in , , ,

CHOZI LA MARADONA NI DENI KUBWA KWA MESSI

Ndiye aliyefunga goli la mkono wa Mungu, hakutosheka hapo akaamua kufunga goli la karne. Yote haya yalitokea siku moja, kwenye mechi moja, uwanja mmoja, katika mashindano ya kombe la dunia la mwaka 1986.

Ndipo hapo alizidi kuwekeza hazina kubwa ya kukumbukwa na vizazi vingi kwa sababu ya alama ambazo aliziweka kupitia miguu yake.

Miguu ambayo alijua kuipa thamani kubwa kipindi alipokuwa anakamata mpira, hakuwa na utani. Hakutaka kufanya kosa lolote kipindi ambacho mpira ulikuwa mguuni mwake.

Alijua ufanisi wa kazi yake ndiyo utakaomfanya akumbukwe na vizazi vyote vutakavyopita katika dunia hii.

Leo hii tunamkumbuka na kumwandika Diego Maradona kama mchezaji nyota kuwahi kutokea katika dunia hii ni kwa sababu ya ufanisi wa kazi ya miguu yake.

Aliibeba timu yake ya taifa kipindi ambacho alihitajika kuibeba na ndiyo maana akaipa kombe la dunia. Tangu aipe kombe la dunia Argentina haijawahi kuchukua tena kombe la dunia.

Miguu yake peke yake ndiyo iliwafanya Argentina wanyanyue mikono juu kufurahia ubingwa wa kombe la dunia.

Leo hii ni siku mpya, siku yenye mateso makubwa sana kwake, muda mwingi anautumia kukaa jukwaani. Hana uwezo tena wa kushuka chini na kuingia uwanjani kuibeba Argentina.

Nguvu zake zipo jukwaani ambako anatumia mikono na mdomo wake kuhamasisha vijana walio uwanjani waweze kurejesha furaha yake iliyopotea tangu mwaka 1986.

Hana furaha tena, kama ilivyokuwa kipindi chake ambapo watu wengi wa Argentina walitegemea furaha kutoka katika miguu yake kama ilivyo muda huu watu wa Argentina akiwemo na yeye (Diego Maradona) anavyotegemea furaha kutoka kwenye miguu ya Lionel Messi.

Miguu ambayo mpaka sasa hivi haijafanikiwa kuweza kuipa furaha yoyote Argentina. Miguu ambayo mpaka sasa hivi haijafikiwa kuifanya mikono inyanyue kombe la aina yoyote katika ngazi ya timu ya taifa.

Ndipo hapo chozi la Diego Maradona linapoanza kutiririka. Chozi hili lina maana kubwa sana, ni chozi lenye maumivu makubwa ndani ya moyo wake. Ni chozi lenye uihataji mkubwa wa furaha katika mpira. Ni chozi ambazo linatoka na kilio kikubwa chenye deni kubwa kwa Lionel Messi.

Kipaji kikubwa ambacho kimeshinda kila kitu kasoro kombe lolote na timu ya taifa. Wengi wanakiu ya kumuona Lionel Messi akishinda. Wanatamani kuiona miguu yake ikiibariki Argentina na kombe hata moja.

Kombe la dunia la mwaka 2014 lilikuwa kombe ambalo wengi walitegemea atachukua lakini cha kusikitisha alikutana na timu inayocheza kitimu kuliko Argentina.

Na hapa ndipo mwanzo wa sababu inayomfanya Lionel Messi ashindwe kubeba kombe lolote na timu ya taifa. Hana timu, yeye ndiye kila kitu kwenye timu. Yeye ndiye mpiga pasi, yeye ndiye mpiga pasi za mwisho na yeye ndiye mfungaji.

Hawajafanikiwa kutengeneza timu ambayo ingeunganisha vipaji vyote kwa pamoja. Timu ambayo ingecheza kitimu, lakini wana timu ambayo inamtegemea mtu mmoja.

Mzigo mkubwa umemwelemea Lionel Messi. Ameshindwa kukimbia na huu mzigo kwa kasi kubwa mpaka mwisho wa mbio.

Kinachobaki ni maumivu ndani ya mioyo ya mashabiki wa timu ya taifa ya Argentina. Wanatamani kuona ushindi lakini mtu aliyepewa dhamana ya kuwapa ushindi hana nguvu za kuibeba timu pekee yake.

Umri unazidi kwenda, hatari ya yeye kustaafu kuchrza timu ya taifa bila kombe inazidi kuwa kubwa.

Ndipo hapo uchungu wa kina Diego Maradona unapoonekana kupitia chozi lao linalotiririka shavuni.

Chozi ambalo linadeni kubwa kwa Lionel Messi, deni ambalo anatakiwa kulilipa ili kuweka furaha kubwa kwenye mioyo ya watu wa Argentina, furaha ambayo itaandikwa kwenye vitabu vya alama ambavyo vitamfanya akumbukwe na vizazi vingi. Deni hili anatakiwa aanze kulilipa kwenye mechi dhidi ya Nigeria.

Report

Written by Martin

Martin Kiyumbi ni mchambuzi wa habari za michezo na mbunifu wa maudhui.

Martin Kiyumbi amewahi kufanya kazi za uchambuzi kwenye vituo mbalimbali vya habari kama Tanzaniasports (tovuti ya habari za michezo ), Jembe FM , Radio Free Africa na TVE.
Martin Kiyumbi anapatikana kwenye e-mail ya [email protected]

What do you think?

71 Points
Upvote Downvote
Tanzania Sports

HISPANIA WAMSAHAU JULEN LOPETEQUI NA KUIKUMBUKA BENDERA YAO

Tanzania Sports

LINI MPIRA UTAWATENDEA HAKI KINA MODRIC NA KROOS