*Spurs wamkamia Paulinho

Msimu wa usajili umeanza kwa kasi, ambapo mahasimu wa London Kaskazini, Arsenal na Totenham Hotspur wanajiimarisha.
Wakari Arsenal walitangaza kumnasa na kumsajili mpachika mabao kinda wa Auxerre ya Ufaransa, Yaya Sanogo, Spurs wanaweka rekodi kwa kumchukua Jose Paulo Bezerra Maciel Junior ‘Paulinho’ kwa pauni milioni 17.
Arsene Wenger, kama kawaida yake ameelekeza macho kwao Ufaransa kwa kuendeleza sera zake za kusajili vijana, kwa kumchukua Sanogo mwenye umri wa miaka 20.
Sanogo anaingia Emirates akiwa mchezaji huru, baada ya mkataba wake na klabu hiyo ya Ligue 1 kumalizika. Amefunga mabao 11 katika mechi zake 24 na Auxerre, na kwa sasa yupo kwenye kikosi cha Timu ya Taifa ya Ufaransa chini ya miaka 20 nchini Uturuki.
Amefunga mabao mawili kwenye mechi za makundi na kusaidia timu yake kuingia kwenye 16 bora, ambapo Mfaransa Wenger anasema Sanogo ni chaguo bora kijana kwa Washika Bunduki wa London na kwamba ataendeleza ukali wake akiwa nao. Alijiunga Auxerre akiwa na umri wa miaka 14.
Kwenye nyumba ya jirani, Spurs wanatoa dau la pauni milioni 17 kwa ajili ya kumnasa kiungo wa Brazil anayechezea Corinthians Paulinho, ambapo mchezaji mwenyewe ameonesha nia ya kuhama.

MOYES NA ROONEY KUAMUA HATMA

Yaya Sanogo
Yaya Sanogo

Wakati hayo yakijiri, kocha mpya wa Manchester United, David Moyes ameanza kazi na ana mtihani wa kwanza mgumu.
Mtihani huo ni kujadiliana na mpachika mabao, Wayne Rooney juu ya hatima yake katika klabu hiyo mabingwa wa soka England.
Rooney ameshaomba zaidi ya mara moja kuondoka United, na ilikuwa chini ya kocha Alex Ferguson aliyestaafu mwishoni mwa msimu uliopita.
Moyes ana historia kubwa na Rooney, kwa sababu ndiye alimsajili na kumkuza Everton, kabla ya kunyakuliwa na Mashetani Wekundu hao.
Hata hivyo, Moyes alikorofishana na Rooney kabla hajahamia United, na imetokea sasa wanakutana tena. Pamoja na mambo mengine, Moyes alimsema vibaya Rooney kwamba alikuwa akila hovyo na kuongezeka uzito hivyo kushindwa kucheza vizuri.
Timu kadhaa zimeeleza kutaka kumchukua Rooney anayechezea pia timu ya taifa ya England, zikiwamo Arsenal ambao hata hivyo kwa kukaribia kumchukua Gonzalo Higuain wa Real Madrid, huenda ikaacha mbio kwa Rooney. Chelsea na Paris Saint-Germain zinaelezwa kumtaka pia.
Kocha msaidizi wa zamani wa United, Mike Phelan anasema kwamba ni wazi Rooney anataka changamoto mpya na tofauti kwa kuchezea klabu nyingine. Arsenal wanaelezwa kumsaka pia Fernando Torres anayeelekea kuondoka Chelsea.

GOLIKIPA MKONGWE FULHAM AONDOKA

Baada ya kuwatumikia Fulham tangu 2008, golikipa mkongwe, Mark Schwarzer anaondoka klabuni hapo, baada ya kukataa mwito wa kusaini mkataba mwingine.
Alijiunga akitokea Middlesbrough na sasa ametimiza miaka 40, lakini anaendelea kuchezea timu ya taifa ya Australia.
Huyu ni mchezaji wa kwanza kutoka ng’ambo kucheza zaidi ya mechi 500 nchini Uingereza. Fulham wamemsajili golikipa wa Kidachi,
Maarten Stekelenburg kutoka klabu ya AS Roma ya Italia mwezi uliopita, na ndiye atachukua nafasi ya Schwarzer.

Paulinho
Paulinho

BRAZIL YAREJESHA HESHIMA NYUMBANI

Timu ya soka ya taifa ya Brazil imerejesha kiwango chake na heshima ya soka katika taifa hilo la Samba.
Ushindi wao mkubwa wa mabao 3-0 dhidi ya Hispania Jumapili hii katika fainali ya Kombe la Mabara ulitosha kuweka hai matumaini yao ya kufanya vyema kwenye Kombe la Dunia 2014 linalofanyika nchini mwao.
Hispania waliloa mbele ya kocha wao mkongwe, Vincent Del Bosque aliyejipatia heshima kubwa kwa kutwaa makombe mengi makubwa ya kihistoria, ikiwa ni pamoja na Kombe la Dunia la Kombe la Ulaya.
Ushindi wa Brazil dhidi ya Hispania ulivuruga heshima ya Wahispania hao, na pia kuendeleza machungu baada ya klabu zao mbili, Barcelona na Real Madrid kuchapwa kwa idadi kubwa ya mabao na klabu za Ujerumani – Bayern Munich na Borussia Dortmund kwenye nusu fainali za Klabu Bingwa Ulaya hivi karibuni.
Hata hivyo, kwa mara nyingine mshambuliaji wa Chelsea, Fernando Torres aliibuka shujaa, kwa kuwa mpachika mabao bora zaidi akifuatiwa na Fred na Neymar wa Brazil.

TIKETI KOMBE LA DUNIA BEI RAHISI

Wananchi wengi wa hali ya kawaida wanaweza kupata fursa ya kuona mechi za Kombe la Dunia 2014, kwa sababu bei ya tiketi zake ni rahisi zaidi.
Katibu Mkuu wa Shirikisho la Soka Duniani (Fifa), Jerome Valcke anasema kwamba tiketi za asilimia 70 ya mechi zote zitakuwa rahisi kuliko ilivyokuwa kwenye mashindano yaliyopita.
Valcke na Rais wa Fifa, Sepp Blatter wamewasifu mabingwa hao wa Kombe la Mabara, Brazil kwa soka safi, lakini pia mipango bora ya urahisi wa tiketi, licha ya maandamano kupinga gharama kubwa za maandalizi.

 

 

Enhanced by Zemanta

Report

Written by Israel Saria

For the last 20 years I have been working as a football pundit. This experience has provided me with a very useful insight into football and the opportunity to carry out extensive research into the game including its players, the stadiums, the rules and tactics and I have also been grateful to meet a wide range of people connected to football in the UK, Tanzania, Germany .....

What do you think?

71 Points
Upvote Downvote

Comments

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Loading…

0

Kagame Cup, shwari….

Yanga, Simba mambo yaiva