in , , ,

Arsène Wenger: UJINGA NI MAAMUZI

*Miaka 14 imepita, miaka ya mateso furaha ikiwa mbali sana na mashabiki
wa Arsenal*

Miaka ambayo imekuwa na hadithi nyingi za kuhuzunisha na kuzaririswa
kwa timu nzima ya Arsenal.

Hakuna furaha, amani ni finyu na imani juu ya Arsene Wenger imepotea
kwa mashabiki wa Arsenal.

Hakuna shabiki wa Arsenal anayefurahia kuona manyanyaso na mateso
wanayoyapata kutoka kwenye timu mbalimbali kubwa.

Hali ambayo inawafanya wengi wasimuunge mkono Arsene Wenger na
wachache kuwa naye ingawa kwa shingo upande.

Ni kocha mwenye historia ndefu na kubwa ndani ya klabu ya Arsenal
akiwa kama kocha mwenye mafanikio makubwa ndani ya klabu ya Arsenal
baada ya George Graham.

Alipata mafanikio kipindi kile ambacho mpira haujawa kama sasa.

Kipindi ambacho waweza mvumilia mchezaji na kumtengeneza kuwa mtu
mkubwa huku ukiendelea kufanya vizuri.

Ndiyo maana aliwavumilia kina Henry na kuwatengeneza kutoka kuwa
washambuliaji wa pembeni mpaka kuwa washambuliaji tishio wa kati.

Mesut Özil, Granit Xhaka na Laurent Koscielny baada ya kuchezea kichapo cha 4-0 pale Anfield

Ni Arsene Wenger huyu ambaye alituletea Henry ndiye aliyetuletea bomba
la kutoa pasi za mwisho ( Cesc Fabregas ).

Hakuna shaka Viera alikuwa mkubwa sana mpaka akawa anaheshimika
kipindi cha Arsene Wenger.

Arsene Wenger alituaminisha ana uwezo wa kufanya kitu kikubwa ambacho
hakuna kocha yoyote anayeweza kufanya hivo, ndiyo maana alifanikiwa
kumaliza ƙmsimu akiwa hajapoteza hata mechi moja ( Invincible) ,
aliende mpaka mechi 49 bila kufungwa.

Alipewa heshima akashujudiwa kama mtu sahihi wa kulinda ghala la
silaha pale Arsenal.

Siku zikakimbia , zikaturuhusu kuyasubiri yajayo, yajayo ambayo
yalikuwa machungu zaidi kwa mashabiki wa Arsenal.

Kilikuwa kilio kikubwa kwa Arsenal kupoteza mchezo wa fainali wa UEFA
dhidi ya Arsenal mwaka 2006.

Kipigo hiki kilikuja na balaa kubwa sana kwenye kikosi cha Arsenal.
Kipigo kilichoendana na ujenzi mpya wa uwanja wa Arsenal ( Emirates).

Iliwalazimu kuhama Highbury, sehemu ambayo ilikuwa yenye mafanikio
kwao. Na ndiyo ikawa mwanzo wa wao kuyakimbia mafanikio na kuyafuta
matatizo.

Klabu ilianza kuishi katika bajeti finyu, walijima ili wajenge uwanja.

Waligeuka kuwa soko la kuuza wachezaji nyota.

Silaha walizokuwa wanazitengeneza zilikuja kugeuka kuwa silaha za kuwauliwa wao.

Vipigo vikubwa vilikuwa rafiki wa Arsenal. Ilikuwa kawaida kwa timu
kufungwa goli 8, 6, 5 kwa sababu tayari walikubali kuchagua kuwa
wadhaifu.

Udhaifu ambao ulienea kwenye kila eneo la timu ya Arsenal.

Kila idara ikawa dhaifu, idara ya matibabu haikuwa imara hali ambayo
ilisababisha kutokuwa na suluhisho sahihi la majeruhi ya wachezaji wa
Arsenal.

David Dein aliondoka, mtu pekee ambaye alikuwa na uhakika wa kumleta
mchezaji yoyote anayetakiwa na Arsene Wenger.

Majukumu yote ya kuhangaika sokoni kutafuta wachezaji akabaki nayo
Arsene Wenger kwa sababu aliamua kuwa hivo.

Maisha ni maamuzi, unapoamua kuwa mtu wa aina fulani ni sawa tu, ndiyo
maana Arsene Wenger hakuangalia umri wake akajitishwa kila aina ya
jukumu.

Ikawa yeye ndiye anayeratibu urefu wa nyasi za uwanja wa mazoezi,
akawa anaratibu mpaka mambo ya jikoni.

Majukumu yakawa mengi yakamzidi akaamua kuachana na mkewe, kuachana na
mkewe ikawa jambo la kawaida kwake kiasi kwamba akawa anaruhusu nyota
wa timu yake kuondoka.

Alimwachia Fabregas kwenda Barcelona, hakuwa muoga kumuona Nasri,
Clichy, Adebayor na Sagna kwenda Manchester City.

Silaha aliyokuwa anaitegemea aliipeleka Manchester United, Van Persie
akawaua wao.

Wakabaki hawana cha kufanya zaidi ya kutengeneza timu kila wakati.

Wakati ambao unaona timu inaimarika ndipo hapo timu inabomolewa.

Leo hii unamleta Lacazzete ukiamini unategeneza kikosi bora, lakini
unaruhusu kuondoka kwa wachezaji nyota wa kushilikiana na hawa
unaowaleta .

Unaanzaje kukubali kumwachia Oxlaide Chamberline mtu ambaye kwa
kiasi kikubwa ameingia vizuri kwenye mfumo wako wa timu?

Report

Written by Martin

Martin Kiyumbi ni mchambuzi wa habari za michezo na mbunifu wa maudhui.

Martin Kiyumbi amewahi kufanya kazi za uchambuzi kwenye vituo mbalimbali vya habari kama Tanzaniasports (tovuti ya habari za michezo ), Jembe FM , Radio Free Africa na TVE.
Martin Kiyumbi anapatikana kwenye e-mail ya [email protected]

What do you think?

71 Points
Upvote Downvote
Tanzania Sports

USHINDI WA CONTE ULIKUWA BAHATI AU UWEZO ?

Tanzania Sports

IDADI YA WACHEZAJI WALIOSAJILIWA TANGIA DIRISHA LIFUNGULIWE NA KUFUNGWA LEO