Ligi Kuu ya England (EPL) imeanza na zogo kubwa ni kichapo walichopokea Arsenal cha mabao 3-1 nyumbani, kutoka kwa Aston Villa.
Juu ya hilo, ni kushindwa kwa klabu hiyo kubwa kusajili nyota wapya, licha ya ahadi kemkem kwamba walishajiandaa kutumia kitita kuongeza nguvu, hasa kwenye ushambuliaji.
Hakuna wasiwasi kwamba Arsene Wenger ni mmoja wa makocha bora kabisa ambao EPL imepata kuwa nao, lakini mkakati wake unaonekana kupitwa na wakati.
Ni kana kwamba anaona kufanya usajili mkubwa na wa kutikisa kama kushindwa na si mafanikio, na ndilo linaweza kuwa jibu pekee la yeye hadi sasa kusajili tu kijana mdogo Yaya Sanogo kutoka Auxerre badala ya nyota wanaotakiwa.
Bodi ya Wakurugenzi ya Arsenal imetamka wazi kwamba wana fedha za kusajili na walikuwa tayari kupigana vikumbo na klabu nyingine kubwa kwenye usajili, lakini siku zinayoyoma hakuna vitendo.
Pauni zote milioni 70 zilizosemwa zimetengwa pamoja na nyingine zilizopatikana baada ya kuuza wachezaji kadhaa na wengine kutolewa kwa mkopo zimewekwa kibindoni tu.
Washabiki wa Arsenal tayari wamebwatuka kwamba hawataki tena Mfaransa huyo aongezewe muda, pindi mkataba wake utakapomalizika mwakani.
Hawawezi kuridhika na madai ya Wenger kwamba walitaka kumsajili Gonzalo Higuain, Luis Suarez na hata Wayne Rooney, kwa sababu dili kama la Higuain ilielekea wazi waliliacha likayeyuka akachukuliwa na klabu nyingine.
Suarez inaeleweka msimamo mkali wa mmiliki na viongozi wa Liverpool, lakini Arsenal walitakiwa kujua asingeachiwa kirahisi, hivyo wangeangalia na kukomaa kupata nyota wengine.
Walifanya mzaha tu kwa wengine kama akina Bernard na Luiz Gustavo – ambapo Gustavo kutoka Bayern Munich alisema wazi alitaka kujiunga Arsenal, lakini Wenger akakunja mikono yake badala ya kuinyoosha kumpokea.
Wapinzani wao waliomaliza ligi juu yao wote wana vikosi imara lakini wameongeza wachezaji kadhaa au hata mmoja kama Manchester United. Waliomaliza nyuma yao pointi moja, Tottenham Hotspur wamejiimarisha vilivyo, na tusishangae msimu huu wakawatimulia vumbi mahasimu wao hao wa London kaskazini.
Spurs wamewasajili mpachika mabao mahiri, Roberto Soldado na kiungo Paulinho na kuna mwingine pia wanadaiwa kukaribia kuwazidi kete Arsenal.
Wachezaji wengine waliokuwapo tayari kuingia Emirates ni kama Victor Wanyama wa Celtic aliyekwenda Southampton kutokana na ubahili wa Arsenal, Marouane Fellaini wa Everton, Michu wa Swansea na hata Ashley Williams na Asmir Begovic.
Kila fursa inapotokea kwa Arsenal kuchukua wachezaji hao, wanajidai wako bize na jambo jingine kisha akishachukuliwa au msimu wa usajili ukiisha utasikia wakisema wamewakosa kwa bahati mbaya.
Msimu uliopita walisajili wachezaji wengi dakika za mwisho, wakiokota wachezaji wa kweli na magarasa, na sasa muda unakatika kidogo kidogo, tunaona Wenger akiwalaumu wanahabari eti kwamba wamepata walichotaka kwa timu yake kuchabangwa na Villa. Sababu gani hii!
Kimsingi timu kama mabingwa watetezi, Manchester United, hawahitaji kuongeza mchezaji, lakini wamehangaika vilivyo kumpata Cesc Fabregas, Leighton Baines Marouane Fellaini japo wamekataliwa. Alex Ferguson kabla ya kuondoka aliwapatia Wilfred Zaha na wanakataa kumwachia Rooney – wanacho kikosi kilichotwaa ubingwa na nyongeza ya Zaha.
Chelsea wamesheheni vipaji vingi, mchanganyiko wa chipukizi na wakongwe lakini bado wameongeza wachezaji wapya. Manchester City wamesajili fowadi kali kabisa, itakuwaje Arsenal waridhike wakati hawakupata kuziba mapengo ya Patrice Vieira wala Robin van Persie?
Wenger anatamba na pauni milioni karibu 100 za usajili mfukoni, anaye Laurent Koscielny aliyezuiwa kucheza mechi baada ya kadi nyekundu, Bacary Sagna na Kieran Gibbs wakiuguliwa majeraha, bado anasema anawania taji?
Tatizo la Arsenal ni kwamba lazima wacheze vizuri sana kushinda mechi zao, lakini waelewe tu kwamba United, Chelsea na City wanaweza kushinda mechi hata wasipocheza vizuri, maana wachezaji wao wapo imara kisaikolojia na wanahimili shinikizo.
Arsenal bado hawako hivyo, si ajabu hata nafasi ya nne wanayoililia kila mwaka wakaikosa safari hii, maana wanatakiwa kununua aina ya wachezaji wenye sifa kama wa timu hizo tatu, lakini Wenger anaonekana kukwepa na kufikiri kivingine kabisa.
Bado Arsenal wanatakiwa kusajili mchezaji mmoja au wawili wa hadhi ya juu, lakini kwa hali ilivyo, watabaki kuwajaribu chipukizi wao na kujidai kwamba wanacho kikosi cha kufaa.
Wenger anatakiwa aelewe kwamba thamani haipo katika ile ada ya uhamisho, bali lile kabati lenye vikombe kila msimu unapomalizika. Yeye amehifadhi fedha miaka nenda rudi, na hiyo si kazi ya kocha.
Alichomoa kuwasajili Higuain na Gustavo kwa sababu ya fedha. Ni kweli pauni zaidi ya milioni 30 ni nyingi kwa Higuain, lakini wanapokosa mbadala wake maana yake ni majanga kwa klabu na safari nje ya nne bora inaelekea kuanza mapema kabisa, isipokuwa kama watarekebisha mambo.
Comments
Loading…