in , , ,

HISPANIA WAMSAHAU JULEN LOPETEQUI NA KUIKUMBUKA BENDERA YAO

Vincent Del Bosque aliweka alama kubwa ndani ya kikosi cha Hispania. Kabati lake alilijaza makombe yote makubwa, hapana shaka alitembea na kikosi cha dhahabu.

Hii waweza kuitumia kama ilikuwa moja ya silaha yake kubwa ambayo alikuwa anajivunia nayo. Dunia iliwatazama kina Iniesta, ikavutiwa na pasi za Xavi ikaogopeshwa na aina ya mpira wa Hispania.

Kila nafsi ilikiri Vincent Del Bosque ametengeneza dudu lililokuwa linatisha kwa sura, dudu lililokuwa linaogofya kwa kiasi kikubwa. Heshima ilijengwa kwenye bendera ya Hispania ikawa ni bendera ambayo ilikuwa na uhuru wa kupepea juu zaidi ya bendera zingine.

Hakuna ufalame unaodumu milele, ndiyo maana kombe la dunia la mwaka 2014 lilikuja na dalili za ƴufalme wa Vincent Del Bosque kuelekea mwishoni. Tulianza kuona dalili kizazi chake cha dhahabu kilikuwa kinaelekea mwishoni na kibaya zaidi hakuwa na wazo na kutengeneza kizazi kipya.

Ndiyo maana hata alipoenda na kikosi hicho hicho katika michuano ya Euro ya mwaka 2016 aliishia katika hatua ya kumi na sita bora na ukawa mwisho wa utawala wa Vincent Del Bosque.

Julen Lopetequi likawa jina jipya katika masikio yetu, hata macho yetu yaliona ni taswira ngeni. Hispania ilikuwa imetuletea mtu ambaye ni mgeni kwetu, hakuwa na historia kubwa wakati akiwa mchezajia na hakuwa na mafanikio ya kutisha alipokuwa kocha.

Mafanikio makubwa aliyapata na vikosi vya vya vijana vya Hispania ambapo alichukua kombe la vijana la ulaya.

Hatukumpa nafasi kubwa ya yeye kufanya vizuri akiwa na timu ya taifa ya wakubwa ikizingatia hakuwahi kufanya vizuri na FC Porto pamoja na kupewa bajeti kubwa.

Tuliona mtu ambaye alikuwa anakuja kuanguka tena, lakini ilikuwa tofauti na mategemeo yetu kwa sababu alianza kutengeneza kizazi kipya nje ya kizazi cha Vincent Del Bosque.

Alifanikiwa kuwaweka pamoja vijana wapya ambao alikuwa nao katika kikosi cha vijana vya timu ya Taifa na wachezaji ambao walikuwa na uzoefu ndani ya kikosi cha timu ya taifa.

Mseto huu ulileta kitu kikubwa ndani ya kikosi cha Hispania, akaanza kupata matokeo mazuri akiwa na timu ya taifa. Tangu aichukue Hispania hajawahi kufungwa, mara ya mwisho kwa Hispania kufungwa ilikuwa katika michuano ya Euro katika hatua ya kumi na sita bora.

Mechi ishirini bila kufungwa huku akishinda mechi kumi na sita (16), na kupata sare mechi nne (4) huku akiwa amepata clean sheets kumi na moja (11).

Hii inaonesha timu ilikuwa imeshaanza kukaa vizuri na kuelewana ndani ya mfumo wa Julen Lopetequi pamoja na mbinu zake.

Siku moja kabla ya kombe la dunia Julen Lopetegui anafukuzwa ndani ya timu, timu ambayo alikuwa ameshaanza kuiandaa na alikuwa ametengeneza mahusiano mazuri na wachezaji, anakuja ƙkocha mpya Fernando Hiero.

Kocha ambaye ataanza na mbinu mpya, mfumo mpya na anaanza upya kutengeneza mahusiano na wachezaji wake.

Hii itakuwa moja ya kazi kubwa sana kwa Fernando Hiero na kibaya zaidi anaanza mechi dhidi ya timu imara, mwanzo ambao unaweza  kusababisha Hispania kuwa na mwelekeo mbaya katika michuano hii.

Kipi akifanye Fernando Hiero? Kulitumia vizuri benchi la ufundi lililokuwa linafanya kazi na Julen Lopetequi ili aendelee na mfumo ambao ulikuwa umewekwa awali na Julen Lopetequi.

Asifikirie kuanzisha vitu vingi vipya katika kikosi chake. Na kikubwa zaidi anachotakiwa ni kuwafanya wachezaji wa timu ya taifa ya Hispania wasionekane wapweke kutokana na kuondoka kwa Julen Lopetequi.

Wanatakiwa wajue kuwa wapo Russia kwa ajili ya nchi yao na siyo kwa ajili ya Julen Lopetequi.

Taifa lao ni kubwa zaidi kuliko mtu mmoja, kuna watu wako nyuma yao wakiwaunga mkono.

Report

Written by Martin

Martin Kiyumbi ni mchambuzi wa habari za michezo na mbunifu wa maudhui.

Martin Kiyumbi amewahi kufanya kazi za uchambuzi kwenye vituo mbalimbali vya habari kama Tanzaniasports (tovuti ya habari za michezo ), Jembe FM , Radio Free Africa na TVE.
Martin Kiyumbi anapatikana kwenye e-mail ya [email protected]

What do you think?

71 Points
Upvote Downvote
Tanzania Sports

KISU ‘KILICHOIUA’ MISRI NA MOROCCO ‘KIMEIUA’ TUNISIA

Tanzania Sports

CHOZI LA MARADONA NI DENI KUBWA KWA MESSI