in , , ,

EPL 2017/18 Pazia kushushwa Ijumaa

ARSENAL

Arsenal walimaliza chini ya nafasi ya nne kwa mara ya kwanza msimu uliopita tangu alipochukua mikoba Arsene Wenger msimu wa 1996/97. Hawatakuwemo kwenye Ligi ya Mabingwa Ulaya msimu huu. Pengine hili ni moja kati ya mambo yanayoweza kuwapa nguvu Washika Bunduki hawa kwenye mbio za kuwania taji la Ligi Kuu ya England. Mpaka sasa Arsenal wameshasajili wachezaji wawili ambao ni mshambuliaji Alexandre Lacazette aliyetokea Olympic Lyon ya Ufaransa na mlinzi mahiri wa kushoto Sead Kolasinac kutoka Schalke 04 ya Ujerumani. Wana timu nzuri hasa kwenye eneo la ushambuliaji lakini upo uwezekano mkubwa wa nyota wao muhimu zaidi, Alexis Sanchez kutimka. Ikiwa Sanchez ataondoka makali ya kikosi cha Arsene Wenger yatakuwa yamepungua mno na huenda wakashindwa kurejea kwenye nafasi nne za juu msimu huu.

BOURNEMOUTH

AFC Bournemouth walifunga mabao mengi zaidi ya Manchester United msimu uliopita wa EPL. Mshambuliaji wao Joshua King alifunga 16 kati ya magoli 55 ya Bournemouth. Walimaliza kwenye nafasi ya 9 wakiwa wamepanda kwa nafasi 7 kutoka msimu wa 2015/16. Wameimarisha kikosi kwa kuwaongeza mlinzi Nathan Ake na golikipa Asmir Begovic kutoka Chelsea pamoja na mshambuliaji mahiri na mzoefu Jermaine Defoe aliyetokea Sunderland walioshuka daraja. Defoe alifunga mabao 15 kwnenye msimu uliopita wa EPL. Uwepo wa Joshua King na nyongeza ya Jermaine Defoe unakifanya kikosi cha Eddie Howe kubaki na makali yake kwenye safu ya ushambuliaji. Hata hivyo wana udhaifu mkubwa kwenye ulinzi na kama watabaki hivi licha ya usajili wa Ake mambo hayatawaendea sawa msimu huu.

BRIGHTON AND HOVE ALBION

Kiasi cha pesa, vilabu vya EPL VILIVYOTUMIA mpaka sasa

Brighton wanaingia kwenye msimu wao wa kwanza wa EPL kwenye historia yao. Walipanda daraja baada ya kumaliza kwenye nafasi ya pili kwenye Ligi Daraja la Pili ya England (English Championship) nyuma ya Newcastle waliokuwa mabingwa. Mchezaji nyota zaidi wa kikosi hiki ni winga Mfaransa Anthony Knockaert ambaye alifunga mabao 15 na kutengeneza mengine 9 kwenye Ligi Daraja la Pili ya England msimu uliopita na kufanikiwa kutwaa tuzo ya mchezaji bora wa michuano hiyo. Wanae pia mshambuliaji Glenn Murray aliyekuwa mfungaji bora wa timu yao msimu uliopita kwa kufunga mabao 23 kwenye English Championship. Wameongeza nguvu kwenye kikosi kwa kusajili wachezaji kadhaa. Wa muhimu zaidi mi kiungo Davy Popper aliyejiunga kutoka PSV. Kibarua cha msingi cha mwalimu Chris Hughton ni kuhakikisha anaibakisha timu kwenye EPL.

BURNLEY

Burnley walimakamata nafasi ya 16 kwenye Ligi Kuu ya England msimu uliopita ambapo kuna tofauti ya nafasi mbili pekee kutoka kwenye ukanda wa kushuka daraja. Kuutumia vizuri uwanja wa nyumbani ndicho kilichowaepusha na kushuka daraja. Alama 33 kati ya 40 walizovuna kwenye msimu mzima walizipata ndani ya dimba lao la Turf Moor. Mara mbili za mwisho walizokuwemo kwenye EPL, 2009/10 na 2014/15 hawakuweza kuepuka kushuka daraja. Lakini safari hii wamefanikiwa kubakia baada ya kupanda daraja msimu uliopita. Nyota wao muhimu zaidi ni mlinda mlango Tom Heaton aliyekuwa kinara wa kuokoa mashuti msimu uliopita akiokoa michomo 143 msimu mzima. Aliwanusuru mno Bournemouth ambao safu yao ya ulinzi haikuwa kwenye ubora. Msimu huu wanahitaji kuimarika kwenye safu ya ulinzi ili waweze kubaki kwenye Ligi Kuu ya England.

