in , , ,

Chelsea, Man U, Man City ushindi

Ilikuwa Jumamosi ya vipigo kwa wanyonge, ambapo Chelsea, Manchester City na Manchester United walikuwa baadhi ya walioshinda.
Chelsea walirejea kwenye usukani wa ligi baada ya ushindi wa 3-0 walioupata nyumbani Stamford Bridge dhidi ya Stoke City.

Mmisri Mohamed Salah aliwapatia Chelsea bao la kuongoza baada ya kunasa mpira wa kiungo Nemanja Matic dakika ya 32.

Frank Lampard alifunga bao la pili kwa mpira uliotokana na penati yake aliyokosa dhidi ya kipa mahiri Asmir Begovic dakika ya 61.
Willian alishindilia bao la tatu dakika ya 72 na kuwawekea Chelsea rekodi ya kutofungwa mechi 77 nyumbani chini ya Kocha Jose Mourinho, ikijumuishwa msimu huu na ule wa awali aliokuwapo kabla ya kuondoka.

Kadhalika wamezima mfululizo wa Stoke kushinda mara tatu mfululizo, na ni tulizo kwa wapenzi wa Chelsea ambao wametoka kufungwa 3-1 na Paris Saint-Germain kwenye mechi ya robo fainali wiki hii nchini Ufaransa.
Chelsea sasa wanaongoza kwa pointi 72 kutokana na mechi 33.

MAN CITY WAWAPIGA SAINTS 4-1

Katika mechi ya mapema Jumamosi, Manchester City waliwakandika Southampton mabao 4-1. City waliotoka kutulizwa na Arsenal kwa kwenda sare ya 1-1 kwenye mechi iliyopita, walianza mchezo kwa nguvu na Yaya Toure akawapatia bao katika dakika ya tatu tu kwa mkwaju wa penati.

Edin Dzeko alionekana kuzidisha madai kwamba aliumizwa vibaya na Jose Fonte wa Saints hadi mwamuzi Chris Foy akatoa penati hiyo, iliyopigwa kiufundi na mchezaji bora wa mwaka wa Afrika mbele ya washabiki 47,009 waliohudhuria.

Southampton ambao wametokea kuwa wagumu katika baadhi ya mechi za Ligi Kuu England walijaribu kuendana na kasi ya Man City waliokuwa nyumbani kwao Etihad na dakika ya 37 walifanikiwa kusawazisha bao kwa mkwaju wa penatio kama wenzao kupitia kwa Rickie Lambert.

Penati hiyo ilitolewa baada ya beki Pablo Zabaleta kumwangusha chini Jack Corck. Katika dakika moja ya mwisho wa kipindi cha kwanza, Samir Nasri na Dzeko walitikisa nyavu za Southampton na kufanya waende mapumziko wakiwa 3-1.

Stevan Jovetic alipigilia msumari kwenye jeneza la Saint kwa kufunga kwa mpira wa karibu. Mbali na kichapo hicho, Southampton pia walipata pigo kwa mchezaji wao, Jay Rodriguez kuumia na kutolewa nje kwa machela.

City sasa wamefikisha mechi 31, wakiwa na moja mkononi na wana pointi 70, moja pungufu ya Liverpool wanaocheza Jumapili hii dhidi ya West Ham United na wapo pointi mbili pungufu ya Chelsea.

MANCHESTER UNITED WAZINDUKA

Manchester United wamepata ushindi ugenini dhidi ya Newcastle United kwa mabao 4-0.
Man U walionekana kubadilika, ambapo Juan Mata alifungua kitabu cha mabao kwa mpira wa adhabu ndogo kutoka umbali wa yadi 20 uliotumbukia wavuni moja kwa moja dakika ya 39.

Mpira wa chini chini wa Javier Hernandez uligonga mwamba kabla Mata tena hajaugiga na kuujaza kimiani kuandika bao la pili kwa Man U dakika ya 50.

Newcastle walishindwa kabisa kwenda mkono kwa mkono na United, ambapo walikubali bao la tatu lililofungwa na Hernandez kutoka yadi sita kabla ya Adnan Januzaj kufunga kitabu cha mabao kwa kuandika la nne dakika ya 90.

Kwa matokeo hayo Man U wamepanda nafasi moja hadi ya sita baada ya kufikisha pointi 57 lakini itategemea mechi ya Jumatatu kati ya Tottenham Hotspur na Sunderland, kwani Spurs wana pointi 56.

SIKU MBAYA KWA WENYEJI WENGI

Jumamosi inaelekea ilikuwa siku mbaya kwa wenyeji wengi, kwani katika mechi nyingine, Aston Villa walipoteza mchezo nyumbani kwa kufungwa 2-1 na Fulham wakati Cardiff nao walishindwa kuhimili nguvu za Crystal Palace walipokubali kipondo cha mabao 3-0.

Hull hata hivyo walitumia vyema dimba la nyumbani kwa kuwafunga Swansea 1-0 lakini Norwich walinyukwa nyumbani kwao walipocheza na West Bromwich Albion, wakakubali kumaliza mchezo kwa kufungwa 1-0.

Nafasi ya mwisho kwa sasa inashikwa na Sunderland waliocheza mechi 30 na kufikisha pointi 25, ya 19 ni Cardiff wenye pointi 26 kutokana na mechi 33 na wa 18 ni Fulham waliokusanya pointi 27 kutokana na mechi 33.

Report

Written by Israel Saria

For the last 20 years I have been working as a football pundit. This experience has provided me with a very useful insight into football and the opportunity to carry out extensive research into the game including its players, the stadiums, the rules and tactics and I have also been grateful to meet a wide range of people connected to football in the UK, Tanzania, Germany .....

What do you think?

71 Points
Upvote Downvote

Comments

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Loading…

0

Tanzania yatinga Fainali ya Kombe la Dunia kwa Watoto wa Mitaani

Simba, Mbeya City polepole