in , , ,

Safi sana Yanga, Kwa hili mnastahili pongezi..

*Kujenga uwanja wa kisasa ni mafanikio makubwa ya klabu…

 

DAR ES SALAAM Young Africans Sports Club, Yanga, Wanajangwani wamepiga hatua kubwa mno ya kimaendeleo na kwa hatua hii tu wanastahili pongezi kubwa. Hatua hiyo kubwa ni kukabidhiwa na kampuni ya ujenzi ya China ya Beijing Construction ramani tatu za viwanja vya soka ili wachague moja wanayoitaka kwa ajili ya kujengewa uwanja hapo makao makuu ya klabu hiyo kwenye mitaa ya Twiga na Jangawani.

Hii ni hatua kubwa kwani si hatua ya kwanza ya utekelezaji unaoanza kwa hatua ya kwanza ya kuwa na wazo. Inafuata ni wazo hilo kuwekwa hadharani kwa kujadiliwa. Kisha uamuzi wa utekelezaji unaoasisi mambo kadhaa ya utekelezaji ikiwemo mkakati wa kuwapata wataalaam wa kufanya tathmini. Kinachofuata ni kuwapata wataalaam hao. Baadaye wataalaam hao kuwezeshwa kufanya kazi yao na kukabidhi taarifa ya tathmini kwa wahusika wa mpango huo, hatua ambayo Yanga wamefikia kwa sasa.

Yanga wamekabidhiwa ramani tatu na kampuni hiyo ya China iliyojenga pia uwanja wetu mkubwa, tunaouita uwanja wa Taifa,ambao kwenye vyombo kadhaa vya habari vya kimataifa unaitwa Benjamin Mkapa Stadium. Sijui jina hilo stahili lilipenyaje kwenye vyombo hivyo, kimojawapo kikiwa kituo maarufu cha runinga cha michezo cha Supersport cha Afrika Kusini.

Ukishafika hatua fulani ya maendeleo kama una dhamira ya dhati ya kwenda mbele ni wazi utasonga mbele na kwa Yanga dhamira ya dhati iko wazi, vinginevyo wasingeingia gharama ya kuwapa Wachina kazi waliyokabidhiwa majuzi.

Yanga wametoa changamoto kubwa kwa mahasimu wao Simba ambao maneno yao kuhusu kuwa na uwanja wao eneo la Bunju, barabara ya Bagamoyo yalikuwa ya kusisismua sana ikiaminika kwamba kufikia sasa kuna kitu kingekuwa kimefanyika. Sasa hivi mazungumzo ni kuhusu timu tu na wachezaji. Hakuna anayezungumzia tena uwanja wa Bunju. Labda ilikuwa ahadi ya kushawishi kura.

Yanga sasa wanapaswa wajipange namna ya kupata fedha za ujenzi wa uwanja zinazoanzia bilioni 48 kwa uwanja wa gharama ndogo hadi bilioni 81 kwa uwanja wa gharama kubwa. Yanga inaweza kukamilisha kazi hiyo bila kuingiza fedha za kifisadi au kupenyezewa fedha za umma na miaka ijayo kukazuka kashfa itakayokuwa mama wa kashfa zote kuwahi kutokea nchini.

Watanzania tuko milioni 45. Watoe milioni 25 (kadirio kubwa) kwamba si watu wa soka kabisa. Kati ya waliobaki gawa nusu kwa nusu Yanga na Simba (ingawa naamini Yanga ina mashabiki wengi kuliko Simba). Utabaki na milioni 10. Kati yao, watoe milioni tano kwamba hawana uwezo (kadirio kubwa). Milioni tano wa Yanga wenye uwezo wakihamasishwa kuchangia 50,000/= kila mmoja kama tunavyohamasishana kwenye michango ya harusi, mchango mmoja tu wa wote unajenga uwanja wa gharama ndogo kati ya ramani tatu. Wakipiga mara mbili yake, unapatikana ule wa gharama kubwa na fedha kubaki!

Kumbuka tangu hesabu ya sensa ya Watanzania 45 ambapo kiuhakika kama sensa ingeendeshwa vizuri tungetangazwa kuwa si chini ya milioni 50,mpaka kufikia Wanayanga wenye uwezo nchi nzima ni hesabu zilizoshushwa chini sana.Ni wazi hilo likiwekwa kwenye utekelezaji hali haitakuwa kama ilivyoelezwa hapa.

Aidha, hapa kimezingatiwa chanzo cha michango tu ya wanayanga. Tukichanganya na vyanzo vingine kama biashara ya jezi, fulana na kofia za Yanga, matangazo ya runinga na kadhalika, ni wazi mzigo kwa Wanayanga wa kuchangia utapungua

Katika hili la michango, ninawashauri viongozi wa Yanga wasiache hata shilingi mia ya Mwanayanga anayehitaji kuchangia ujenzi wa uwanja wa klabu yake, awe mwanachama, shabiki, mnazi au mpenzi. Uandaliwe utaratibu wa kukusanya pesa hizo. Wanayanga milioni tano wakitoa mia mia tu,unapata shilingi milioni 500! Hii ni hela. Ikiwa elfu elfu, bilioni tano. Umekosa nini.

Naamini kabisa viongozi wa Yanga ni watu wa mikakati na hili watalipangilia vizuri zaidi kuliko inavyodhaniwa. Cha msingi na cha kusisitiza sana, wajiepushe na fedha zozote za kihalifu pamoja na fedha ya umma ambayo ni ya wote wakiwemo Simba na wa vilabu vingine pamoja na wasiohusika na soka. Tuwe mbali na pesa hizo kuepuka kashfa.

Ninachowaomba Watanzania wenzangu, Yanga wanafanya jambo kubwa na lenye tija, hivyo tuwape moyo wa kuendelea nalo. Tuachane na kauli za kuwakatisha tamaa kama kuiita mipango yake kuwa danadana kwa sababu tu hawajaainisha vyanzo vya pesa za ujenzi wa uwanja wao. Naamini vyanzo vyao vya mapato wanavijua na watavitumia kukamilisha ujenzi huo.

Safi sana Yanga, kwa hili tuko pamoja sana. Japo mimi ni Simba!

Report

Written by Israel Saria

For the last 20 years I have been working as a football pundit. This experience has provided me with a very useful insight into football and the opportunity to carry out extensive research into the game including its players, the stadiums, the rules and tactics and I have also been grateful to meet a wide range of people connected to football in the UK, Tanzania, Germany .....

What do you think?

71 Points
Upvote Downvote

Comments

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Loading…

0

Chelsea wakwea ya tatu

Man City wababe wa Man United