CHELSEA

Mabingwa hawa watetezi walipanda kwa nafasi tisa msimu uliopita baada ya kumaliza kwenye nafasi ya 10 msimu wa 2015/16. Diego Costa aliyewafungia mabao mengi zaidi kwenye Ligi Kuu ya England huenda akaondoka kikosini kabla ya dirisha la usajili kufungwa kwa kile kinachotajwa kuwa Antonio Conte hana mpango nae. Chelsea wamewaongeza kikosini wachezaji wanne mbaka sasa ambao ni mshambuliaji Alvaro Morata aliyetokea Real Madrid, kiungo Tiemoue Bakayoko aliyetokea Monaco, Antonio Rudiger kutoka Roma na golikipa Willy Caballero aliyetokea Manchester City. Morata alifanya vizuri akiwa na Madrid msimu uliopita lakini kiwango duni alichoonesha kwenye michezo ya kirafiki kimeanza kuleta mashaka. Mshambuliaji Michy Batshuayi ameonesha makali ya kutosha kwenye michezo ya kirafiki. Hata hivyo uamuzi wa kumuacha Diego Costa pengine utawagharimu Chelsea msimu huu.

CRYSTAL PALACE

Crystal Palace wamemleta meneja Frank De Boer ndani ya EPL ambapo ni mara ya kwanza Mholanzi huyo anakuja kwenye soka la England. Mchezaji huyu wa zamani wa FC Barcelona amewahi kufundisha katika klabu za Ajax na Inter Milan. Amewahi kushinda taji la Ligi Kuu ya Uholanzi mara nne akiwa kocha wa timu hiyo. Ingawa ni mgeni kwenye soka la England, hapana shaka uzoefu alio nao kwenye soka unatosha kabisa kuwapaisha Crystal Palace kutoka kwenye nafasi ya 14 na kwenda kwenye 10 bora msimu huu. Kwenye kikosi cha Crystal Palace mbaka sasa wamesajiliwa wachezaji wawili ambao ni Ruben Loftus-Cheek aliyetua kwa mkopo akitokea Chelsea na Hairo Riedewald aliyetokea Ajax kwa ada ya paundi miloni 8. Uwepo wa Wilfried Zaha na Christian Benteke waliofanya vizuri msimu uliopita unamuogezea De Boer nafasi ya kufanikiwa na kikosi cha Crystal Palace.

EVERTON

Ni wazi kuwa kikosi cha Ronald Koeman ni kati ya timu ambazo zinaweza kusemwa kuwa zitakuwa kwenye vita ya kuwania nafasi nne za juu msimu huu. Msimu uliopita walimaliza kwenye nafasi ya 7 ambapo walipanda kwa nafasi 4 kutoka kwenye nafasi waliyokamata msimu wa 2015/16 kabla ya ujio wa Koeman. Mfungaji wao mahiri Romelu Lukaku ametimkia Manchester United kwa ada ya paundi milioni 75 huku mshambuliaji nyota Wayne Rooney akipishana nae na kurejea Goodison Park. Ni kweli kuondoka kwa Romelu Lukaku ni pigo kwa Everton. Lakini ikumbukwe timu hii imefanya usajili mzuri mno ikiwashusha wachezaji kadhaa wenye uwezo akiwemo kiungo mshambuliaji Davy Klaassen aliyetokea Ajax na Sandro Ramirez, mchezaji wa zamani wa Barcelona aliyejiunga kutoka Malaga ya Hispania.

HUDDERSFIELD

Huddersfield Town watacheza kwenye Ligi Kuu ya England kwa mara ya kwanza msimu huu. Kwa vyovyote vile lengo kuu la klabu hii kwa msimu huu ni kujaribu kujiepusha na kushuka daraja. Walimaliza kwenye nafasi ya tano kwenye English Champioship msimu uliopita na kupata nafasi ya kufuzu kupitia mtoano wa kugombea nafasi ya kupanda daraja ambapo waliwafunga Reading kwa penati mwezi Mei. Wapo chini ya meneja David Wagner mwenye uzoefu kidogo mno wa kufundisha soka. Huddersfield Town ni timu ya kwanza ya wakubwa kufundishwa na nyota huyo wa zamani wa timu ya taifa ya Marekani baada ya kuwahi kuifundisha kikosi cha vijana cha Borussia Dortmund miaka kadhaa ya nyuma. Huddersfield wameongeza nyota zaidi ya kumi kwenye kikosi. Hili itawapa changamoto kwa kuwa watakuwa na kikosi chenye wachezaji ambao hawajazoeana vizuri.

