in , , ,

Arsenal raha tupu kileleni


*Everton, Newcastle, West Ham washinda
*Mtoto hatumwi dukani Spurs na Man U

 
Vinara wa Ligi Kuu ya England (EPL), Arsenal wamefanikiwa kuendeleza wimbi la ushindi nchini Wales, baada ya kuwanyuka Cardiff City 3-0.

Arsenal wamefanikiwa kufungua pengo la pointi saba lakini wapinzani wao wa karibu, Liverpool na Chelsea wana mchezo mmoja mkononi.

Wakicheza ugenini, Arsenal walikuwa nusura wapate bao dakika ya kwanza kutoka kwa Jack Wilshere aliyefanya hivyo mechi iliyopita dhidi ya Southampton, lakini kiki yake iligonga mwamba.

Aaron Ramsey, mchezaji wa zamani wa Cardiff alirudi nyumbani katika hali tofauti na alifanikiwa kufunga mabao mawili bila kushangilia, likiwa ni la kwanza na la mwisho.

Mesut Ozil ndiye alikuwa mpishi wa bao la kwanza na la pili, ambapo la pili lilifungwa na kiungo aliyeingia kipindi cha pili, Mathieu Flamini.

Awali, Olivier Giroud alishindwa kufunga akidhani kwamba alikuwa ameotea, akabaki kuduwaa na mpira, kumwangalia mshika kibendera na alipogundua hajaotea alishachelewa na kukosa bao la wazi.

Katika mechi nyingine, Everton walipata ushindi mnono wa mabao 4-0 wakicheza nyumbani Goodison Park dhidi ya wagumu Stoke, ambapo mabao yalifungwa na Deulofeu, Coleman, Oviedo na Lukaku.

Ushindi huo umewafikisha Everton wanaofundishwa na Roberto Martinez katika nafasi ya nne.
Hii ni mara ya kwanza kwa Everton kuingia katika nne bora kwenye EPL msimu huu na wanaelekea watakuwa hatari kwenye mechi zijazo.

Newcastle nao walifanikiwa kupata ushindi dhidi ya timu ngumu ya West Bromwich Albion, ambapo waliwafunga kwa 2-1 kupitia mabao ya Yoan Gouffran na Mousa Sissoko wakati Chris Brunt akisawazisha lile la kwanza kabla ya kulia baadaye.

Ushindi huo umekuwa wa msaada mkubwa kwa vijana wa Alan Pardew, kwani wamepanda hadi nafasi ya tano kwenye msimamo wa ligi japkuwa anaweza kushushwa sana na timu nne zilizo nyuma yao kwa sababu hazijacheza mzunguko wao wa 13.

Hatimaye Big Sam, au kwa jina halisi Sam Allardyce alipata ushindi muhimu kwenye ligi hii, pale alipowafunga wachovu Fulham mabao 3-0 na kumwacha kocha wa Fulham, Martin Jol akiwa haamini kwa sababu yupo kwenye wakati mgumu na huenda akafutwa kazi

West Ham kwa ushindi huo wamefika nafasi ya 15 huku Fulham wakichechemea katika nagasi ya 18 – eneo la kushuka daraja.

Katika matokeo mengine, Aston Villa wakicheza nyumbani walibanwa na Sunderland na kwenda suluhu na Norwich wakafanikiwa kuwabamiza Crystal Palace 1-0.

Jumapili hii zinasubiriwa mechi kubwa, ambapo Tottenhum Hotspur waliofungwa mabao 6-0 na Manchester City wikiendi iliyopita, wanawakaribisha Manchester United kwao White Hart Lane katika mechi ya mchana.

Hull watakuwa wenyeji wa Liverpool huku Chelsea wakiwa Stamford Bridge na ugeni wa Southampton. Manchester City watatafuta faraja zaidi watakapocheza nyumbani dhidi ya Swansea kutoka Wales.

Report

Written by Israel Saria

For the last 20 years I have been working as a football pundit. This experience has provided me with a very useful insight into football and the opportunity to carry out extensive research into the game including its players, the stadiums, the rules and tactics and I have also been grateful to meet a wide range of people connected to football in the UK, Tanzania, Germany .....

What do you think?

71 Points
Upvote Downvote

Comments

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Loading…

0

Ronaldo namba moja Real Madrid

Gareth Bale aanza hat-trick