Hatimaye Chelsea wametwaa ubingwa wa England waliokuwa wakiutarajia baaada ya kuwaacha wenzao kwa mbali.
Bao la Eden Hazard, mchezaji bora aliyechaguliwa na Chama cha Wanasoka wa Kulipwa (PFA) ndilo limewapa Chelsea ushindi.
Hazard alifunga bao baada ya penati yake kuokolewa na golikipa Julian Speroni, kish aakaupata mpira alioutema na kuutia kimiani, na lilikuwa bao pekee la mchezo.
Huu ni ubingwa wa kwanza kwa Chelsea tangu 2010, na wameupata huku wakiwa bado wamebakiza mechi tatu, ikiwa ni furaha kubwa kwa kocha wao, Jose Mourinho.
Haikuwa mechi rahisi kwenye dimba la Stamford Bridge, ambapo Palace walikuwa wameapa kuharibu majaribio ya Chelsea kutangazwa mabingwa mapema.
Wametwaa ubingwa wakiwaacha wanaowafuata, Manchester City, wakiwa pointi 13 nyuma, huku wakifungana kwa mechi, japokuwa Arsenal wanaoshika nafasi ya tatu wamecheza mechi mmbili pungufu ya wawili hao.
Mourinho amesema kwamba anajihisi mwenye furaha, anajivunia hilo lakini pia akasema kwamba amechoka. Huu ni ubingwa wa tatu kwa Mourinho akiwa kocha wa Chelsea katika vipindi viwili tofauti.
Wachezaji, benchi la ufundi na washabiki walifurahia ubingwa baada ya kipenga cha mwisho, ambapo wameunasa ubingwa bila ya mfungaji bora hadi sasa, Diego Costa, anayetarajiwa kuwa nje hadi mwisho wa msimu kwa matatizo yake ya misuli ya paja.
Katika mechi nyingine, Manchester City wakicheza ugenini wamewapiga Tottenham Hotspur 1-0 kwa bao la Sergio Aguero na kuendelea kubaki katika nafasi ya pili.
Chelsea wamekuwa mabingwa baada ya kufikisha pointi 83 kwa michezo 35, Man City wanazo 70 kwa michezo kama hiyo wakati Arsenal wanazo 67 kwa mechi 33.
Man United waliopoteza mechi tatu mfululizo wanashika nafasi ya nne wakiwa pia wamecheza mechi 35, wakifukuzwa na Liverpool wenye pointi 61 kwa mechi hizo hizo. Spurs wanazo 58 wakati Southampton wana moja pungufu.
Mkiani wapo wale wale, Sunderland wakiwa na pointi 33, Queen Park Rangers (QPR) wakiwa nazo 27 na chini kabisa hawajaondoka Burnley wenye 26 na ni ngumu kwao kukiepuka kikombe cha kushuka daraja.