LEICESTER CITY

Msimu uliopita Leicester walimtimua aliyekuwa meneja wao Claudio Ranieri baada ya mfululizo wa matokeo mabaya uliowaweka kwenye ukanda wa kushuka daraja. Walimleta meneja Craig Shakespeare aliyewatoa kwenye hatari baada ya kushinda michezo mitano mfululizo. Walimaliza ligi kwenye nafasi ya 12 ambapo walishuka kwa nafasi 11 kutoka kwenye msimu wa 2015/16 ambamo waliutwaa ubingwa wao wa kwanza wa EPL chini ya meneja Claudio Ranieri. Nyota wapya waliosajiliwa ni watatu pekee mbaka sasa. Hao ni mlinzi Harry Maguire kutoka Hull City aliyetua kwa dau la paundi milioni 17, kiungo Vincente Iborra aliyetokea Sevilla kwa dau la paundi milioni 12.5 na golikipa Eldin Jakupovic. Bado wana nyota wao mahiri Riyad Mahrez na Jamie Vardy. Shakespeare ana nafasi nzuri ya kuendeleza ubora wake msimu huu na kuiingiza timu kwenye nafasi za juu zaidi.

LIVERPOOL

Liverpool hawana lengo lingine isipokuwa kupigania taji la Ligi Kuu ya England msimu huu. Msimu uliopita walimaliza kwenye nafasi ya nne na hivyo watarejea kwenye Ligi ya Mabingwa msimu huu. Wana kiwango kizuri mno kwenye safu ya ushambuliaji inayoundwa na Sadio Mane, Philippe Coutinho, Roberto Firmino na Mohammed Salah waliomuongeza msimu huu kutoka Roma ya Italia. Wamesajili pia nyota wengine wawili ambao ni Andrew Robertson kutoka Hull City na Dominic Solanke kutoka Chelsea. Kwenye eneo la kingo na beki pia wana wachezaji wanaotosha kuwawezesha kushindania taji la EPL msimu huu huku bado wakiwawania mlinzi Virgil Van Dijk wa Southampton na kiungo Naby Keita wa RB Leipzig ya Ujerumani. Hata hivyo Liverpool watapunguzwa makali kwa kiasi kikubwa iwapo nyota wa mkubwa zaidi Coutinho anayetajwa kuwaniwa na Barcelona ataihama klabu hiyo.

MANCHESTER CITY

Pep Guardiola anaingia kwenye msimu wake wa pili akiwa meneja wa Manchester City. Msimu uliopita licha ya kutumia fedha nyingi zaidi ya klabu zote za England Pep hakufanikiwa kuwapa taji la EPL matajiri hao wa Etihad ambapo alimaliza kwenye nafasi ya tatu nyuma ya Chelsea na Tottenham. Kiuhalisia walimaliza chini ya malengo kikizingatiwa kikosi walichokuwa nacho, fedha walizotumia na hadhi yao ya miaka ya karibuni. Wameimarisha kikosi chao zaidi msimu huu kwa matumizi ya pesa kama kawaida wakiwaongeza walinzi wa pembeni Kyle Walker kutoka Tottenham na Benjamin Mendy kutoka Monaco na kiungo Bernado Silva kutoka Benfica pamoja na nyota wengine kadhaa. Usajili wa Walker na Mendy ndio usajili muhimu zaidi wa kikosi chao kwa kuwa walikuwa na udhaifu mkubwa mno kwenye nafasi za walinzi wa pembeni.

MANCHESTER UNITED

Manchester United wanaingia kwenye msimu wao wa tano tangu msimu waliotwaa taji la EPL kwa mara ya mwisho. Ni moja kati ya timu ambazo lengo lake kuu msimu huu ni kutwaa taji la EPL. Walionesha uwezo mkubwa mno kwenye ulinzi msimu uliopita ambapo waliruhusu maba 29 pekee ambayo ni machache kuliko timu nyingine yoyote ya EPL ukiwatoa Tottenham waliokuwa vinara kwenye kipengele hicho. Hata hivyo udhaifu mkubwa zaidi kwenye kikosi cha Jose Mourinho ulikuwa kwenye ushambuliaji ambapo walishindwa kutengeneza nafasi za kutosha za kufunga mabao. Walifunga mabao 54 pekee ambayo ni machache kwa bao moja dhidi ya mabao yaliyofungwa na Bournemouth. Ubutu wao huo ulikuwa sababu kuu ya kuwafanya washindwe kumaliza kwenye nafasi nne za juu kinyume na malengo yao. Nyongeza ya Romelu Lukaku kikosini itawainua kwa kiasi kikubwa iwapo wataweza kutengeneza nafasi za kutosha.

