kocha wa zamani wa Uholanzi alikuwa pia kocha wa muda
Stamford Bridge 2009 ambapo alifanikiwa kuwaongoza kutwaa Kombe la FA
na kwa sasa hana kazi. Ijumaa hii alikuwa katika moja ya hoteli za
Jiji la London akijadiliana na viongozi wa Chelsea.
Chelsea ambao ni mabingwa watetezi, walianza kusema wanapigania nafasi
walau ya nne, kisha wakasema walau ya sita, lakini sasa kibao
kimegeuka na usemi ni mpango wa kuepuka kushuka daraja.
Makocha kadhaa, wakiwamo Sam Alleryce, Slaven Bilic na Tony Pulis
walieleza kushitushwa kwao kwa Mourinho kufukuzwa kazi, Alledyce
akisema inaonesha kwamba hakuna aliye na uhakika wa kazi iwapo
hawashindi mechi, Bilic akasema Ligi Kuu imepoteza mtu muhimu na Pulis
akaeleza kwamba siku zote inasikitisha mtu akipoteza kibarua chake.
Mourinho ameondoka miezi saba tu baada ya kuwapatia Chelsea ubingwa,
ambapo huu umekuwa msimu wake mbaya zaidi, na alieleza kuhisi kuwapo
usaliti miongoni mwa wachezaji aliowafundisha na kuwapandisha kiwango
kufika juu mno kiasi cha wao kushindwa kukifanya endelevu.
Hiddink amefanikiwa kuwaongoza PSV Eindhovein kutwaa ubingwa wa
Uholanzi mara sita pamoja na ubingwa wa Ulaya na pia amepata
kufundisha Korea Kusini, Australia na Urusi kabla ya kuingia Chelsea.
Aliichukua timu baada ya kufukuzwa kwa Luiz Felipe Scolari na tangu
alipoondoka Stamford Bridge hajapata mafanikio makubwa Uturuki, Anzhi
Makhachkala nchini Urusi wala akiwa na Timu ya Taifa ya Uholanzi
alikojiuzulu Juni mwaka huu baada ya kuonekana kushindwa kuwasaidia
kufuzu kwa Euro 2006.
Nahodha wa Chelsea, John Terry ameeleza kuondoka kwa Mourinho kwamba
kumekuja na kuifanya siku kuwa ya huzuni kubwa, miezi 30 tangu
alipojiunga hapo. Terry alikuwa nahodha wakati Chelsea walipotwaa
ubingwa mara tatu chini ya Mreno huyo.
Kocha mwingine aliyekuwa akitarajiwa kuchukuliwa na Chelsea, Carlo
Ancelotti aliyefukuzwa na Real Madrid mwishoni mwa msimu uliopita,
amesema kwamba Chelsea hawajawasiliana naye. Ndiye aliwaongoza Chelsea
kati ya 2009 na 2011 na kuwapa ubingwa wa England na Kombe la FA.
Chelsea walikuwa wakitafuta kocha wa 11 katika kipindi cha miaka 12 na
kumekuwapo taarifa kwamba wakati Hiddink anaweza kuchukua hatamu hadi
mwishoni mwa msimu, Ancelotti anaweza kwenda Bayern Munich ambako
kocha Pep Guardiola anadhaniwa atafungasha virago kuhamia timu
nyingine.
Wiki iliyopita Ancelotti (56) alisema kwamba amekuwa akijifunza
Kijerumani, akieleza kwamba lugha hiyo ni ngumu sana lakini ikiwa
Mtaliano Giovanni Trapattoni alimudu akiwa na Bayern Munich miaka ya
’90 haoni kwa nini yeye ashindwe lugha hiyo.
Ancelotti amekuwa mapumzikoni huku akijinoa katika maeneo tofauti,
baadaya miaka mitatu yenye mafanikio makubwa, akiwapa Real ubingwa wa
10 (La Decima) wa Ulaya mwaka 2014.
Taarifa nyingine zinasema kwamba Chelsea watalazimika kumlipa fidia Dk
Eva Carneiro aliyekorofishwa na kudhihakiwa na Mourinho wakati
akitekeleza majukumu yake uwanjani, kisha akaamua kuacha kazi.
Chelsea, ambao pengine walichanganyikiwa na hali ya timu yao walio
katika nafasi ya 16, pointi moja kutoka eneo la kushuka daraja,
hawakuwasilisha katika Mahakama ya Kazi ya London majibu ya hoja za
Carneiro hadi muda wa mwisho ambao ulikuwa Alhamisi hii na pia
hawakuomba kuongezewa muda.