Mambo yamebadilika tena, ambapo mshambuliaji wa Chelsea, Diego Costa amefungiwa mechi tatu huku beki wa kati wa Arsenal, Gabriel Paulista akifutiwa adhabu ya kukosa idadi hiyo ya mechi.
Costa ameadhibiwa baada ya Chama cha Soka (FA) kumshitaki kwa utovu mkubwa wa nidhamu kwenye mechi dhidi ya Arsenal Jumamosi, ambapo alimpiga usoni beki wa kati wa The Gunners, Laurent Koscielny mara kadhaa.
FA walichukua hatua hiyo baada ya mwamuzi Mike Dean aliyemtoa nje Paulista kwa kadi nyekundu ya moja kwa moja, hakuona tukio la Costa, hivyo ikabidi FA wachukue mkanda na kuwapa jopo la waamuzi wa zamani wapitie na kila mmoja kutoa uamuzi wake.
Costa ametiwa hatiani kwa mchezo mchafu na kwa kufungiwa kwake, Costa atakosa mechi ya Kombe la Ligi dhidi ya Walsall Jumatano hii na zile za Ligi Kuu dhidi ya Newcastle na Southampton, licha ya kuwa alikana kosa hilo Jumanne hii. Kocha wake, Jose Mourinho naye alikuwa akimuunga mkono, na kumpongeza kwa jinsi anavyocheza.
Kwa upande mwingine, kocha wa Arsenal, Arsene Wenger na Naibu Nahodha wao, Per Mertesacker walitoa maoni yao mapema wakisema kwamba Costa alitakiwa apewe kadi nyekundu na kufungiwa.
Costa alimfanyia rafu Koscielny ambaye hakujibu, na baada ya hapo akamrudia Paulista, ikiwa ni pamoja na kumkaba shingo na kumwachia alama ya mkwaruzo, na katika kujitetea ndipo mwamuzi Dean akampa Paulista kadi nyekundu mwishoni mwa kipindi cha kwanza, kwenye mechi ambayo Arsenal walilala kwa 2-0.
Katika taarifa yao, Chelsea wameeleza kwamba wamesikitishwa sana na uamuzi wa Kamati ya Udhibiti ya FA kumfungia Costa na kwamba wanasubiri taarifa yao ya maandishi juu ya sababu kabla ya wao kujadili na kutoa maoni yao.
Kwa upande mwingine, Arsenal wameshinda rufaa yao dhidi ya kadi nyekundu aliyopewa Paulista, hivyo hatakosa mechi tatu kama ilivyokuwa imetakiwa awali. Mbrazili huyo, hata hivyo, anatakiwa kujibu kosa jingine la kutotoka uwanjani pindi alipooneshwa kadi nyekundu, majibu yanayotakiwa Alhamisi hii.