NEWCASTLE UNITED

Silaha kuu waliyo nayo Newcastle United msimu huu ni Rafael Benitez. Huyu ni mwalimu mwenye uzoefu mkubwa akiwahi kuzifundisha kwa mafanikio klabu kubwa kadhaa zikiwemo Valencia, Liverpool na Inter Milan. Amewarejesha Newcastle kwenye Ligi Kuu ya England baada ya kutwaa taji la English Championship. Wana timu yenye uwezo mkubwa wa kushambulia. Walikuwa vinara wa mabao kwenye English Championship wakifunga mabao 86 ambapo mshambuliaji wao Dwigt Gayle alifunga 23 kati ya hayo. Ni Chris Wood wa Leeds United pekee aliyemzidi Dwight kwenye orodha ya wafungaji. Ingawa si rahisi Dwight kufunga idadi hiyo ya mabao kwenye EPL lakini uwezo wake unatosha kuwawezesha Newcastle kutimiza malengo yao kwenye EPL ya msimu huu. Usajili wa winga mahiri raia wa Ghana, Christian Atsu unawaongezea makali zaidi Newcastle United.

SOUTHAMPTON

Southampton walikamata nafasi ya nane kwenye EPL msimu uliopita wakiwa wamepanda kwa nafasi moja kutoka kwenye nafasi ya tisa waliyokamata msimu wa 2015/16. Wanaingia kwenye msimu wakiwa na mwalimu mpya Mauricio Pellegrino aliyeiongoza Alaves ya Hispania kutinga fainali ya Kombe la Mfalme msimu uliopita ambapo walipoteza kwa Barcelona. Ni meneja anayetajwa kuwa na uwezo mkubwa wa kuhamasisha kikosi. Bila shaka Pellegrino ni nyongeza ya maana kwa Southampton. Udhaifu mkubwa uliooneshwa na Soutampton msimu uliopita ni kwenye ushambuliaji. Idadi ya mabao 41, waliyofunga inazidi idadi ya mabao ya timu nne za mkiani pekee. Mshambuliaji wao tegemeo Nathan Redmond aliishia na magoli saba msimu mzima na akawa kinara wa mabao kwenye timu yake. Mbaka sasa hawajasajili mshambuliaji yeyote. Ikiwa wataamua kubaki na washambuliaji wale wale ni vigumu kufikia malengo yao ya msimu.

STOKE CITY

Sifa ya Stoke City kama moja ya timu zenye ulinzi imara ilipotea msimu uliopita. Waliruhusu mabao 56 ambayo ni mengi kuliko msimu wowote katika mismu yao nane ya nyuma kwenye Ligi Kuu ya England. Pengine hili limeshapata suluhisho kwa kuwa wamemleta kwa mkopo mlinzi hodari kijana Kurt Zouma kutoka Chelsea. Pigo kubwa walilopata mbaka sasa Stoke City kwenye dirisha la usajili ni kumpoteza mshambuliaji wao Marko Arnautovic aliyetimkia West Ham kwa ada ya paundi milioni 25. Kuondoka kwake kunaweza kuwagharimu Stoke. Hata hivyo kikosi kimesheheni washambuliaji mahiri kama Peter Crouch na Said Berahino. Ikiwa mbinu za mwalimu mzoefu Mark Hughes zitawawesha kutengeneza nafasi za kutosha washambuliaji hawa wanao uwezo wa kupachika mabao ya kutosha.

SWANSEA

Swansea walitumia karibu nusu ya msimu uliopita wakiwa kwenye ukanda wa kushuka daraja. Ni mwalimu Paul Clement aliyewanusuru na kushuka daraja baada ya kuteuliwa kuchukua nafasi ya Bob Bradley aliyetimuliwa kutokana na mfululizo wa matokeo mabaya. Clement aliiongoza Swansea kushinda michezo 9 kati ya 18 akiwa na Swansea tangu alipoteuliwa Januari. Kikosi kilichopo kimesheheni nyota kadhaa wa kutumainiwa akiwemo mshambuliaji Fernando Llorente aliyewafungia mabao 15 kwenye msimu uliopita wa EPL ambayo ni zaidi ya asilimia 30 za mabao yote ya Swansea. Tatizo kubwa alilo na Clement ni uwezekano wa kumpoteza nyota wake muhimu Gylfi Sigurdsson anayewaniwa na klabu kadhaa ikiwemo Evertom. Ari waliyo nayo baada ya mfululizo wa matokeo mazuri chini ya Clement inaweza kuwapa mafanikio msimu huu.

