in , , ,

Bado tuna swali kwa Amunike ?

Hawezi kuonekana kama shujaa kwa wengi kwenye hii furaha ambayo tuko nayo kwa sasa sisi Watanzania ndani ya mioyo yetu.

Ushajaa wake utakuja wapi wakati asilimia kubwa ya watu hawamkubali sana? Asilimia kubwa ya watu hawapendezwi na aina ya ufundishaji wake.

Kuna wakati mtu yuko tayari kusema tumeshinda kwa uwezo wa wachezaji wetu kujituma, hamasa kubwa iliyokuwa ndani ya uwanja na siyo kwa sababu ya mbinu za mwaliku Emmanuel Amunike.

Haya yote yanakuja ili kuonesha tu kuwa huyu bwana hana uwezo wa kuifundisha timu yetu ya Taifa kabisa na hastahili kabisa.

Doa lilianza kuangukia kwenye nguo ya Emmanuel Amunike katika mechi dhidi ya Cape Verde tuliyofugwa goli 3-0.

Mechi ambayo aliweka wachezaji wengi ambao wana sifa kubwa ya kujizuia , wengi walidhani kwa sababu tu tulikuwa ugenini.

Kwenye mechi dhidi ya Lesotho aliwapanga wachezaji kwenye nafasi ambazo zilionekana siyo zao kabisa.

Hali ambayo ilisababisha wao wachezaji kufanya makosa binafsi na kufungwa kwenye mechi ambayo tulikuwa na hamu ya kushinda kweli kweli ili kujihakikishia moja kwa moja kufuzu.

Tukafungwa pale Maseru, lawama zikawamngukia Emmanuel Amunike , hiki ni kitu cha kawaida sana kwa sababu kocha ndiye hubeba zigo la kinyesi.

Mechi ya Uganda ilikaribia, mechi ambayo sisi tulikuwa tunatakiwa kushinda na kuiombea mabaya Lesotho.

Ki vyovyote vile sisi wazo letu la kwanza ni kushinda tu kabla ya wazo jingine lolote lile. Tulianza kumtukana Emmanuel Amunike kwenye uteuzi wake wa kikosi.

Aliacha baadhi ya wachezaji ambao kwa kiasi kikubwa watu wengi walikuwa wanaona wanastahili kuwepo ndani ya kikosi cha timu ya Taifa.

Utaanzaje kumwacha Ibrahim Ajib kwenye kikosi chako na watu wakakuelewa vizuri?. Yani mchezaji anayeongoza kwa kupiga pasi nyingi za mwisho ndani ya ligi kuu ?

Akaachwa?, tena kwenye mechi ambayo unatakiwa kushinda, mechi ambayo unatakiwa kutengeneza nafasi nyingi za magoli ndani ya uwanja ?

Hakika huwezi kueleweka kirahisi sana. Lakini Emmanuel Amunike alikiamini kichwa chake peke yake, akakielewa kichwa chake na kuamua kutembea nacho kama rafiki peke yake anayemwamini.

Unajua kwanini alifanya hivi ?, jibu ni dogo tu. Alifanya hivi kwa kuamini taaluma yake. Aliamini kile ambacho alikuwa anakiamini.

Aliamini kwenye aina ya mfumo ambao alikuwa anautumaini. Aliamini kwenye mbinu ambazo alikuwa anaziwaza kuzitumia siku ya mechi.

Kwa hiyo ndiyo maana akaamua kuwa na wachezaji ambao wangekuwa sahihi kwenye mfumo wake na mbinu zake alizokuwa anazifikiria kuzitumia ndani ya mchezo huu wa Uganda.

Ndiyo maana kichwa chake peke yake alibaki kukiamini kwenye aina ya wachezaji ambao alikuwa akiwahitaji.

Kwenye mechi ya Uganda akaonesha kitu tofauti na matazamio ya wengi. Akatumia mbinu tofauti kabisa ambazo zilifanikishwa na jeshi lake imara.

Uliwaona Taifa Stars walivyokuwa wanatengeneza mashambulizi ?. Walikuwa wanatumia eneo la pembeni sana.

Wachezaji wa pembeni ndiyo walikuwa wanahakikisha wanaleta mashambulizi langoni mwa timu ya Uganda.

Kuanzia mabeki wa pembeni Hassan Kessy na Gadiel Michael ambao walikuwa wanasaidia kuipandisha timu eneo la mbele.

Pia wachezaji wake wa mbele walikuwa walikuwa wanatawanyika pembeni kutanua uwanja. Mfano, John Bocco hakuwa anasimama eneo la katikati ya kumi na nane.

Yeye alikuwa anapanua uwanja kwa kuja pembeni mwa uwanja hasa hasa eneo la kulia mwa uwanaja mwisho wa siku John Bocco alikuwa na madhara.

Simon Msuva naye alikuwa anakuwa pembeni sana hasa eneo la kulia. Vivo hivo kwa Fareed Mussa ambaye na yeye alikuwa anakaa pembeni mwa Uwanja muda mwingi.

Eneo ambalo alilokuwa anakaa Fareed Mussa kuna wakati Mbwana Samatta alikuwa anakuja kuongeza nguvu.

Sasa hapo ndipo utaona maana halisi ya Emmanuel Amunike kuita aina ya wachezaji ambao alikuwa anawaamini kuwa wanaweza kuendana na mfumo wake.

Kwanini nasema hivo ? , aina ya wachezaji wengi ambao walikuwa wanalalamikiwa kutoitwa kwenye timu ya Taifa ni wachezaji ambao walikuwa hawana uwezo wa kuendana kwenye mfumo huu.

Hapa ndipo ushujaa wa Emmanuel Amunike ulipoibuka. Ila watu hawawezi kuuona ushujaa huu kwa sababu tu hawataki tu kuuona.

Hawataki kabisa kuamini kuwa Emmanuel Amunike amefanya sisi twende Misri. Hawataki kabisa kusikia hiki kitu.

Wataongea vingi sana ili tu kuupindisha ukweli, ila ukweli una baki pale pale kuwa Emmanuel Amunike ndiye mtu wa kwanza kutupeleka Misri.

Report

Written by Martin

Martin Kiyumbi ni mchambuzi wa habari za michezo na mbunifu wa maudhui.

Martin Kiyumbi amewahi kufanya kazi za uchambuzi kwenye vituo mbalimbali vya habari kama Tanzaniasports (tovuti ya habari za michezo ), Jembe FM , Radio Free Africa na TVE.
Martin Kiyumbi anapatikana kwenye e-mail ya [email protected]

What do you think?

71 Points
Upvote Downvote
Tanzania Sports

Simba endeleeni kukubali kuitwa “underdogs”

Tanzania Sports

Karibu kwenye ulimwengu wa KINDOKI