in , , ,

FIFA: Nani kuwa rais?

Shirikisho la Soka la Kimataifa (FIFA) linatafuta uongozi mpya, baada ya rais wake, Sepp Blatter kutangaza kwamba ataachia ngazi, lakini pia akiwa amesimamishwa kwa siku 90 huku akichunguzwa kwa ufisadi.

Mchakato wa kupata mrithi wake umeanza, ambapo upokeaji wa majina ya wagombea umeshafungwa na miongoni mwa watu saba waliojitokeza atachaguliwa mmoja Februari 26 mwakani. Kwa sasa, Rais wa Shirikisho la Soka la Afrika (CAF), Issa Hayatou anakaimu urais huo.

Ni akina nani hao wanaowania nafasi hiyo kubwa zaidi katika ulimwengu wa soka? Fuatana nami kuwajua.

 

Gianni Infantino

Infantino ana uraia wa Italia na Uswisi, akiwa na umri wa miaka 45 na kazi yake ni katibu mkuu wa Shirikisho la Soka la Ulaya (UEFA), nafasi aliyoshika tangu 2009.  Alijiunga UEFA akiwa mwanasheria na katibu mkuu wa Kituo cha Kimataifa cha Mafunzo ya Michezo (CIES) katika Chuo Kikuu cha Neuchâtel.

“Ilani yangu itakuwa kwenye msingi wa mahitaji ya mageuzi na kuona kwamba FIFA inahudumia kwa dhati maslahi ya mataifa wanachama 209, bila kujali udogo au ukubwa wao, hivyo ajenda ya soka na ya maendeleo ya soka ndiyo kipaumbele,” anasema.

Advertisement
Advertisement

 

 

Tokyo Sexwale

 

Raia huyu wa Afrika Kusini ana umri wa miaka 62, amepata kuwa mfungwa wa kisiasa kwa miaka 13 katika kisiwa cha Robben kutokana na harakati zake za kupinga ubaguzi wa rangi. Ameshakuwa waziri wa serikali, mjumbe wa kamati maalumu ya FIFA ya kupambana na ubaguzi, ambapo amekuwa kwenye masuala ya soka kwa miaka saba. Kwa sasa ni tajiri mkubwa, baada ya kujikita kwenye biashara ya madini.

“Ilikuwa furaha kubwa kuona FIFA wakiwa nasi hapa (fainali za Kombe la Dunia 2010 nchini Afrika Kusini) lakini pia kuuona ulimwengu wa soka ukijikusanya Afrika Kusini; ile tofauti ya rangi, upinde wa mvua wa wanadamu na kupeleka ujumbe kote duniani kwamba FIFA ina nguvu ya kuunganisha wote,” anasema.

 

 

Prince Ali bin al-Hussein

Mwana mfalme wa Jordan ana umri wa miaka 39 lakini amekuwa kwenye ‘gemu’ kwa miaka 16. Kwa sasa ni rais wa Chama cha Soka cha Jordan, mwasisi na rais wa Shirikisho la Soka la Asia Magharibi. Amepata kuwa makamu wa rais wa FIFA.

Ana haya ya kusema: “Ulimwengu wa soka unahitaji kuongozwa na chombo chenye hadhi kubwa – shirikisho la kimataifa ambalo litakuwa kiutumishi zaidi na mfano wa kuigwa wa maadili, lenye uwazi na utawala bora.”

 

Musa Bility

 

Bility ana umri wa miaka 48, akitoka Liberia ambako ni rais wa Chama cha Soka cha huko na amekuwa katika masuala ya soka kwa miaka mitano. Huyu ni mfanyabiashara mkubwa, akimiliki Srimex Oil Enterprise, kampuni kubwa zaidi ya kuingiza mafuta nchini Liberia.

“Sote tunakubaliana kwamba soka inakabiliwa na wakati mgumu lakini pia ni katika nyakati ngumu viongozi mahiri huibuka,” anasema.

 

Michel Platini

 

Rais wa UEFA tangu 2007 anayetoka Ufaransa akiwa na umri wa miaka 60, na amekuwa katika soka kwa miaka43 na pia ni makamu wa rais wa FIFA. Kwa sasa amesimamishwa kwa siku 90 kujihusisha na masuala ya soka, akichunguzwa sambamba na Blatter kwa tuhuma za kupeana mlungula.

Alikuwa mwanasoka mahiri katika klabu za Nancy, Saint-Etienne na Juventus. Ni huyu alikuwa nahodha wa Timu ya Taifa ya Ufaransa waliotwaa ubingwa wa Ulaya 1984. Alikuwa kocha wa timu hiyo kati ya 1988 na 1992. Kuanzia hapo hadi 1998, alikuwa rais mwenza wa Kamati ya Maandalizi ya Fainali za Kombe la Dunia na kisha makamu wa rais wa Shirikisho la Soka la Ufaransa. Tangu 2002, Platini amekuwa mjumbe wa kamati ya utendaji ya FIFA.

“Nategemea uungwaji mkono kutoka kwenu sambamba na mapenzi yetu ya pamoja kwa soka, ili kwa pamoja tuwape makumi ya mamilioni ya washabiki wa soka na FIFA kile wanachotaka: FIFA ya kupigiwa mfano, yenye umoja na inayoonesha mshikamano, FIFA inayoheshimiwa na kupendwa na watu,” anasema.

 

 

Jerome Champagne

 

Mfaransa huyu mwenye umri wa miaka 57 amekuwa kwenye soka kwa miaka 17 na kazi yake sasa ni mshauri katika masuala ya soka ya kimataifa. Amepata kuwa mwanadiplomasia, alifanya kazi FIFA kwa miaka 11 akiwa mtendaji na mshauri wa Rais Blatter kabla ya kuondoka 2010.

“Tunashuhudia mwezi huu wa kampeni za uchaguzi zikitawaliwa na utata kwenye dili zilizofanyika kwa siri, tunapohitaji, kuliko wakati mwingine wowote, mjadala wa wazi juu ya hatima yake,” anasema.

 

 

Sheikh Salman bin Ebrahim al-Khalifa

 

Ustaadhi huyu anayetoka Bahrain ana umri wa miaka 49 na uzoefu wake kwenye soka ni wa miaka 17. Huyu ndiye rais wa Shirikisho la Soka la Asia na makamu mwenyekiti mwenza wa FIFA. Amepata pia kuwa mkuu wa FA ya Bahrain.

“Sitafuti kuwa rais mtendaji. Nadhani tunatakiwa kuleta watu sahihi FIFA, tunatakiwa kuwapa kazi hizo wanataaluma,” ndiyo maoni yake.

Report

Written by Israel Saria

For the last 20 years I have been working as a football pundit. This experience has provided me with a very useful insight into football and the opportunity to carry out extensive research into the game including its players, the stadiums, the rules and tactics and I have also been grateful to meet a wide range of people connected to football in the UK, Tanzania, Germany .....

What do you think?

71 Points
Upvote Downvote
Tanzania Sports

Man United nao wakatwa

Tanzania Sports

Chelsea mbendembende