TOTTENHAM HOTSPUR

Tottenham walimaliza katika nafasi ya pili kwenye msimu uliopita wa Ligi Kuu ya England. Walikuwa bora zaidi kwenye ulinzi wakiruhusu mabao 26 pekee ambayo ni machche kuliko timu nyingine yoyote. Walikuwa vinara pia kwenye idadi ya mabao ya kufunga ambapo waliweka wavuni jumla ya mabao 86. Wana kikosi kilichosheni vipaji vya hali ya juu akiwemo Harry Kane aliyenyakuwa kiatu cha dhahabu akifunga mabao 29 kwenye EPL. Hakuna udhaifu wowote wa wazi wa kimchezo unaoweza kuonekana kwenye kikosi hiki cha Maurico Pochettino. Ni wazi kuwa msimu huu watakuwa miongoni mwa timu zenye nafasi ya kutwaa ubingwa ikiwa watafanikiwa kuwabakiza nyota wao muhimu kikosini. Mbaka sasa Spurs hawajafanya usajili wowote licha ya kumuuza mlinzi wao mahiri wa kulia Kyle Walker.

WATFORD

Watford ndiyo timu iliyoshika mkia kati ya timu 17 zilizofanikiwa kusalia kwenye EPL. Ni alama 6 pekee zilizowatenganisha na ukanda wa kushuka daraja msimu uliopita. Wamo pia kwenye orodha ya timu tano zilizofunga mabao machache zaidi na pia kwenye orodha ya timu tano zilizoruhusu mabao mengi zaidi msimu uliopita. Kiuhalisia sehemu kubwa ya kikosi cha Watford ilikuwa na kiwango kidogo mno msimu uliopita. Ni timu inayohitaji kufanya manunuzi ya uhakika ili kujiweka mbali na uwezekano wa kushuka daraja msimu huu. Tayari wamefanya usajili wa wachezaji wanne ambao ni Tom Cleverley kutoka Everton, Kiko Femenia kutoka Alaves Will Hughes kutoka Derby na Nathaniel Chalobah kutoka Chelsea. Meneja wao mpya Marco Silva ni mgeni na Ligi Kuu ya England lakini aliiongoza Olympiacos ya Ugiriki kutwaa taji la ligi kuu msimu wa 2015/16 hivyo anatosha kutumainiwa.

WEST BROMWICH

West Bromwich ni kati ya timu za daraja la kati zinazoingia kwenye msimu huu zikiwa na hamasa pamoja na malengo ya kupanda juu iwezekananyo. Msimu uliopita walikamata nafasi ya 10 ambayo ni ya juu zaidi kwa timu hiyo kwa misimu minne ya nyuma. Wachezaji hawakuonesha uwezo binafsi wa kiwango kikubwa kwenye mashindano lakini kilichowapa mafanikio ni utulivu wa mwalimu Tony Pulis. Mbinu zake na kuepuka kubadilsha vikosi mara kwa mara ni moja kati ya vitu vilivyokuwa vikimpatia matokeo mazuri. Hata hivyo wachezaji wanatakiwa kuonesha uwezo binafsi na kutengeneza nafasi zaidi za kufunga mabao kwa kuwa walionesha udhaifu fulani msimu uliopita. Ingawa walimaliza kwenye nafasi ya 10 walizidiwa kwa idadi ya mabao hata na Swansea waliokuwa chini yao kwa nafasi tano. Usajili wa mshambuliaji Jay Rodriguez kutoka Southampton pengine utawainua vijana wa Tony Pulis.

WEST HAM

West Ham walishindwa kuingia kwenye nafasi 10 za juu msimu uliopita ambapo waliporomoka kwa nafasi nne kutoka kwenye nafasi yao ya msimu wa 2015/16. Malengo ya mwalimu Slaven Bilic bila shaka yatakuwa ni kukirejesha kikosi chake walau kwenye mbio za kushindania nafasi za kushiriki moja kati ya mashindano ya Ulaya. Ameongeza majina makubwa kwenye kikosi wakiwemo mlinzi wa zamani wa Manchester City Pablo Zabaleta aliyejiunga kwa uhamisho huru, mlinda mlango Joe Hart aliyetokea Manchester City na washambuliaji Javier Hernandez kutoka Bayer Leverkusen na Marko Arnautovic kutoka Stoke City. Pengine uzoefu wa wachezaji hawa waliowahi kutwaa mataji makubwa utaongeza hamasa kwenye kikosi cha West Ham.

Report

Written by Kassim

What do you think?

71 Points
Upvote Downvote
Tanzania Sports

Arsenal Vs Chelsea: Ngao ya Hisani..

Tanzania Sports

NI UWEZO WA ZIDANE AU BAHATI ?