in , ,

Karibu kwenye ulimwengu wa KINDOKI

Ulimwengu ambao watu wengi waliudharau. Hawakutaka kabisa kuukubali kama ndiyo sehemu sahihi kwao wao kuishi.

Ulimwengu ambao watu wengi hawakutaka kabisa kuuweka karibu na macho yao. Utawekaje karibu na macho yako kitu ambacho kinakuumiza?

Bila shaka ni kitu kigumu sana kuvumilika. Kwao wao waliamini huyu ni mtu ambaye alikuwa na bahati kubwa sana ya kuwepo Yanga.

Na kuna wakati uwepo wake ulihusishwa kwa kiasi kikubwa na Uraia unaofanana na kocha wake mkuu wa Yanga, Mwinyi Zahera.

Yani kwa kifupi kabisa, Mwinyi Zahera alikuwa anamfanya Klaus Kindoki aendelee kuwepo Yanga na siyo kiwango chake.

Hivi ndivo watu walivyokuwa wanawaza, huwezi kuwakataza kuwaza hivo hata siku moja kwa sababu ya mtazamo wao ambao walikuwa wanautazama.

Waliona hivyo, wakaona Klaus Kindoki hafai hata kidogo kuvaa jezi ya mtaa wa Jangwani. Kwao wao kuna aina ya makipa ndiyo ambao walikuwa wanastahili.

Utawezaje kuwaaminisha watu kuwa Klaus Kindoki ndiye golikipa wa Yanga kwenye timu ambayo Juma Pondamali Mensah amewahi kudakia ?

Utawezaje kuwaaminisha watu kuhusu uwepo wa Klaus Kindoki kwenye timu ambayo ina mataji 27 ya ligi kuu ?

Timu kongwe, timu kubwa hapa Tanzania. Timu yenye presha kubwa ndani na nje ya uwanja ?. Timu ambayo inaamini imezaliwa kwa ajili ya kushinda tu ?

Yani haki zote za ushindi kwenye kila mechi zililetwa kwa ajili ya Yanga tu. Hiki ndicho kitu cha kwanza ambacho kilimfanya Klaus Kindoki kuonekana siyo kipa wa kuvaa jezi ya Yanga.

Klaus Kindoki amefanya kosa katika mechi za mwanzoni akiwa na Yanga. Kufanya kosa katika mpira wa miguu ni kitu cha kawaida sana.

Kwa sababu tu mpira ni mchezo wa makosa, yani makosa yamewekwa ndani ya mpira wa miguu ili tupate bingwa na ambaye anashindwa.

Mpira wa miguu haujawahi kuumbwa uwe sahihi kabisa katika sayari hii. Umeumbwa kwa ajili ya makosa.

Kwa bahati mbaya kabisa Klaus Kindoki alifanya makosa mwanzoni kabisa. Yani kipindi ambacho anakuja Yanga.

Kipindi ambacho kila jicho la mwanayanga linamtazama yeye kwa shauku kubwa kutaka kujua kama anaweza kubwa sahihi kwenye timu yao.

Lakini kwa bahati mbaya kabisa akaanza vibaya. Kindoki likawa jina rasmi kwa mtu yeyote ambaye anafanya makosa.

Presha ilikuwa kubwa sana ndani yake. Mashabiki wanataka matokeo mazuri ndani ya uwanja lakini kwa bahati mbaya yeye anafanya makosa.

Makosa ambayo yalimtolea kabisa kutokujiamini ndani ya uwanja. Hata kiwango chake kikawa kinaonekana cha kawaida sana.

Kwa sababu tu alikuwa hawezi kujiamini tena kubwa anaweza kufanya jambo kubwa akiwa anailinda Yanga.

Ilimchukua muda mrefu kumjenga Klaus Kindoki mpaka kufikia hatua ya yeye kuweza kufanya vizuri tena baada ya kutoka kwenye Giza la makosa.

Tabia moja ambayo huwa siyo nzuri kwa mashabiki wa mpira wa miguu, na ndiyo tabia ambayo mashabiki wengi hawajawaji kuzaliwa nayo ni wao kutokuwa wavumilivu.

Neno uvumilivu halipo kabisa kwenye akili na vinywa vyao. Yani akili zao zikiona makosa, vinywa vyao hutanuka na kumkataa aliyefanya makosa.

Mashabiki wengi hawana nafasi ya pili kwenye mpira wa miguu. Kwao wao wana nafasi moja tu. Yani hawawezi kukupa nafasi ya pili.

Kwao wao ukikosea Mara moja tu ndiyo huja na hitimisho kuwa wewe ni mbovu. Na hawataishia kusema hivo tu kwenye vinywa vyao.

Wataendelea kuonesha kutokukuamini kila uchwao. Kila kocha anapokuamini wao huja tofauti kabisa na kutokukuamini kabisa.

Hapa ndipo huwa mwanzo wa kupoteza vipaji vingi kwa sababu tu ya kuuliwa kisaikolojia. Hiki kilikuwa kinaenda kumtokea Klaus Kindoki.

Alikuwa anaenda kuuliwa kisaikolojia na mashabiki. Ilifika hatua mashabiki wa Yanga wakawa hawamwamini kabisa kila alipokuwa anapewa nafasi.

Walishindwa kufahamu kuwa wao walikuwa wana nafasi kubwa sana ya kumjenga Klaus Kindoki kwa kumfanya awe imara hata kama anapitia magumu.

Hawakutaka kabisa kumtelekeza Klaus Kindoki, lakini hicho ndicho kitu ambacho walifanya. Walimtelekeza, mwanzoni alionekana kuteteleka.

Lakini alituliza akili, akaingiza kujiamini ndani yake , akawa anaamini kabisa anaweza kukabiliana na hiki kitu ambacho kinaonekana kigumu.

Taratibu akaanza kurejesha kujiamini kwake ndani ya mikono yake. Mwisho wa siku Klaus Kindoki akawa mchezaji muhimu ndani ya kikosi cha Yanga.

Mechi ya hatua ya kumi na sita bora dhidi ya Namungo Fc yeye ndiye aliyeilinda ipsavyo Yanga na kuipeleka katika hatua ya robo fainali.

Jana kailinda Yanga ipasavyo katika mechi ya robo fainali dhidi ya Alliance. Ndiye aliyepangua penati ambayo Yanga iliipeleka nusu fainali. Klaus Kindoki anawakaribisha Yanga kwenye ulimwengu wake rasmi.

Report

Written by Martin

Martin Kiyumbi ni mchambuzi wa habari za michezo na mbunifu wa maudhui.

Martin Kiyumbi amewahi kufanya kazi za uchambuzi kwenye vituo mbalimbali vya habari kama Tanzaniasports (tovuti ya habari za michezo ), Jembe FM , Radio Free Africa na TVE.
Martin Kiyumbi anapatikana kwenye e-mail ya [email protected]

What do you think?

71 Points
Upvote Downvote
Tanzania Sports

Bado tuna swali kwa Amunike ?

Tanzania Sports

Hii ni BARCA ndani ya miaka 10 iliyopita