in , , ,

Chelsea wakwea ya tatu

*Newcastle wajiweka pazuri, QPR bado

 

Chelsea wamerejea nafasi ya tatu, japokuwa walilazimika kufanya kazi ya ziada dhidi ya Sunderland ya Paolo Di Canio.
Mtaliano huyo mwenye makeke alianza kwa kupata alichokitaka, kwani timu zilikwenda mapumziko Sunderland wakiwa mbele kwa bao moja, ambalo beki Cesar Azpilicueta alijifunga dakika ya 45.
Wakati Di Canio akiendeleza utaratibu wake wa kawaida wa kutoa ishara nyingi kwa wachezaji na wasaidizi wake kwenye benchi, mchezaji wake, Matt Kilgallon alifanya kosa lile lile la Azpilicueta na kujifunga dakika ya 47.
Chelsea waliokuwa nafasi ya tano, walipambana hadi kupata bao la pili dakika ya 55 kupitia kwa Branislav Ivanovic aliyeugusa shuti la David Luiz.
Kwa mbwembwe za Di Canio aliyechukua nafasi ya Martin O’Neill aliyefukuzwa Sunderland, ni dhahiri kutakuwapo burudani ya pekee uwanjani kwa mechi zilizosalia, akipigana kuwabakisha Black Cats ligi kuu.
Di Canio anakuwa kocha wa tano, wakiwamo wale wa muda, kuanza kibarua ligi kuu kwa safari ya Stamford Bridge, na hakuna kati yao aliyefanikiwa kuambulia hata pointi moja.
Matokeo hayo yanawaacha Sunderland katika nafasi ya 17, wakifungana pointi 31 na Wigan walio nafasi ya 18. Chelsea wamefikisha pointi 58 sawa na Tottenham Hotspurs, lakini Spurs wamecheza mechi moja zaidi.

NEWCASTLE WAPUMUA

20130401-230703.jpg

Newcastle United wamejiweka pazuri kidogo kwenye msimamo wa ligi, baada ya kupata bao dakika za mwisho dhidi ya Fulham.
Nyota wao, Papiss Cisse ndiye alifunga bao pekee la mchezo, na kuwafanya Newcastle wawe na pointi tano juu ya eneo la hatari, kwani wamejikusanyia pointi 36 na wanashika nafasi ya 13.
Cisse alikosa mabao kadhaa kabla ya hilo, ikiwa ni pamoja na kugonga mtambaa wa panya, huku Fulham walio nafasi ya 10 nao wakikosakosa kupitia Dimitar Berbatov.

QPR LA KUVUNDA HALINA UBANI

IMG_0100

Queen Park Rangers walikuwa mchezaji mmoja pungufu kwa dakika 70, wakafanikiwa kupata bao la kuongoza dhidi ya Wigan, lakini waliruhusu kufungwa dakika ya mwisho ya mchezo.
Wachezaji na kocha wao, Harry Redknapp walionesha kukata tamaa, baada ya bao la Shaun Maloney kufuatia mpira wa adhabu ndogo katika dakika ya 94.
Adhabu hiyo ilitolewa baada ya rafu ya kizembe na isiyo na sababu ya Stephane Mbia dhidi ya mshambuliaji wa Wigan. Mbia ndiye aliyezaa bao la QPR, kwa kumpasia mpira Loic Remy dakika ya 85.
Vijana hao wa Loftus Road walio wa pili kutoka mkiani kwa pointi zao 24, walibaki 10 baada ya Boby Zamora kupewa kadi nyekundu dakika ya 20 kutokana na kile mwamuzi alichoona ni rafu mbaya dhidi ya Jordi Gomez.
Wigan sasa wanashika nafasi ya 18, ndani ya eneo la kushuka daraja, na kocha wao, Roberto Martinez anasema wanataka kuonesha kwamba wanatafuta vikombe na si kuwa tu ndani ya ligi hii maarufu kuliko zote duniani.

SPURS BILA BALE WAAMBULIA SARE

Tottenham Hotspurs wakicheza bila tegemeo lao, Gareth Bale aliye majeruhi waliambulia sare ya mabao 2-2 dhidi ya Everton.
Walianza vyema kwa bao dakika ya kwanza kupitia kwa Emmanuel Adebayor, lakini Phil Jagielka aliwasawazishia Everton dakika ya 15 kabla ya Kevin Mirallas kupachika jingine dakika ya 53.
Hata hivyo, Gylfi Sigurdsson alisawazisha dakika ya 87 na kuwahakikishia Spurs kubaki nafasi muhimu ya nne, wakiwa pointi mbili mbele ya Arsenal na pia wakiwa mbele mchezo mmoja.

WEST HAM WAWAKOMALIA LIVERPOOL

IMG_0349

Liverpool wameshindwa kuendeleza wimbi lao la ushindi, baada ya jitihada zao kugonga mwamba kwa West Ham United.
Liverpool wanaofundishwa na Brendan Rodgers walianza mchezo wakikabiliwa na mashambulizi ya haraka langoni mwao kutoka kwa Hammers.
Alikuwa Mohamed Diame aliyekaribia kuwaliza Reds baada ya Carlton Cole kuwashitukiza mabeki na kuwachomoka na mpira, lakini hakuweza kufunga.
Nahodha wa Liverpool, Steven Gerrard nusura atundike mpira nyavuni, lakini shuti lake liliokolewa kwenye mstari wa goli na James Tomkins.

Kwa matokeo hayo, Liverpool wanashika nafasi ya saba wakati West Ham wapo nafasi ya 12.

Report

Written by Israel Saria

For the last 20 years I have been working as a football pundit. This experience has provided me with a very useful insight into football and the opportunity to carry out extensive research into the game including its players, the stadiums, the rules and tactics and I have also been grateful to meet a wide range of people connected to football in the UK, Tanzania, Germany .....

What do you think?

71 Points
Upvote Downvote

Comments

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Loading…

0

Bayern Munich mabingwa Ujerumani

Safi sana Yanga, Kwa hili mnastahili pongezi..