Barcelona wana mahitaji makubwa ya kusukwa upya kwa kikosi chao, lakini kutokana na changamoto ya upatikanaji wa fedha, inamaanisha itakuwa vigumu kama si kutowezekana kabisa.
Walipocharazwa mabao 4-1 nyumbani kwao na Paris Saint-Germain (PSG), Barca walionekana wazi kwamba wanapwaya na jambo linatakiwa kufanyika kurekebisha hali hiyo. Hii si aina ya Barcelona tuliowazoea, hasa wakiwa kwenye ngome yao ya Nou Camp.
Wakiwa wameketi kwenye majukwaa wakikunja nyuso zao kwa masikitiko ya mwenendo wa mchezo na matokeo, walikuwa wakongwe na mashujaa wa Barca, Sergio Busquets na Gerard Pique, wakichoshwa na jinsi Kylian Mbappe alivyokuwa akiwanyanyasa watu na hata kufunga mabao matatu, yaani hat-trick.
Mbappe na wenzake wamewaonesha wachezaji wa Barca, benchi la ufundi, viongozi na hata washabiki tofauti kubwa iliyopo baina ya timu mbili hizi kubwa za Ulaya. Uwanjani waliokuwa wamebaki wakicheza ni pamoja na Lionel Messi.
Alitengeneza na kufunga penati iliyowapa bao pekee, ikiwaacha na mlima mrefu na uliochongoka wa kupanda ugenini Ufaransa baadaye. Bao hilo liliwafanya Barca kuwa mbele kwa bao hilo, lakini PSG walipoweka gia zao na kuanza kukimbizana kwenye ‘double road’ bao lile lilionekana kutokuwa na maana kabisa.
Ilikuwa mara ya pili kwa Barcelona kupoteza mechi nyumbani kwenye michuano ya UAFA tangu 2013 na mara ya sita tu katika mechi 278 za Ulaya na walipoteza kwa tofauti ya mabao walau matatu.
Kocha wa Barca, Ronald Koeman ambaye ni mchezaji wao wa zamani alibadili mfumo kutoka 4-2-3-1 kwenda 4-3-3 ikaonekana mabadiliko chanya kidogo. Hawa ni watu ambao wamekuwa na ushindi mara 10 na sare mbili kwenye mechi zao 12 zilizopita za Ligi Kuu ya Hispania – La Liga.
Waliingia uwanjani wakiwa wanajiamini, kwa mtiririko wa matokeo hayo, Messi akiwa pia mtamu kwa mabao 10 kwenye mechi 10, akirudia kwenye matawi yake ya juu. Washabiki walikuwa wengi kuwakaribisha wachezaji waliowasili kwa basi lao, vyombo vya habari vikiwa vimezungumzia sana kichapo cha 6-1 walichopata PSG kwenye mtoko wao wa mwisho hapo Nou Camp.
Kumbe bora wangetazama na kukumbukia kisago cha 8-2 kutoka kwa Bayern Munich kwenye robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Ulaya (UCL) kiangazi kilichoopita. Laiti kama mchezaji wa zamani na ‘pacha’ wa Messi, Neymar na Angel Di Maria wangekuwa timamu kimwili, si ajabu kisago kama hicho cha Bayern kingejiri tena.
Mbappe alikuwa wa kimataifa hasa, akiwaonesha Barca aina ya wacheaji wanaohitaji, kwani lazima kikosi kitengenezwe upya ili kurudisha makali ya enzi zile ya akina Carles Puyol, Xavi na Andres Iniesta walioondoka karibuni na kuacha alama kubwa hapo.
Rais wa zamani wa Barca, Josep Maria Bartomeu alijaribu kumsajili Marco Verratti, aliyekuwa mzuri kwenye kiungo lakini PSG walizuia muvu zake. Washabiki wamebaki kwenye sintofahamu iwapo Messi naye ataondoka muda wake ukimalizika na kwamba nani atajaza pengo lake.
Mtiti wa Machi 10 kule Parc des Princes mtoto hatatumwa dukani, maana nani ataweza kuwazuia PSG? Ina maana huenda Barcelona wakatolewa UCL kabla ya robo fainali kwa mara ya kwanza tangu msimu wa 2006/7.
“Nitakuwa nakudanganya lakini ukweli ni kwamba kucheza ugenini baada ya kufungwa 4-1 nyumbani uwezekano wa kushinda na kuvuka ni mdogo sana,” anakiri Koeman.
Kwa hali ilivyo, kuna mahitaji makubwa ya wachezaji wapya wa kukisuka upya kikosi cha Barcelona, lakini kwa vile hakuna fedha, itabidi kuwatengeneza hao hao walio nao, maana hakuna jinsi.
Comments
Loading…