Mikoa ya Arusha, Mara na Kigoma iko kwenye hatihati ya kutoshiriki uchaguzi mkuu wa Chama cha Netiboli Tanzania (CHANETA) utakaofanyika April 20 mkoani Dodoma, kutokana na kushindwa kulipa ada ya uanachama wa chama hicho.
Akizungumza na waandishi wa habari jana, Kaimu Katibu Mkuu wa CHANETA, Rose Mkisi, aliitaja mikoa mingine ambayo iko hatarini kukosa nafasi ya kushiriki uchaguzi mkuu kwa kutolipa ada ni Iringa, Rukwa na Kilimanjaro.
Mkisi alisema kuwa mikoa yote isiyolipa ada hadi kufikia leo mchana haitaruhusiwa kushiriki mkutano huo muhimu wa kuchagua viongozi wapya.
“Wasipolipa ada zao hadi kufikia kesho mchana (leo) hatutakuwa na namna nyingine isipokuwa ni kuendelea na mchakato wetu na wao hawatashiriki kwavile hawatakuwa na sifa,” alisema Mkisi.
Aliitaja mikoa ambayo imekamilisha sharti la kulipa ada kuwa ni pamoja na Kagera, Mbeya, Pwani, Manyara na Dodoma.
Mikoa mingine ni Katavi, Dar es Salaam,Tanga, Ruvuma, Mtwara, Tabora, Lindi, na Shinyanga.
Mkisi alizitaja baadhi ya klabu zenye sifa ya kushiriki uchaguzi kuwa ni Uhamiaji Dar es Salaam, Magereza, Tamisemi Dodoma, Filbert Bayi, Polisi Dar, Polisi Mbeya, Hamambe ya Mbeya, Mgulani, JKT Mbweni, Tumbaku Morogoro, Umoja Queens, Mapinduzi Dodoma, Bandari Dar es Salaam na JKT Ruvu.
“Maandalizi ya uchaguzi yanaendelea vizuri,” alisema Mkisi.
Wagombea wa nafasi ya uenyekiti katika uchaguzi huo ni Anna Kibira, Shy Rose Bhanji huku Zainabu Mbiro na Agnes Mangasila wakiwania nafasi ya makamu mwenyekiti na Agnes Khatibu akiwania kuwa mweka hazina).
Waliochukua fomu kuwania ujumbe ni Yasinta Silvester, Mwajuma Kisengo, Ana Mary Protasi, Rose Kisiwa, Judith Ilunda, Hilder Mwakatobe, Penina Igwe, Asha Sapi na Fortunata Kabeja.
Comments
Loading…