in , , ,

Chelsea wang’aa Europa


*Spurs wavutwa shati, Bale aumia
*Newcastle wakoga ‘vumbi’ ugenini

Robo fainali ya Kombe la Ligi ya Europa imeanza kwa kicheko kwa Rafa Benitez, sintofahamu kwa Andre Villas-Boas na kilio kwa Alan Pardew.
Chelsea walishuka Stamford Bridge kwa nguvu na kuwakandamiza Rubin Kazan kutoka Urusi mabao 3-1.
Wakati hali ikiwa hivyo, Tottenham Hotspurs walilazimika kufanya kazi ya ziada kukomboa mabao mawili waliyokuwa wametangulia kufungwa na FC Basel ya Uswisi.
Pamoja na kukomboa mabao hayo, kocha Villas-Boas aliondoka uwanjani kwa sikitiko, baada ya tegemeo lake katika upachikaji mabao, Gareth Bale kuumia na kutolewa uanjani akibebwa na machela.
Kwa upande wa Newcastle wanaofundishwa na Pardew, wana kazi ya ziada nyumbani, baada ya kupigwa mabao 3-1 na Benfica nchini Ureno.

Katika dimba laStamford Bridge, Chelsea walipata mabao yao kupitia kwa Fernando Torres aliyefunga mawili na Victor Moses.
Hata hivyo, bao la penati la Bebars Natcho litawapa nguvu Rubin Kazan kwenye mechi ya marudiano nyumbani kwao Urusi wiki ijayo.
Kazan walipata penati baada ya nahodha wa Chelsea, John Terry kushika mpira kwa makusudi kwenye eneo la hatari.
Ama katika uwanja wa White Hart Lane jijini London, Spurs licha ya kutoa sare ya 2-2, kubwa waliloondoka nalo ni kuumia kwa tegemeo lao kwenye mashindano yote, Bale aliyeonekana kupata majeraha makubwa.
Mapema mchezoni, nyota mwingine, Aaron Lenon alisalimu amri na kutoka, baada ya kuonekana kuwa na maumivu, na dakika 10 za mwisho, William Gallas naye alitoka nje baada ya kuumia.
Bale alipotoka, Spurs walibaki wachezaji tisa uwanjani, kwani kocha wao alishaingiza uwanjani idadi inayoruhusiwa kwa wale wa akiba. Hata hivyo, haikuchukua muda mrefu, mechi ikamalizwa, licha ya kuwa zilikuwa zimeongezwa dakika tatu.
Basel walionekana makini zaidi uwanjani, japokuwa walipopoteana Spurs walipata mabao hayo mawili kupitia kwa Emmanuel Adebayor dakika ya 40 na Gylfi Sigurssdon dakika ya 58.
Washabiki wa Spurs walikuwa wamelowa kabla ya hapo, kwani Valentin na Fabian Frei walitangulia kuwafungia Basel mabao mazuri dakika ya 30 na ya 35, na nusura wapachike la tatu.
Katika robo fainali nyingine, Fenerbahce waliwafunga Lazio ya Italia mabao 2-0 katika mechi iliyopigwa Uturuki.
Mabao ya wenyeji yalifungwa na Pierre Webo wa Cameroon kwa penati na lile la dakika za mwisho la mchezaji wa zamani wa Liverpool, Dirk Kuyt.
Kiungo Mnigeria, Ogenyi Onazi anayekipiga Lazio alipewa kadi nyekundu kwa mchezo mbaya.
Wiki ijayo itashuhudia timu nne zikijichuja kuingia nusu fainali ya mashindano haya ya Ligi ya Europa.

Report

Written by Israel Saria

For the last 20 years I have been working as a football pundit. This experience has provided me with a very useful insight into football and the opportunity to carry out extensive research into the game including its players, the stadiums, the rules and tactics and I have also been grateful to meet a wide range of people connected to football in the UK, Tanzania, Germany .....

What do you think?

71 Points
Upvote Downvote

Comments

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Loading…

0

Hongera Abdulhalim Humud: Jomo Cosmos isiwe mwisho wa safari..

Arsenal mwendo mdundo